Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 35:16-29

Mwanzo 35:16-29 Biblia Habari Njema (BHN)

Yakobo na jamaa yake yote waliendelea na safari yao kutoka Betheli. Walipokuwa umbali fulani kabla ya kufika Efratha, Raheli akashikwa na uchungu mkali wa kuzaa. Naye alipokuwa katika uchungu huo, mkunga akamwambia, “Usiogope, umepata mtoto mwingine wa kiume.” Raheli huku akikata roho, akampa huyo mtoto jina Ben-oni. Lakini baba yake akamwita mtoto huyo Benyamini. Basi, Raheli akafariki na kuzikwa kando ya njia iendayo Efratha (yaani Bethlehemu). Yakobo akasimika nguzo ya kumbukumbu juu ya kaburi la Raheli ambayo ipo mpaka leo. Israeli akaendelea na safari yake na kupiga kambi yake baada ya kuupita mnara wa Ederi. Wakati Israeli alipokuwa anakaa nchini humo, mwanawe Reubeni, alilala na Bilha, suria wa baba yake; naye Israeli akasikia habari hizo. Yakobo alikuwa na watoto wa kiume kumi na wawili. Wana wa Lea walikuwa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Yakobo, Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari na Zebuluni. Watoto wa kiume wa Raheli walikuwa Yosefu na Benyamini. Watoto wa kiume waliozaliwa na Bilha, mjakazi wa Raheli, walikuwa Dani na Naftali. Na watoto wa kiume waliozaliwa na Zilpa, mjakazi wa Lea, walikuwa Gadi na Asheri. Hao ndio watoto wa kiume wa Yakobo, aliowazaa alipokuwa kule Padan-aramu. Yakobo aliondoka akaenda Mamre kwa baba yake Isaka, huko Kiriath-arba, yaani Hebroni, mahali ambapo Abrahamu na Isaka walikaa kama wageni. Isaka alikuwa na miaka 180 akafariki akiwa mzee wa miaka mingi. Watoto wake, Esau na Yakobo wakamzika.

Shirikisha
Soma Mwanzo 35

Mwanzo 35:16-29 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kisha wakaondoka Betheli. Walipokuwa umbali fulani kabla ya kufika Efrathi, Raheli akaanza kusikia uchungu na alipata shida kuu. Alipokuwa katika shida hii katika kujifungua, mkunga akamwambia, “Usiogope, kwa sababu umempata mwana mwingine.” Hapo alipopumua pumzi yake ya mwisho, kwa maana alikuwa akifa, akamwita mwanawe Benoni. Lakini babaye akamwita Benyamini. Kwa hiyo Raheli akafa, akazikwa kando ya njia iendayo Efrathi (ndio Bethlehemu). Juu ya kaburi lake, Yakobo akasimamisha nguzo, ambayo mpaka leo inatambulisha kaburi la Raheli. Israeli akaendelea tena na safari yake na kupiga hema mbele mnara wa Ederi. Wakati Israeli alipokuwa akiishi katika nchi ile, Reubeni mwanawe alikutana kimwili na suria wa baba yake aitwaye Bilha, naye Israeli akasikia jambo hili. Yakobo alikuwa na wana kumi na wawili: Wana wa Lea walikuwa: Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Yakobo, Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari na Zabuloni. Wana wa Raheli walikuwa: Yosefu na Benyamini. Wana waliozaliwa na Bilha mtumishi wa kike wa Raheli walikuwa: Dani na Naftali. Wana waliozaliwa na Zilpa mtumishi wa kike wa Lea walikuwa: Gadi na Asheri. Hawa walikuwa wana wa Yakobo, waliozaliwa kwake akiwa Padan-Aramu. Yakobo akarudi nyumbani kwa baba yake Isaki huko Mamre, karibu na Kiriath-Arba (yaani Hebroni), ambapo walikuwa wameishi Abrahamu na Isaki. Isaki aliishi miaka 180. Kisha Isaki akapumua pumzi yake ya mwisho akafa, akakusanywa pamoja na watu wake akiwa mzee wa miaka mingi. Nao wanawe Esau na Yakobo wakamzika.

Shirikisha
Soma Mwanzo 35