Mwanzo 35:16-29
Mwanzo 35:16-29 NEN
Kisha wakaondoka Betheli. Walipokuwa umbali fulani kabla ya kufika Efrathi, Raheli akaanza kusikia uchungu na alipata shida kuu. Alipokuwa katika shida hii katika kujifungua, mkunga akamwambia, “Usiogope, kwa sababu umempata mwana mwingine.” Hapo alipopumua pumzi yake ya mwisho, kwa maana alikuwa akifa, akamwita mwanawe Benoni. Lakini babaye akamwita Benyamini. Kwa hiyo Raheli akafa, akazikwa kando ya njia iendayo Efrathi (ndio Bethlehemu). Juu ya kaburi lake, Yakobo akasimamisha nguzo, ambayo mpaka leo inatambulisha kaburi la Raheli. Israeli akaendelea tena na safari yake na kupiga hema mbele mnara wa Ederi. Wakati Israeli alipokuwa akiishi katika nchi ile, Reubeni mwanawe alikutana kimwili na suria wa baba yake aitwaye Bilha, naye Israeli akasikia jambo hili. Yakobo alikuwa na wana kumi na wawili: Wana wa Lea walikuwa: Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Yakobo, Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari na Zabuloni. Wana wa Raheli walikuwa: Yosefu na Benyamini. Wana waliozaliwa na Bilha mtumishi wa kike wa Raheli walikuwa: Dani na Naftali. Wana waliozaliwa na Zilpa mtumishi wa kike wa Lea walikuwa: Gadi na Asheri. Hawa walikuwa wana wa Yakobo, waliozaliwa kwake akiwa Padan-Aramu. Yakobo akarudi nyumbani kwa baba yake Isaki huko Mamre, karibu na Kiriath-Arba (yaani Hebroni), ambapo walikuwa wameishi Abrahamu na Isaki. Isaki aliishi miaka 180. Kisha Isaki akapumua pumzi yake ya mwisho akafa, akakusanywa pamoja na watu wake akiwa mzee wa miaka mingi. Nao wanawe Esau na Yakobo wakamzika.