Mwanzo 15:8-21
Mwanzo 15:8-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini Abramu akamwambia, “Ee Mwenyezi-Mungu, nitajuaje kwamba nitaimiliki nchi hii?” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Niletee ndama wa miaka mitatu, mwanambuzi jike wa miaka mitatu, kondoo dume wa miaka mitatu, na hua na kinda la njiwa.” Abramu akamletea hao wote, akamkata kila mnyama vipande viwili, akavipanga katika safu mbili, vikielekeana; lakini ndege hakuwakata vipande viwili. Na tai walipoijia hiyo mizoga, Abramu akawa anawafukuza. Jua lilipokuwa likitua, Abramu alishikwa na usingizi mzito; hofu na giza nene vikamfunika. Hapo Mwenyezi-Mungu akamwambia Abramu, “Ujue hakika ya kwamba wazawa wako watakaa kama wageni katika nchi isiyo yao, watakuwa watumwa na watateswa kwa muda wa miaka 400. Hata hivyo, nitaliadhibu taifa watakalolitumikia, na hatimaye watatoka wakiwa na mali nyingi. Lakini wewe mwenyewe utaishi maisha marefu na kufariki kwa amani. Wazawa wako watarudi hapa katika kizazi cha nne, kwa sababu uovu wa Waamori haujakamilika bado.” Jua lilipokwisha tua na giza kuingia, tanuri ifukayo moshi na mwenge uwakao moto vikapita katikati ya vile vipande vya nyama. Siku hiyo, Mwenyezi-Mungu akafanya agano na Abramu akisema, “Wazawa wako ninawapa nchi hii, toka mto wa Misri hadi ule mto mkubwa wa Eufrate, yaani nchi za Wakeni, Wakenizi, Wakadmoni, Wahiti, Waperizi, Warefai, Waamori, Wakanaani, Wagirgashi na Wayebusi.”
Mwanzo 15:8-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akasema, Ee Bwana MUNGU, nipateje kujua ya kwamba nitaimiliki? Akamwambia, Unipatie ndama wa miaka mitatu, na mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo dume wa miaka mitatu, na hua, na mwana njiwa. Akampatia hao wote, akawapasua vipande viwili, akaweka kila kipande kuelekea mwenzake, ila ndege hakuwapasua. Na tai walipotua juu ya mizoga Abramu akawafukuza. Na jua lilipokuwa likichwa usingizi mzito ulimshika Abramu, hofu ya giza kuu ikamwangukia. BWANA akamwambia Abramu, Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa kwa muda wa miaka mia nne. Hata na taifa lile, watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali nyingi. Lakini wewe utakwenda kwa baba zako kwa amani, utazikwa katika uzee mwema. Na kizazi cha nne kitarudi hapa, maana uovu wa Waamori haujatimia bado. Ikawa, jua lilipokuchwa likawa giza, tazama, tanuri ya moshi na mwenge unaowaka ulipita kati ya vile vipande vya nyama. Siku ile BWANA akafanya agano na Abramu, akasema, Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati, Mkeni, na Mkenizi, na Mkadmoni, na Mhiti, na Mperizi, na Mrefai, na Mwamori, na Mkanaani, na Mgirgashi, na Myebusi.
Mwanzo 15:8-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akasema, Ee Bwana MUNGU, nipateje kujua ya kwamba nitairithi? Akamwambia, Unipatie ndama wa miaka mitatu, na mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo mume wa miaka mitatu, na hua, na mwana njiwa. Akampatia hao wote, akawapasua vipande viwili, akaweka kila kipande kuelekea mwenzake, ila ndege hakuwapasua. Hata tai walipotua juu ya mizoga Abramu akawafukuza. Na jua lilipokuwa likichwa usingizi mzito ulimshika Abramu, hofu ya giza kuu ikamwangukia. BWANA akamwambia Abramu, Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa miaka mia nne. Hata na taifa lile, watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali mengi. Lakini wewe utakwenda kwa baba zako kwa amani, utazikwa katika uzee mwema. Na kizazi cha nne kitarudi hapa, maana haujatimia uovu wa Waamori bado. Ikawa, jua lilipokuchwa likawa giza, tazama, tanuru ya moshi na mwenge unaowaka ulipita kati ya vile vipande vya nyama. Siku ile BWANA akafanya agano na Abramu, akasema, Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati, Mkeni, na Mkenizi, na Mkadmoni, na Mhiti, na Mperizi, na Mrefai, na Mwamori, na Mkanaani, na Mgirgashi, na Myebusi.
Mwanzo 15:8-21 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Lakini Abramu akasema, “Ee BWANA Mwenyezi, nitawezaje kujua kwamba nitapata kuimiliki?” Ndipo BWANA akamwambia, “Niletee mtamba wa ngʼombe, mbuzi na kondoo dume, kila mmoja wa miaka mitatu, pamoja na hua na kinda la njiwa.” Abramu akamletea hivi vyote, akampasua kila mnyama vipande viwili, akavipanga kila kimoja kuelekea mwenzake, lakini hata hivyo ndege, hakuwapasua vipande viwili. Kisha ndege walao nyama wakatua juu ya mizoga, lakini Abramu akawafukuza. Wakati jua lilipokuwa linatua, Abramu akashikwa na usingizi mzito, giza nene na la kutisha likaja juu yake. Kisha BWANA akamwambia, “Ujue hakika kwamba wazao wako watakuwa wageni kwenye nchi ambayo si yao, nao watafanywa watumwa na kuteswa kwa miaka mia nne. Lakini nitaliadhibu taifa lile watakalolitumikia kama watumwa, na baadaye watatoka huko na mali nyingi. Wewe, hata hivyo utakwenda kwa baba zako kwa amani na kuzikwa katika uzee mwema. Katika kizazi cha nne wazao wako watarudi hapa, kwa maana dhambi ya Waamori bado haijafikia kipimo kilichojaa.” Wakati jua lilipokuwa limezama na giza limeingia, tanuru la moshi na mwali wa moto unaowaka vikatokea na kupita kati ya vile vipande vya nyama. Siku hiyo BWANA akafanya Agano na Abramu, na kumwambia, “Nitawapa wazao wako nchi hii, kuanzia Kijito cha Misri hadi mto ule mkubwa, Frati, yaani nchi ya Wakeni, Wakenizi, Wakadmoni, Wahiti, Waperizi, Warefai, Waamori, Wakanaani, Wagirgashi na Wayebusi.”