Mwanzo 15:8-21
Mwanzo 15:8-21 NENO
Lakini Abramu akasema, “Ee Bwana Mungu Mwenyezi, nitawezaje kujua kwamba nitaimiliki?” Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia, “Niletee ndama jike, mbuzi, na kondoo dume, kila mmoja wa miaka mitatu, pamoja na hua na kinda la njiwa.” Abramu akamletea hivi vyote, akampasua kila mnyama vipande viwili, akavipanga kila kimoja kuelekea mwenzake, lakini hata hivyo ndege hakuwapasua vipande viwili. Kisha ndege walao nyama wakatua juu ya mizoga, lakini Abramu akawafukuza. Jua lilipokuwa linatua, Abramu akashikwa na usingizi mzito, na giza nene na la kutisha likaja juu yake. Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia, “Ujue hakika kwamba wazao wako watakuwa wageni katika nchi isiyo yao, nao watafanywa watumwa na kuteswa kwa miaka mia nne. Lakini nitaliadhibu taifa lile watakalolitumikia kama watumwa, na baadaye watatoka huko na mali nyingi. Wewe hata hivyo utaenda kwa baba zako kwa amani, na kuzikwa katika uzee mwema. Katika kizazi cha nne wazao wako watarudi hapa, kwa maana uovu wa Waamori bado haujafikia kipimo.” Jua lilipokuwa limezama na giza limeingia, tanuru la moshi na mwali wa moto unaowaka vikatokea na kupita kati ya vile vipande vya nyama. Siku hiyo Mwenyezi Mungu akafanya agano na Abramu, na kumwambia, “Nitawapa wazao wako nchi hii, kuanzia Kijito cha Misri hadi mto ule mkubwa, Frati: yaani nchi ya Wakeni, Wakenizi, Wakadmoni, Wahiti, Waperizi, Warefai, Waamori, Wakanaani, Wagirgashi na Wayebusi.”