Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 18:20-33

Mwanzo 18:20-33 Biblia Habari Njema (BHN)

Basi, Mwenyezi-Mungu akasema, “Kuna malalamiko mengi dhidi ya watu wa Sodoma na Gomora, na dhambi yao ni kubwa mno. Hivyo nitashuka kwenda huko nijionee mwenyewe kama kweli wamefanya kadiri ya kilio kilichonifikia. Nataka kujua.” Kutoka hapo, wale watu wakashika njia kuelekea Sodoma, lakini Mwenyezi-Mungu akawa amebaki, amesimama pamoja na Abrahamu. Basi, Abrahamu akamkaribia Mwenyezi-Mungu, akamwuliza, “Je, kweli utawaangamiza watu wema pamoja na waovu? Huenda ikawa mna watu wema hamsini humo mjini. Je, utauangamiza mji mzima badala ya kuuacha kwa sababu ya hao wema hamsini waliomo humo? Sidhani kama utafanya hivyo! Kuwaua watu wema pamoja na waovu; wema kutendewa sawa na waovu! La, hasha! Hakimu wa dunia yote hataacha kutenda yaliyo sawa!” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nikikuta watu wema hamsini kule mjini Sodoma, basi nitauacha mji wote salama kwa ajili yao.” Abrahamu akasema, “Nimethubutu kuzungumza na Bwana, mimi niliye mavumbi na majivu tu. Huenda wakapatikana watu wema arubaini na watano badala ya hamsini. Je, utauangamiza mji mzima kwa sababu wamepungua watu watano?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Sitauangamiza mji ikiwa kuna watu wema arubaini na watano.” Abrahamu akaongeza kusema, “Pengine watu arubaini watapatikana humo.” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Kwa ajili ya watu wema arubaini, sitafanya hivyo.” Abrahamu akaongeza kusema, “Ee Bwana, naomba usinikasirikie, nami nitasema tena. Huenda wakapatikana watu wema thelathini.” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Sitafanya hivyo nikiwakuta hao thelathini.” Abrahamu akasema, “Nimethubutu kuzungumza na Bwana. Labda watapatikana watu wema ishirini.” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Kwa ajili ya hao ishirini, sitauangamiza.” Hatimaye, Abrahamu akasema, “Ee Bwana, nakuomba usikasirike, ila nitasema tena mara moja tu. Je, wakipatikana watu wema kumi, itakuwaje?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Kwa ajili ya hao watu wema kumi, sitauangamiza mji huo.” Mwenyezi-Mungu alipomaliza kuzungumza na Abrahamu, alikwenda zake; naye Abrahamu akarudi nyumbani kwake.

Shirikisha
Soma Mwanzo 18

Mwanzo 18:20-33 Swahili Revised Union Version (SRUV)

BWANA akasema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana, basi, nitashuka sasa nione kama wanayotenda ni kiasi cha kilio kilichonijia; na kama sivyo, nitajua. Basi wale watu wakatoka huko wakaelekea Sodoma; lakini Abrahamu alibaki amesimama mbele za BWANA. Abrahamu akakaribia, akasema, Je! Utaharibu mwenye haki pamoja na mwovu? Huenda wakawapo wenye haki hamsini katika mji, utaharibu, wala hutauacha mji kwa ajili ya hao hamsini wenye haki waliomo? La hasha! Usifanye hivyo, ukamwue mwenye haki pamoja na mwovu, mwenye haki awe kama mwovu. Hasha! Mhukumu ulimwengu wote asitende haki? BWANA akasema, Nikiona katika Sodoma wenye haki hamsini mjini, nitapaacha mahali pote kwa ajili yao. Abrahamu akajibu, akasema, Basi, nimeshika kusema na Bwana, nami ni mavumbi na majivu tu. Huenda wakapunguka watano katika wale hamsini wenye haki, je! Utaharibu mji wote kwa kupungua watano? Akasema, Sitauharibu, nikiona humo arubaini na watano. Akazidi tena kusema naye, akinena, Huenda wakaonekana humo arubaini? Akasema, Sitafanya kwa ajili ya hao arubaini. Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema, Huenda wakaonekana huko thelathini? Akasema, Sitafanya, nikiona humo thelathini. Akasema, Tazama, nimeshika kusema na Bwana, huenda wakaonekana huko ishirini? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao ishirini. Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema mara hii tu, Huenda wakaonekana huko kumi? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi. Basi BWANA alipokwisha kuzungumza na Abrahamu, akaenda zake; Abrahamu naye akarudi mahali pake.

Shirikisha
Soma Mwanzo 18

Mwanzo 18:20-33 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

BWANA akasema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana, basi, nitashuka sasa nione kama wanayotenda ni kiasi cha kilio kilichonijia; na kama sivyo, nitajua. Basi wale watu wakatoka huko wakaelekea Sodoma; lakini Ibrahimu alikuwa akali akisimama mbele za BWANA. Ibrahimu akakaribia, akasema, Je! Utaharibu mwenye haki pamoja na mwovu? Huenda wakawapo wenye haki hamsini katika mji, utaharibu, wala hutauacha mji kwa ajili ya hao hamsini wenye haki waliomo? Hasha usifanye hivyo, ukamwue mwenye haki pamoja na mwovu, mwenye haki awe kama mwovu. Hasha; Mhukumu ulimwengu wote asitende haki? BWANA akasema, Nikiona katika Sodoma wenye haki hamsini mjini, nitapaacha mahali pote kwa ajili yao. Ibrahimu akajibu, akasema, Basi, nimeshika kusema na Bwana, nami ni mavumbi na majivu tu. Huenda wakapunguka watano katika wale hamsini wenye haki, je! Utaharibu mji wote kwa kupungua watano? Akasema, Sitauharibu, nikiona humo arobaini na watano. Akazidi tena kusema naye, akinena, Huenda wakaonekana humo arobaini? Akasema, Sitafanya kwa ajili ya hao arobaini. Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema, Huenda wakaonekana huko thelathini? Akasema, Sitafanya, nikiona humo thelathini. Akasema, Tazama, nimeshika kusema na Bwana, huenda wakaonekana huko ishirini? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao ishirini. Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema mara hii tu, Huenda wakaonekana huko kumi? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi. Basi BWANA alipokwisha kuzungumza na Ibrahimu, akaenda zake; Ibrahimu naye akarudi mahali pake.

Shirikisha
Soma Mwanzo 18

Mwanzo 18:20-33 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Basi BWANA akasema, “Kilio dhidi ya Sodoma na Gomora ni kikubwa sana na dhambi yao inasikitisha sana, kwamba nitashuka nione kama waliyoyatenda ni mabaya kiasi cha kilio kilichonifikia. Kama sivyo, nitajua.” Basi wale watu wakageuka wakaenda kuelekea Sodoma, lakini Abrahamu akabaki amesimama mbele za BWANA. Ndipo Abrahamu akamsogelea akasema: “Je, utawaangamiza wenye haki na waovu? Je, ikiwa watakuwepo watu wenye haki hamsini katika mji huo, hivi kweli utauangamiza na wala hutauacha kwa ajili ya hao watu hamsini wenye haki waliomo ndani yake? Hilo na liwe mbali nawe, kufanya jambo kama hilo, kuwaua wenye haki pamoja na waovu, kuwatendea wenye haki sawasawa na waovu. Iwe mbali nawe! Je, Mwamuzi wa dunia yote hatafanya lililo sawa?” BWANA akasema, “Kama nikipata watu hamsini wenye haki katika mji wa Sodoma, nitausamehe huo mji wote kwa ajili yao.” Kisha Abrahamu akasema tena: “Sasa kwa kuwa nimekuwa na ujasiri wa kuzungumza na Bwana, ingawa mimi si kitu bali ni mavumbi na majivu; je, kama hesabu ya wenye haki imepungua watano katika hamsini, utauangamiza huo mji wote kwa ajili ya hao watano waliopungua?” Bwana akamwambia, “Kama nikiwakuta huko watu arobaini na watano, sitauangamiza.” Abrahamu akazungumza naye kwa mara nyingine, “Je, kama huko watapatikana watu arobaini tu?” Akamjibu, “Kwa ajili ya hao arobaini, sitauangamiza.” Ndipo akasema, “Bwana na asikasirike, lakini niruhusu nizungumze. Je, kama huko watakuwepo thelathini tu?” Akajibu, “Sitapaangamiza ikiwa nitawakuta huko watu thelathini.” Abrahamu akasema, “Sasa kwa kuwa nimekuwa na ujasiri sana kuzungumza na Bwana, je, kama wakipatikana huko watu ishirini tu?” Bwana akajibu, “Kwa ajili ya hao ishirini, sitauangamiza.” Abrahamu akasema, “Bwana na asikasirike, lakini niruhusu nizungumze tena mara moja tu. Itakuwaje kama watapatikana huko watu kumi tu?” Bwana akajibu, “Kwa ajili ya hao kumi, sitauangamiza.” BWANA alipomaliza kuzungumza na Abrahamu, akaondoka, naye Abrahamu akarudi nyumbani kwake.

Shirikisha
Soma Mwanzo 18

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha