Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 25:19-34

Mwanzo 25:19-34 Biblia Habari Njema (BHN)

Hawa ndio wazawa wa Isaka mwana wa Abrahamu. Isaka alipokuwa na umri wa miaka arubaini alimwoa Rebeka, binti Bethueli, Mwaramu wa Padan-aramu. Rebeka alikuwa dada yake Labani. Rebeka alikuwa tasa, kwa hiyo Isaka akamwomba Mwenyezi-Mungu. Naye Mwenyezi-Mungu akakubali ombi lake, Rebeka akapata mimba. Mimba hiyo ilikuwa ya mapacha. Watoto hao wakashindana tumboni mwake Rebeka, naye akasema, “Kama hivi ndivyo mambo yalivyo, ya nini kuishi?” Basi, akaenda kumwuliza Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Mataifa mawili yamo tumboni mwako; makabila mawili yatakayozaliwa nawe, yatafarakana. Moja litakuwa lenye nguvu kuliko lingine; mkubwa atamtumikia mdogo.” Siku zake za kujifungua zilipotimia, Rebeka alijifungua mapacha. Wa kwanza alikuwa mwekundu, mwenye nywele mwili wote; hivyo wakamwita Esau. Wa pili alizaliwa akiwa amemshika Esau kisigino, hivyo wakampa jina Yakobo. Isaka alikuwa na umri wa miaka sitini wakati Esau na Yakobo walipozaliwa. Watoto hao wakakua; Esau akawa mwindaji hodari, mpenda maisha ya mbugani, na Yakobo akawa mtu mtulivu, mpenda maisha ya nyumbani. Basi, Isaka akampenda Esau kwa sababu alipenda kula mawindo yake, lakini Rebeka akampenda Yakobo. Siku moja, Yakobo alipokuwa anapika dengu, Esau alirudi nyumbani kutoka mawindoni ana njaa sana. Kwa hiyo akamwambia Yakobo, “Nafa njaa; tafadhali, nigawie chakula hicho chekundu nile.” (Ndiyo maana walimpanga jina Edomu yaani mwekundu). Yakobo akajibu, “Kwanza niuzie haki yako ya mzaliwa wa kwanza.” Esau akasema, “Sawa! Niko karibu kufa; haki yangu ya mzaliwa wa kwanza itanifaa nini?” Yakobo akamwambia, “Niapie kwanza.” Basi, Esau akamwapia na kumwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza. Ndipo Yakobo akampa Esau mkate na dengu kiasi. Esau akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo ndivyo Esau alivyoidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.

Shirikisha
Soma Mwanzo 25

Mwanzo 25:19-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Na hivi ndivyo vizazi vya Isaka, mwana wa Abrahamu. Abrahamu alimzaa Isaka. Isaka akawa mwenye miaka arubaini alipomtwaa Rebeka binti Bethueli, Mshami, wa Padan-aramu, ndugu wa Labani, Mshami, kuwa mke wake. Isaka akamwomba BWANA kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye BWANA akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba. Watoto wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda kumwuliza BWANA. BWANA akamwambia, Mataifa mawili yako tumboni mwako, Na makabila mawili ya watu watafarakana tangu tumboni mwako. Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili, Na mkubwa atamtumikia mdogo. Siku zake za kuzaa zilipotimia, tazama! Mapacha walikuwamo tumboni mwake. Wa kwanza akatoka, naye alikuwa mwekundu mwili wote kama vazi la nywele. Wakamwita jina lake Esau. Baadaye ndugu yake akatoka, na mkono wake ukiwa umemshika Esau kisigino. Akaitwa jina lake Yakobo. Isaka alikuwa mwenye miaka sitini mkewe alipowazaa. Watoto wakakua, Esau alikuwa mtu ajuaye kuwinda wanyama, mtu wa nyikani, na Yakobo alikuwa mtu mtulivu, mwenye kukaa hemani. Basi Isaka akampenda Esau, kwa sababu alikula mawindo yake, na Rebeka akampenda Yakobo. Yakobo akapika chakula cha dengu. Esau akaja kutoka mbugani, naye alikuwa amechoka sana. Esau akamwambia Yakobo, Tafadhali, unipe hicho chakula chekundu nile, kwa kuwa ninazimia mimi. Kwa hiyo walimwita jina lake Edomu. Yakobo akamwambia, Kwanza niuzie leo haki yako ya mzaliwa wa kwanza. Esau akasema, Tazama, mimi ni karibu kufa, itanifaa nini haki hii ya uzazi? Yakobo akamwambia, Niapie kwanza. Naye akamwapia, akamwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza. Yakobo akampa Esau mkate na chakula cha dengu, naye akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo Esau akaidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.

Shirikisha
Soma Mwanzo 25

Mwanzo 25:19-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Na hivi ndivyo vizazi vya Isaka, mwana wa Ibrahimu. Ibrahimu alimzaa Isaka. Isaka akawa mwenye miaka arobaini alipomtwaa Rebeka binti Bethueli, Mshami, wa Padan-aramu, ndugu wa Labani, Mshami, kuwa mke wake. Isaka akamwomba BWANA kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye BWANA akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba. Watoto wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda kumwuliza BWANA. BWANA akamwambia, Mataifa mawili yako tumboni mwako, Na kabila mbili za watu watafarakana tangu tumboni mwako. Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili, Na mkubwa atamtumikia mdogo. Siku zake za kuzaa zilipotimia, tazama! Mapacha walikuwamo tumboni mwake. Wa kwanza akatoka, naye alikuwa mwekundu mwili wote kama vazi la nywele. Wakamwita jina lake Esau. Baadaye ndugu yake akatoka, na mkono wake unamshika Esau kisigino. Akaitwa jina lake Yakobo. Isaka alikuwa mwenye miaka sitini mkewe alipowazaa. Watoto wakakua, Esau alikuwa mtu ajuaye kuwinda wanyama, mtu wa nyikani, na Yakobo alikuwa mtu mtulivu, mwenye kukaa hemani. Basi Isaka akampenda Esau, kwa sababu alikula mawindo yake, na Rebeka akampenda Yakobo. Yakobo akapika chakula cha dengu. Esau akaja kutoka nyikani, naye alikuwa amechoka sana. Esau akamwambia Yakobo, Tafadhali, unipe hicho chakula chekundu nile, kwa kuwa ninazimia mimi. Kwa hiyo walimwita jina lake Edomu. Yakobo akamwambia, Kwanza niuzie leo haki yako ya mzaliwa wa kwanza. Esau akasema, Tazama, mimi ni karibu kufa, itanifaa nini haki hii ya uzazi? Yakobo akamwambia, Uniapie kwanza. Naye akamwapia, akamwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza. Yakobo akampa Esau mkate na chakula cha dengu, naye akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo Esau akaidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.

Shirikisha
Soma Mwanzo 25

Mwanzo 25:19-34 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Hivi ndivyo vizazi vya Isaki mwana wa Abrahamu. Abrahamu akamzaa Isaki, Isaki alikuwa na umri wa miaka arobaini alipomwoa Rebeka binti Bethueli Mwaramu kutoka Padan-Aramu, nduguye Labani Mwaramu. Isaki akamwomba BWANA kwa ajili ya mke wake, kwa sababu alikuwa tasa. BWANA akajibu maombi yake na Rebeka mkewe akapata mimba. Watoto wakashindana tumboni mwake, akasema, “Kwa nini haya yanatokea kwangu?” Kwa hiyo akaenda kumuuliza BWANA. BWANA akamjibu, “Mataifa mawili yamo tumboni mwako, na mataifa hayo mawili kutoka ndani yako watatenganishwa. Mmoja atakuwa na nguvu zaidi kuliko mwingine, na yule mkubwa atamtumikia yule mdogo.” Wakati wake wa kujifungua ulipotimia, walikuwepo mapacha wa kiume tumboni mwake. Wa kwanza kuzaliwa alikuwa mwekundu, mwili wake wote ulikuwa kama mtu aliyevaa vazi lenye nywele; wakamwita jina lake Esau. Baadaye, ndugu yake akatoka, mkono wake ukiwa umemshika Esau kisigino; akaitwa jina lake Yakobo. Isaki alikuwa mwenye miaka sitini Rebeka alipowazaa. Watoto wakakua, naye Esau akakuwa mwindaji hodari, mtu wa mbugani, wakati Yakobo alikuwa mtu mtulivu, mwenye kukaa nyumbani. Isaki, ambaye alikuwa anapendelea zaidi nyama za porini, alimpenda Esau, bali Rebeka alimpenda Yakobo. Siku moja Yakobo alipika mchuzi wa dengu, Esau akarudi kutoka porini akiwa na njaa kali. Esau akamwambia Yakobo, “Haraka, nipe huo mchuzi mwekundu! Nina njaa kali sana!” (Hii ndiyo sababu pia aliitwa Edomu.) Yakobo akamjibu, “Niuzie kwanza haki yako ya mzaliwa wa kwanza.” Esau akasema, “Tazama, mimi niko karibu ya kufa, itanifaa nini haki ya mzaliwa wa kwanza?” Yakobo akamwambia, “Niapie kwanza.” Hivyo Esau akamwapia, akamuuzia Yakobo haki yake ya kuzaliwa. Ndipo Yakobo akampa Esau mkate na ule mchuzi wa dengu. Akala na kunywa, kisha akainuka akaenda zake. Kwa hiyo Esau alidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.

Shirikisha
Soma Mwanzo 25