Mwanzo 26:12-23
Mwanzo 26:12-23 NEN
Isaki akapanda mazao katika nchi hiyo, kwa mwaka huo huo, akavuna mara mia, kwa sababu BWANA alimbariki. Isaki akawa tajiri, mali zake zikaendelea kuongezeka mpaka akawa tajiri sana. Akawa na mifugo ya kondoo na ngʼombe, na watumishi wengi sana, kiasi kwamba Wafilisti wakamwonea wivu. Kwa hiyo visima vyote vilivyochimbwa na watumishi wakati wa Abrahamu baba yake, Wafilisti wakavifukia, wakavijaza udongo. Ndipo Abimeleki akamwambia Isaki, “Ondoka kwetu, kwa maana umetuzidi nguvu sana.” Basi Isaki akatoka huko akajenga kambi katika Bonde la Gerari, akaishi huko. Ndipo Isaki akavichimbua tena vile visima vya maji ambavyo vilichimbwa siku zile za Abrahamu baba yake, ambavyo Wafilisti walivifukia baada ya kufa Abrahamu, akavipa majina yale yale ambayo baba yake alikuwa amevipa. Watumishi wa Isaki wakachimba katika lile bonde wakagundua huko kisima chenye maji safi. Lakini wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaki wakisema, “Maji haya ni yetu!” Ndipo akakiita kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. Kisha wakachimba kisima kingine, lakini hata hicho pia wakakigombania, akakiita Sitna. Akaondoka huko, akachimba kisima kingine, wala hakuna yeyote aliyekigombania. Akakiita Rehobothi, akisema, “Sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutastawi katika nchi.” Kutoka pale akaenda Beer-Sheba.