Mwanzo 34:1-19
Mwanzo 34:1-19 NENO
Basi Dina, binti Yakobo aliyezaliwa na Lea, akaenda kuwatembelea wanawake wa nchi ile. Ikawa Shekemu mwana wa Hamori Mhivi, mtawala wa eneo lile, alipomwona, akamchukua na kumnajisi. Moyo wake ukavutwa sana kwa Dina binti Yakobo, akampenda huyu msichana na akazungumza naye kwa kumbembeleza. Shekemu akamwambia Hamori, baba yake, “Nipatie msichana huyu awe mke wangu.” Yakobo aliposikia kwamba binti yake Dina amenajisiwa, wanawe walikuwa mashambani wakichunga mifugo yake. Kwa hiyo akalinyamazia jambo hilo hadi waliporudi nyumbani. Kisha Hamori baba yake Shekemu akaenda kuzungumza na Yakobo. Basi wana wa Yakobo wakarudi kutoka mashambani mara tu waliposikia kilichotukia. Walijawa na huzuni na ghadhabu, kwa sababu Shekemu alikuwa amefanya jambo la aibu katika Israeli kwa kukutana kimwili na binti Yakobo, jambo ambalo halikupasa kutendwa. Lakini Hamori akawaambia, “Moyo wa mwanangu Shekemu umeelekea kwa binti yenu. Tafadhali mpeni awe mke wake. Oaneni na sisi; tupeni binti zenu, nanyi mchukue binti zetu. Mwaweza kuishi nasi, nchi ni wazi kwenu. Ishini ndani yake, mfanye biashara humu na mjipatie mali.” Kisha Shekemu akamwambia baba yake Dina pamoja na ndugu zake, “Naomba nipate kibali machoni penu, nami nitawapa chochote mtakachosema. Niambieni kiasi cha mahari na zawadi nitakayoileta, hata iwe kubwa kiasi gani, nami nitawalipa chochote mtakachodai. Nipeni tu huyu msichana awe mke wangu.” Kwa sababu dada yao Dina alikuwa amenajisiwa, wana wa Yakobo wakajibu kwa udanganyifu walipozungumza na Shekemu pamoja na Hamori, baba yake. Wakawaambia, “Hatuwezi kufanya jambo kama hili. Hatuwezi kumtoa dada yetu kwa mtu ambaye hajatahiriwa. Hiyo itakuwa aibu kwetu. Tutakuruhusu kwa sharti moja tu, kwamba mtakuwa kama sisi kwa kuwatahiri wanaume wenu wote. Kisha tutawapa binti zetu na sisi tutawachukua binti zenu. Tutaishi kwenu na tutakuwa watu wamoja nanyi. Lakini mkikataa kutahiriwa, tutamchukua dada yetu na kuondoka.” Pendekezo lao likakubalika kwa Hamori na Shekemu mwanawe. Kijana huyo, aliyekuwa ameheshimiwa kati ya wote walioishi nyumbani mwa baba yake, hakupoteza muda kufanya waliyoyasema, kwa sababu alikuwa amependezwa sana na binti Yakobo.