Mwanzo 26:12-23
Mwanzo 26:12-23 SRUV
Mwaka huo Isaka akapanda mbegu katika nchi ile, naye akapata mavuno mara mia zaidi. BWANA akambariki. Na mtu huyu akawa mkuu, akazidi kusitawi, hata akawa mkuu sana. Akawa na mali ya kondoo, na mali ya ng'ombe, na watumwa wengi. Hao Wafilisti wakamhusudu. Na vile visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake, siku za Abrahamu babaye, Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza udongo. Abimeleki akamwambia Isaka, Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi. Basi Isaka akatoka huko akapiga kambi katika bonde la Gerari, akakaa huko. Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Abrahamu babaye; maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Abrahamu; naye akaviita majina kufuata majina aliyoviita babaye. Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika. Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna. Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi. Akapanda kutoka hapo mpaka Beer-sheba.