Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 18:20-33

Mwanzo 18:20-33 NEN

Basi BWANA akasema, “Kilio dhidi ya Sodoma na Gomora ni kikubwa sana na dhambi yao inasikitisha sana, kwamba nitashuka nione kama waliyoyatenda ni mabaya kiasi cha kilio kilichonifikia. Kama sivyo, nitajua.” Basi wale watu wakageuka wakaenda kuelekea Sodoma, lakini Abrahamu akabaki amesimama mbele za BWANA. Ndipo Abrahamu akamsogelea akasema: “Je, utawaangamiza wenye haki na waovu? Je, ikiwa watakuwepo watu wenye haki hamsini katika mji huo, hivi kweli utauangamiza na wala hutauacha kwa ajili ya hao watu hamsini wenye haki waliomo ndani yake? Hilo na liwe mbali nawe, kufanya jambo kama hilo, kuwaua wenye haki pamoja na waovu, kuwatendea wenye haki sawasawa na waovu. Iwe mbali nawe! Je, Mwamuzi wa dunia yote hatafanya lililo sawa?” BWANA akasema, “Kama nikipata watu hamsini wenye haki katika mji wa Sodoma, nitausamehe huo mji wote kwa ajili yao.” Kisha Abrahamu akasema tena: “Sasa kwa kuwa nimekuwa na ujasiri wa kuzungumza na Bwana, ingawa mimi si kitu bali ni mavumbi na majivu; je, kama hesabu ya wenye haki imepungua watano katika hamsini, utauangamiza huo mji wote kwa ajili ya hao watano waliopungua?” Bwana akamwambia, “Kama nikiwakuta huko watu arobaini na watano, sitauangamiza.” Abrahamu akazungumza naye kwa mara nyingine, “Je, kama huko watapatikana watu arobaini tu?” Akamjibu, “Kwa ajili ya hao arobaini, sitauangamiza.” Ndipo akasema, “Bwana na asikasirike, lakini niruhusu nizungumze. Je, kama huko watakuwepo thelathini tu?” Akajibu, “Sitapaangamiza ikiwa nitawakuta huko watu thelathini.” Abrahamu akasema, “Sasa kwa kuwa nimekuwa na ujasiri sana kuzungumza na Bwana, je, kama wakipatikana huko watu ishirini tu?” Bwana akajibu, “Kwa ajili ya hao ishirini, sitauangamiza.” Abrahamu akasema, “Bwana na asikasirike, lakini niruhusu nizungumze tena mara moja tu. Itakuwaje kama watapatikana huko watu kumi tu?” Bwana akajibu, “Kwa ajili ya hao kumi, sitauangamiza.” BWANA alipomaliza kuzungumza na Abrahamu, akaondoka, naye Abrahamu akarudi nyumbani kwake.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mwanzo 18:20-33

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha