Mwanzo 26:12-23
Mwanzo 26:12-23 NENO
Isaka akapanda mazao katika nchi hiyo, na kwa mwaka huo huo akavuna mara mia, kwa sababu Mwenyezi Mungu alimbariki. Isaka akawa tajiri, nayo mali yake ikaendelea kuongezeka hata akawa tajiri sana. Akawa na mifugo ya kondoo na ng’ombe, na watumishi wengi sana, kiasi kwamba Wafilisti wakamwonea wivu. Kwa hiyo visima vyote vilivyochimbwa na watumishi wakati wa Ibrahimu baba yake, Wafilisti wakavifukia, wakavijaza udongo. Ndipo Abimeleki akamwambia Isaka, “Ondoka kwetu, kwa maana umetuzidi nguvu sana.” Basi Isaka akatoka huko, akajenga kambi katika Bonde la Gerari, akaishi huko. Ndipo Isaka akavichimbua tena vile visima vya maji ambavyo vilichimbwa siku zile za Ibrahimu baba yake, ambavyo Wafilisti walivifukia baada ya Ibrahimu kufa, akavipa majina yale yale ambayo baba yake alikuwa amevipa. Watumishi wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakagundua huko kisima chenye maji safi. Lakini wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, “Maji haya ni yetu!” Ndipo akakiita kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. Kisha wakachimba kisima kingine, lakini hata hicho pia wakakigombania; akakiita Sitna. Akaondoka huko, akachimba kisima kingine, wala hakuna yeyote aliyekigombania. Akakiita Rehobothi, akisema, “Sasa Mwenyezi Mungu ametufanyia nafasi, nasi tutastawi katika nchi.” Kutoka pale akaenda Beer-Sheba.