Mwanzo 34:1-19
Mwanzo 34:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku moja, Dina, binti yake Yakobo na Lea, alikwenda kuwatembelea wanawake wa nchi hiyo. Basi, Shekemu, mwana wa Hamori, Mhivi, aliyekuwa mkuu wa nchi hiyo, alipomwona Dina, akamshika, akalala naye kwa nguvu. Lakini Shekemu akavutiwa sana na huyo msichana, akampenda hata akaanza kumbembeleza. Kwa hiyo, Shekemu akazungumza na Hamori baba yake, akamwambia, “Tafadhali, niombee huyo msichana nimwoe.” Yakobo akapata habari kwamba Dina, bintiye, alikuwa amenajisiwa na Shekemu; lakini kwa kuwa wanawe walikuwa malishoni, alinyamaza mpaka waliporudi. Hamori, baba yake Shekemu, akaenda kwa Yakobo ili azungumze naye, na wakati huohuo watoto wa kiume wa Yakobo wakawa wanarudi nyumbani kutoka malishoni. Waliposikia hayo, vijana hao wakaona uchungu mwingi na kukasirika sana, kwa vile Shekemu alikuwa amewafanyia watu wa Israeli ovu hilo la kulala na binti ya Yakobo, maana jambo hilo lilikuwa mwiko. Lakini Hamori akawaambia, “Mwanangu Shekemu anampenda sana binti yenu. Basi, tafadhali mumruhusu amwoe. Acheni tuoane: Nyinyi mtatuoza binti zenu, nasi tutawaoza binti zetu. Kwa hiyo mtaishi pamoja nasi; mtakuwa huru katika nchi hii. Mtaishi humu, mfanye biashara na kujipatia mali.” Hali kadhalika, Shekemu akawaambia baba na ndugu zake Dina, “Tafadhali, mniwie radhi, nami nitawapeni chochote mtakachosema. Niambieni kiasi chochote cha mahari na zawadi, hata kikiwa kikubwa namna gani, nami nitatoa, mradi tu mnioze msichana huyu.” Basi, watoto wa kiume wa Yakobo wakamjibu Shekemu na baba yake Hamori kwa hila, kwa kuwa Shekemu alikuwa amekwisha mnajisi dada yao Dina. Waliwaambia, “Hatuwezi kumwoza dada yetu kwa mtu asiyetahiriwa. Kufanya hivyo ni aibu kwetu. Tutakubaliana nanyi tu kwa sharti hili: Kwamba mtakuwa kama sisi kwa kumtahiri kila mwanamume miongoni mwenu. Hapo ndipo tutakapowaoza binti zetu na kuwaoa binti zenu; tutaishi pamoja nanyi na kuwa jamaa moja. Lakini msipokubaliana nasi na kutahiriwa, basi, sisi tutamchukua binti yetu na kwenda zetu.” Pendekezo lao likawapendeza Hamori na mwanawe Shekemu. Kijana huyo hakusita hata kidogo kutekeleza sharti hilo, kwa vile alivyompenda binti wa Yakobo. Isitoshe, Shekemu ndiye aliyeheshimika kuliko wote nyumbani kwao.
Mwanzo 34:1-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Dina, binti Lea, ambaye Lea alimzalia Yakobo, akatoka kuwaona binti za nchi. Shekemu, mwana wa Hamori, Mhivi, mkuu wa nchi, akamwona akamtwaa, akalala naye, akambikiri. Moyo wake ukaambatana na Dina binti Yakobo, akampenda huyu msichana, akasema na huyu msichana kwa maneno mazuri. Shekemu akamwambia Hamori, babaye, akasema, Unipatie msichana huyu awe mke wangu. Basi Yakobo akasikia ya kwamba amembikiri Dina, binti yake. Na wanawe walikuwako pamoja na wanyama wake nyikani. Yakobo akanyamaza, hadi walipokuja. Akatoka Hamori, babaye Shekemu, kumwendea Yakobo, aseme naye. Wanawe Yakobo waliposikia hayo, wakaja kutoka malishoni; nao wakasikitika sana, wakakasirika mno, kwa sababu amefanya upumbavu katika Israeli kwa kulala na binti Yakobo, jambo lisilostahili kutendeka. Hamori akasema nao, akinena, roho ya Shekemu, mwanangu, inamtamani binti yenu, tafadhalini, mpeni amwoe. Mkaoane na sisi, mtupe sisi binti zenu, nanyi mkatwae binti zetu. Nanyi mtakaa nasi, na nchi hii itakuwa mbele yenu; kaeni, na kufanya biashara humo, mkapate mali humo. Shekemu akamwambia babaye yule msichana na nduguze, Na nikubalike machoni penu, na mtakavyoniambia nitatoa. Mjapoongeza sana mahari na zawadi, nitatoa kadiri ya mtakavyoniambia, lakini mnipe huyu msichana, awe mke wangu. Wana wa Yakobo wakawajibu Shekemu na Hamori babaye, kwa hila, maana amemharibu Dina, dada yao, wakawaambia, Hatuwezi kufanya neno hili, tumpe dada yetu mtu asiyetahiriwa; ingekuwa aibu kwetu. Lakini kwa sharti hii tu tutapatana nanyi; mkiwa kama sisi, akitahiriwa kila mwanamume wenu, ndipo tutawapa ninyi binti yetu, na sisi tutatwaa binti zenu tutakaa pamoja nanyi, nasi tutakuwa watu wamoja. Lakini kama hamtusikii na kutahiriwa, basi tutamtwaa binti yetu, nasi tutakwenda zetu. Maneno yao yakawa mema machoni pa Hamori, na machoni pa Shekemu, mwana wa Hamori. Na yule kijana hakukawia kulifanya neno lile, maana amependezewa na binti Yakobo, naye alikuwa mwenye heshima kuliko wote nyumbani mwa babaye.
Mwanzo 34:1-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Dina, binti Lea, ambaye Lea alimzalia Yakobo, akatoka kuwaona binti za nchi. Shekemu, mwana wa Hamori, Mhivi, mkuu wa nchi, akamwona akamtwaa, akalala naye, akambikiri. Moyo wake ukaambatana na Dina binti Yakobo, akampenda huyu msichana, akasema na huyu msichana kwa maneno mazuri. Shekemu akamwambia Hamori, babaye, akasema, Unipatie msichana huyu awe mke wangu. Basi Yakobo akasikia ya kwamba amembikiri Dina, binti yake. Na wanawe walikuwako pamoja na wanyama wake nyikani. Yakobo akanyamaza, hata walipokuja. Akatoka Hamori, babaye Shekemu, kumwendea Yakobo, aseme naye. Wanawe Yakobo waliposikia hayo, wakaja kutoka nyikani; nao wakasikitika sana, wakakasirika mno, kwa sababu amefanya upumbavu katika Israeli kwa kulala na binti Yakobo, neno lisilojuzu kutendeka. Hamori akasema nao, akinena, Roho ya Shekemu, mwanangu, inamtamani binti yenu, tafadhalini, mpeni amwoe. Mkaoane na sisi, mtupe sisi binti zenu, nanyi mkatwae binti zetu. Nanyi mtakaa nasi, na nchi hii itakuwa mbele yenu; kaeni, na kufanya biashara humo, mkapate mali humo. Shekemu akamwambia babaye yule msichana na nduguze, Na nikubalike machoni penu, na mtakavyoniambia nitatoa. Mjapoongeza sana mahari na zawadi, nitatoa kadiri ya mtakavyoniambia, lakini mnipe huyu msichana, awe mke wangu. Wana wa Yakobo wakawajibu Shekemu na Hamori babaye, kwa hila, maana amemharibu Dina, umbu lao, wakawaambia, Hatuwezi kufanya neno hili, tumpe umbu letu mtu asiyetahiriwa; ingekuwa aibu kwetu. Lakini kwa sharti hii tu tutapatana nanyi; mkiwa kama sisi, akitahiriwa kila mwanamume wenu, ndipo tutawapa ninyi binti yetu, na sisi tutatwaa binti zenu tutakaa pamoja nanyi, nasi tutakuwa watu wamoja. Lakini kama hamtusikii na kutahiriwa, basi tutamtwaa umbu letu, nasi tutakwenda zetu. Maneno yao yakawa mema machoni pa Hamori, na machoni pa Shekemu, mwana wa Hamori. Na yule kijana hakukawia kulifanya neno lile, maana amependezewa na binti Yakobo, naye alikuwa mwenye heshima kuliko wote nyumbani mwa babaye.
Mwanzo 34:1-19 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi Dina, binti Yakobo aliyezaliwa na Lea, akaenda kuwatembelea wanawake wa nchi ile. Ikawa Shekemu mwana wa Hamori Mhivi, mtawala wa eneo lile, alipomwona, akamchukua na kumnajisi. Moyo wake ukavutwa sana kwa Dina binti Yakobo, akampenda huyu msichana na akazungumza naye kwa kumbembeleza. Shekemu akamwambia Hamori, baba yake, “Nipatie msichana huyu awe mke wangu.” Yakobo aliposikia kwamba binti yake Dina amenajisiwa, wanawe walikuwa mashambani wakichunga mifugo yake. Kwa hiyo akalinyamazia jambo hilo hadi waliporudi nyumbani. Kisha Hamori baba yake Shekemu akaenda kuzungumza na Yakobo. Basi wana wa Yakobo wakarudi kutoka mashambani mara tu waliposikia kilichotukia. Walijawa na huzuni na ghadhabu, kwa sababu Shekemu alikuwa amefanya jambo la aibu katika Israeli kwa kukutana kimwili na binti Yakobo, jambo ambalo halikupasa kutendwa. Lakini Hamori akawaambia, “Moyo wa mwanangu Shekemu umeelekea kwa binti yenu. Tafadhali mpeni awe mke wake. Oaneni na sisi; tupeni binti zenu, nanyi mchukue binti zetu. Mwaweza kuishi nasi, nchi ni wazi kwenu. Ishini ndani yake, mfanye biashara humu na mjipatie mali.” Kisha Shekemu akamwambia baba yake Dina pamoja na ndugu zake, “Naomba nipate kibali machoni penu, nami nitawapa chochote mtakachosema. Niambieni kiasi cha mahari na zawadi nitakayoileta, hata iwe kubwa kiasi gani, nami nitawalipa chochote mtakachodai. Nipeni tu huyu msichana awe mke wangu.” Kwa sababu dada yao Dina alikuwa amenajisiwa, wana wa Yakobo wakajibu kwa udanganyifu walipozungumza na Shekemu pamoja na Hamori, baba yake. Wakawaambia, “Hatuwezi kufanya jambo kama hili. Hatuwezi kumtoa dada yetu kwa mtu ambaye hajatahiriwa. Hiyo itakuwa aibu kwetu. Tutakuruhusu kwa sharti moja tu, kwamba mtakuwa kama sisi kwa kuwatahiri wanaume wenu wote. Kisha tutawapa binti zetu na sisi tutawachukua binti zenu. Tutaishi kwenu na tutakuwa watu wamoja nanyi. Lakini mkikataa kutahiriwa, tutamchukua dada yetu na kuondoka.” Pendekezo lao likakubalika kwa Hamori na Shekemu mwanawe. Kijana huyo, aliyekuwa ameheshimiwa kati ya wote walioishi nyumbani mwa baba yake, hakupoteza muda kufanya waliyoyasema, kwa sababu alikuwa amependezwa sana na binti Yakobo.