Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 25:19-34

Mwanzo 25:19-34 NEN

Hivi ndivyo vizazi vya Isaki mwana wa Abrahamu. Abrahamu akamzaa Isaki, Isaki alikuwa na umri wa miaka arobaini alipomwoa Rebeka binti Bethueli Mwaramu kutoka Padan-Aramu, nduguye Labani Mwaramu. Isaki akamwomba BWANA kwa ajili ya mke wake, kwa sababu alikuwa tasa. BWANA akajibu maombi yake na Rebeka mkewe akapata mimba. Watoto wakashindana tumboni mwake, akasema, “Kwa nini haya yanatokea kwangu?” Kwa hiyo akaenda kumuuliza BWANA. BWANA akamjibu, “Mataifa mawili yamo tumboni mwako, na mataifa hayo mawili kutoka ndani yako watatenganishwa. Mmoja atakuwa na nguvu zaidi kuliko mwingine, na yule mkubwa atamtumikia yule mdogo.” Wakati wake wa kujifungua ulipotimia, walikuwepo mapacha wa kiume tumboni mwake. Wa kwanza kuzaliwa alikuwa mwekundu, mwili wake wote ulikuwa kama mtu aliyevaa vazi lenye nywele; wakamwita jina lake Esau. Baadaye, ndugu yake akatoka, mkono wake ukiwa umemshika Esau kisigino; akaitwa jina lake Yakobo. Isaki alikuwa mwenye miaka sitini Rebeka alipowazaa. Watoto wakakua, naye Esau akakuwa mwindaji hodari, mtu wa mbugani, wakati Yakobo alikuwa mtu mtulivu, mwenye kukaa nyumbani. Isaki, ambaye alikuwa anapendelea zaidi nyama za porini, alimpenda Esau, bali Rebeka alimpenda Yakobo. Siku moja Yakobo alipika mchuzi wa dengu, Esau akarudi kutoka porini akiwa na njaa kali. Esau akamwambia Yakobo, “Haraka, nipe huo mchuzi mwekundu! Nina njaa kali sana!” (Hii ndiyo sababu pia aliitwa Edomu.) Yakobo akamjibu, “Niuzie kwanza haki yako ya mzaliwa wa kwanza.” Esau akasema, “Tazama, mimi niko karibu ya kufa, itanifaa nini haki ya mzaliwa wa kwanza?” Yakobo akamwambia, “Niapie kwanza.” Hivyo Esau akamwapia, akamuuzia Yakobo haki yake ya kuzaliwa. Ndipo Yakobo akampa Esau mkate na ule mchuzi wa dengu. Akala na kunywa, kisha akainuka akaenda zake. Kwa hiyo Esau alidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mwanzo 25:19-34

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha