Mwanzo 15:8-21
Mwanzo 15:8-21 SRUV
Akasema, Ee Bwana MUNGU, nipateje kujua ya kwamba nitaimiliki? Akamwambia, Unipatie ndama wa miaka mitatu, na mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo dume wa miaka mitatu, na hua, na mwana njiwa. Akampatia hao wote, akawapasua vipande viwili, akaweka kila kipande kuelekea mwenzake, ila ndege hakuwapasua. Na tai walipotua juu ya mizoga Abramu akawafukuza. Na jua lilipokuwa likichwa usingizi mzito ulimshika Abramu, hofu ya giza kuu ikamwangukia. BWANA akamwambia Abramu, Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa kwa muda wa miaka mia nne. Hata na taifa lile, watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali nyingi. Lakini wewe utakwenda kwa baba zako kwa amani, utazikwa katika uzee mwema. Na kizazi cha nne kitarudi hapa, maana uovu wa Waamori haujatimia bado. Ikawa, jua lilipokuchwa likawa giza, tazama, tanuri ya moshi na mwenge unaowaka ulipita kati ya vile vipande vya nyama. Siku ile BWANA akafanya agano na Abramu, akasema, Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati, Mkeni, na Mkenizi, na Mkadmoni, na Mhiti, na Mperizi, na Mrefai, na Mwamori, na Mkanaani, na Mgirgashi, na Myebusi.