Mwanzo 4:1-16
Mwanzo 4:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Adamu akalala na Hawa mkewe, naye akapata mimba, akamzaa Kaini. Hawa akasema, “Nimepata mtoto wa kiume kwa msaada wa Mwenyezi-Mungu!” Halafu akamzaa Abeli nduguye. Abeli alikuwa mfugaji kondoo na Kaini alikuwa mkulima. Baada ya muda fulani, Kaini alimtolea Mwenyezi-Mungu sadaka kutokana na mazao ya shambani, naye Abeli akamtolea Mungu sadaka ya wazawa wa kwanza wa kondoo wake na nyama nono. Mwenyezi-Mungu akapendezwa na Abeli na tambiko yake, lakini hakupendezwa na Kaini wala na tambiko yake. Basi, Kaini akakasirika sana na uso wake ukakunjamana. Mwenyezi-Mungu akamwambia Kaini, “Kwa nini umekasirika, na kwa nini uso wako umekunjamana? Je, ukitenda vyema hutakubaliwa? Na usipotenda vyema, basi, dhambi inakuvizia mlangoni; inakutamani, lakini unapaswa kuishinda.” Baadaye, Kaini akamwambia Abeli nduguye, “Twende nje shambani” Basi, walipokuwa shambani, Kaini akamvamia Abeli nduguye, akamuua. Mwenyezi-Mungu akamwuliza Kaini, “Ndugu yako Abeli yuko wapi?” Kaini akamjibu, “Mimi sijui! Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” Mwenyezi-Mungu akasema, “Umefanya nini? Damu ya ndugu yako yanililia kutoka udongoni. Sasa wewe umelaaniwa! Hutailima tena ardhi yenye rutuba ambayo kama kinywa imeipokea damu ya nduguyo uliyemuua. Ukiilima ardhi haitakupatia tena mazao yake. Utakuwa mtu wa kutangatanga, asiye na makao maalumu duniani.” Kaini akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Adhabu yangu ni kubwa mno; siwezi kuistahimili. Leo umenifukuza kutoka ardhi yenye rutuba na mbali nawe. Basi, nitakuwa mtu wa kutangatanga, asiye na makao maalumu duniani, na yeyote atakayeniona ataniua.” Lakini Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Sivyo! Atakayekuua wewe Kaini atalipizwa mara saba.” Basi, Mwenyezi-Mungu akamtia Kaini alama ya tahadhari, ili yeyote atakayemwona asimuue. Kisha Kaini akaondoka mbele ya Mwenyezi-Mungu, akawa anaishi katika nchi ya Nodi, upande wa mashariki wa Edeni.
Mwanzo 4:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Adamu akamjua Hawa mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Kaini, akasema, Nimepata mtoto wa kiume kwa msaada wa BWANA. Akaongeza akamzaa ndugu yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima. Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA. Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana. BWANA akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana? Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, lakini yapasa uishinde. Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani]. Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye, akamwua. BWANA akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, kwani mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi. Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kutoka kwa mkono wako; utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na makao duniani. Kaini akamwambia BWANA, Adhabu yangu imeniwia kubwa, haichukuliki. Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na makao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua. BWANA akamwambia, Kwa sababu hiyo yeyote atakayemwua Kaini atalipizwa kisasi mara saba. BWANA akamtia Kaini alama, mtu amwonaye asije akampiga. Kaini akatoka mbele za uso wa BWANA, akakaa katika nchi ya Nodi, Mashariki mwa Edeni.
Mwanzo 4:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Adamu akamjua Hawa mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Kaini, akasema, Nimepata mtoto mwanamume kwa BWANA. Akaongeza akamzaa ndugu yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima ardhi. Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA. Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana. BWANA akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana? Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani]. Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye, akamwua. BWANA akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi. Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako; utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani. Kaini akamwambia BWANA, Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki. Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua. BWANA akamwambia, Kwa sababu hiyo ye yote atakayemwua Kaini atalipizwa kisasi mara saba. BWANA akamtia Kaini alama, mtu amwonaye asije akampiga. Kaini akatoka mbele za uso wa BWANA, akakaa katika nchi ya Nodi, mbele ya Edeni.
Mwanzo 4:1-16 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Adamu akakutana kimwili na mkewe Hawa, naye akapata mimba, akamzaa Kaini. Hawa akasema, “Kwa msaada wa Mwenyezi Mungu nimemzaa mtoto wa kiume.” Baadaye akamzaa Habili ndugu yake. Basi Habili akawa mfugaji, na Kaini akawa mkulima. Baada ya muda, Kaini akaleta baadhi ya mazao ya shamba ikiwa sadaka kwa Mwenyezi Mungu. Lakini Habili akaleta fungu nono kutoka baadhi ya wazaliwa wa kwanza wa mifugo yake. Mwenyezi Mungu akamkubali Habili pamoja na sadaka yake, lakini Mungu hakumkubali Kaini pamoja na sadaka yake. Kwa hiyo Kaini akakasirika sana, uso wake ukawa na huzuni. Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Kaini, “Kwa nini umekasirika? Kwa nini uso wako una huzuni? Ukifanya lililo sawa, je, hutakubalika? Lakini usipofanya lililo sawa, dhambi inakuvizia mlangoni mwako, ikikutamani wewe, lakini inakupasa uishinde.” Basi Kaini akamwambia ndugu yake Habili, “Twende shambani.” Walipokuwa shambani, Kaini akamshambulia Habili ndugu yake, akamuua. Kisha Mwenyezi Mungu akamuuliza Kaini, “Ndugu yako Habili yuko wapi?” Akamjibu, “Sijui. Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” Mwenyezi Mungu akasema, “Umefanya nini? Sikiliza! Damu ya ndugu yako inanililia mimi kutoka ardhini. Sasa umelaaniwa na umehamishwa kutoka ardhi, ambayo imefungua kinywa chake na kupokea damu ya ndugu yako kutoka mkononi mwako. Utakapoilima ardhi, haitakupa tena mazao yake. Utakuwa mtu wa kutangatanga duniani bila utulivu.” Kaini akamwambia Mwenyezi Mungu, “Adhabu yangu ni zaidi ya ninavyoweza kustahimili. Leo unanifukuza kutoka nchi, nami nitafichwa mbali na uwepo wako. Nitakuwa mtu wa kutangatanga duniani bila utulivu, na yeyote anionaye ataniua.” Lakini Mwenyezi Mungu akamwambia, “La, sivyo! Ikiwa mtu yeyote atamuua Kaini, atalipizwa kisasi mara saba.” Kisha Mwenyezi Mungu akamwekea Kaini alama ili yeyote angemwona asimuue. Kwa hiyo Kaini akaondoka mbele za Mwenyezi Mungu, akaenda kuishi katika nchi ya Nodi, mashariki mwa Edeni.