Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 34:1-19

Mwanzo 34:1-19 SRUV

Basi Dina, binti Lea, ambaye Lea alimzalia Yakobo, akatoka kuwaona binti za nchi. Shekemu, mwana wa Hamori, Mhivi, mkuu wa nchi, akamwona akamtwaa, akalala naye, akambikiri. Moyo wake ukaambatana na Dina binti Yakobo, akampenda huyu msichana, akasema na huyu msichana kwa maneno mazuri. Shekemu akamwambia Hamori, babaye, akasema, Unipatie msichana huyu awe mke wangu. Basi Yakobo akasikia ya kwamba amembikiri Dina, binti yake. Na wanawe walikuwako pamoja na wanyama wake nyikani. Yakobo akanyamaza, hadi walipokuja. Akatoka Hamori, babaye Shekemu, kumwendea Yakobo, aseme naye. Wanawe Yakobo waliposikia hayo, wakaja kutoka malishoni; nao wakasikitika sana, wakakasirika mno, kwa sababu amefanya upumbavu katika Israeli kwa kulala na binti Yakobo, jambo lisilostahili kutendeka. Hamori akasema nao, akinena, roho ya Shekemu, mwanangu, inamtamani binti yenu, tafadhalini, mpeni amwoe. Mkaoane na sisi, mtupe sisi binti zenu, nanyi mkatwae binti zetu. Nanyi mtakaa nasi, na nchi hii itakuwa mbele yenu; kaeni, na kufanya biashara humo, mkapate mali humo. Shekemu akamwambia babaye yule msichana na nduguze, Na nikubalike machoni penu, na mtakavyoniambia nitatoa. Mjapoongeza sana mahari na zawadi, nitatoa kadiri ya mtakavyoniambia, lakini mnipe huyu msichana, awe mke wangu. Wana wa Yakobo wakawajibu Shekemu na Hamori babaye, kwa hila, maana amemharibu Dina, dada yao, wakawaambia, Hatuwezi kufanya neno hili, tumpe dada yetu mtu asiyetahiriwa; ingekuwa aibu kwetu. Lakini kwa sharti hii tu tutapatana nanyi; mkiwa kama sisi, akitahiriwa kila mwanamume wenu, ndipo tutawapa ninyi binti yetu, na sisi tutatwaa binti zenu tutakaa pamoja nanyi, nasi tutakuwa watu wamoja. Lakini kama hamtusikii na kutahiriwa, basi tutamtwaa binti yetu, nasi tutakwenda zetu. Maneno yao yakawa mema machoni pa Hamori, na machoni pa Shekemu, mwana wa Hamori. Na yule kijana hakukawia kulifanya neno lile, maana amependezewa na binti Yakobo, naye alikuwa mwenye heshima kuliko wote nyumbani mwa babaye.

Soma Mwanzo 34