Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwa 25

25
Wazawa wa Ketura
1Ibrahimu alioa mke mwingine jina lake akiitwa Ketura. 2#1 Nya 1:32Akamzalia Zimrani, na Yokshani, na Medani, na Midiani, na Ishbaki, na Sua.
3Yokshani akamzaa Sheba, na Dedani; na wana wa Dedani walikuwa Waashuri na Waletushi, na Waleumi.
4Na wana wa Midiani walikuwa, Efa, na Eferi, na Hanoki, na Abida, na Eldaa.
Hao wote walikuwa ni wana wa Ketura.
5 # Mwa 24:36 Ibrahimu akampa Isaka yote aliyokuwa nayo. 6#Mwa 21:14; Amu 6:3Lakini wana wa masuria aliokuwa nao Ibrahimu, Ibrahimu akawapa zawadi, naye akawaondoa katika mahali alipokaa Isaka mwanawe, wakati wa uhai wake, waende pande za mashariki, mpaka nchi ya Kedemu.
Kifo cha Abrahamu
7Hizi ndizo siku za miaka ya maisha ya Ibrahimu alizoishi, miaka mia, na sabini na mitano. 8#Mwa 15:15; 47:8,9; 35:29; 49:33; Mdo 13:36Ibrahimu akafariki, naye akafa katika uzee mwema, mzee sana, ameshiba siku, akakusanyika kwa watu wake. 9#Mwa 49:29,30; 50:13Isaka na Ishmaeli wanawe wakamzika katika pango ya Makpela, katika shamba la Efroni bin Sohari Mhiti, lielekealo Mamre. 10#Mwa 23:3-16Katika lile shamba alilolinunua Ibrahimu kwa wazawa Hethi, huko ndiko alikozikwa Ibrahimu na Sara mkewe.
11 # Mwa 16:14; 24:62 Ikawa, baada ya kufa kwake Ibrahimu, Mungu akambariki Isaka mwanawe. Naye Isaka akakaa karibu ya Beer-lahai-roi.
Uzao wa Ishmaeli
12 # 1 Nya 1:29 Hivi ndivyo vizazi vya Ishmaeli, mwana wa Ibrahimu, ambaye Hajiri, Mmisri, mjakazi wa Sara, alimzalia Ibrahimu. 13Na haya ndiyo majina ya wana wa Ishmaeli, kwa majina yao, na kwa vizazi vyao.
Mzaliwa wa kwanza wa Ishmaeli, ni Nebayothi, na Kedari, na Abdeeli, na Mibsamu, 14na Mishma, na Duma, na Masa, 15na Hadadi, na Tema, na Yeturi, na Nafishi, na Kedema. 16#Mwa 17:20Hao ndio wana wa Ishmaeli, na hayo ni majina yao, katika miji yao, na katika vituo vyao, maseyidi kumi na wawili kwa kufuata jamaa zao.
17 # Mwa 25:8; 49:33; Mk 15:37 Na hii ndiyo miaka ya maisha ya Ishmaeli, miaka mia na thelathini na saba. Akakata roho, akafa, akakusanyika kwa watu wake.
18 # 1 Sam 15:7; Mwa 16:12 Wakakaa toka Havila mpaka Shuri, unaoelekea Misri, kwa njia ya kwenda Ashuru. Akakaa katikati ya ndugu zake wote.
Kuzaliwa na Kukua kwa Esau na Yakobo
19 # Mt 1:2 Na hivi ndivyo vizazi vya Isaka, mwana wa Ibrahimu. Ibrahimu alimzaa Isaka. 20#Mwa 22:23; 24:29,67Isaka akawa mwenye miaka arobaini alipomtwaa Rebeka binti Bethueli, Mshami, wa Padan-aramu, ndugu wa Labani, Mshami, kuwa mke wake.
21 # 1 Sam 1:11; 1 Nya 5:20; 2 Nya 33:13; Ezr 8:23; Rum 9:10 Isaka akamwomba BWANA kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye BWANA akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba. 22#1 Sam 9:9; 10:22Watoto wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda kumwuliza BWANA. 23#Rum 9:12; Mwa 24:60BWANA akamwambia,
Mataifa mawili yako tumboni mwako,
Na kabila mbili za watu watafarakana tangu tumboni mwako.
Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili,
Na mkubwa atamtumikia mdogo.
24Siku zake za kuzaa zilipotimia, tazama! Mapacha walikuwamo tumboni mwake. 25#Mwa 27:11Wa kwanza akatoka, naye alikuwa mwekundu mwili wote kama vazi la nywele. Wakamwita jina lake Esau. 26#Hos 12:3; Mwa 27:36Baadaye ndugu yake akatoka, na mkono wake unamshika Esau kisigino. Akaitwa jina lake Yakobo. Isaka alikuwa mwenye miaka sitini mkewe alipowazaa. 27#Mwa 27:3,5; Ayu 1:1,8; 2:3; Ebr 11:9Watoto wakakua, Esau alikuwa mtu ajuaye kuwinda wanyama, mtu wa nyikani, na Yakobo alikuwa mtu mtulivu, mwenye kukaa hemani. 28#Mwa 27:6,19Basi Isaka akampenda Esau, kwa sababu alikula mawindo yake, na Rebeka akampenda Yakobo.
Esau Auza Haki ya Uzaliwa Wake
29Yakobo akapika chakula cha dengu. Esau akaja kutoka nyikani, naye alikuwa amechoka sana. 30Esau akamwambia Yakobo, Tafadhali, unipe hicho chakula chekundu nile, kwa kuwa ninazimia mimi. Kwa hiyo walimwita jina lake Edomu.#25:30Edomu maana yake ni Mwekundu. 31Yakobo akamwambia, Kwanza niuzie leo haki yako ya mzaliwa wa kwanza. 32Esau akasema, Tazama, mimi ni karibu kufa, itanifaa nini haki hii ya uzazi? 33#Ebr 12:16Yakobo akamwambia, Uniapie kwanza. Naye akamwapia, akamwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza. 34#1 Kor 15:32Yakobo akampa Esau mkate na chakula cha dengu, naye akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo Esau akaidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.

Iliyochaguliwa sasa

Mwa 25: SUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha