Mwanzo 14:17-24
Mwanzo 14:17-24 NENO
Abramu aliporudi baada ya kumshinda Mfalme Kedorlaoma na wale wafalme waliojiunga naye, mfalme wa Sodoma akatoka kwenda kumlaki katika Bonde la Shawe (yaani Bonde la Mfalme). Ndipo Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai. Alikuwa kuhani wa Mungu Aliye Juu Sana. Naye akambariki Abramu, akisema, “Abarikiwe Abramu na Mungu Aliye Juu Sana, Muumba wa mbingu na nchi. Abarikiwe Mungu Aliye Juu Sana, ambaye amewaweka adui zako mkononi mwako.” Ndipo Abramu akampa Melkizedeki sehemu ya kumi ya kila kitu. Mfalme wa Sodoma akamwambia Abramu, “Nipe hao watu, nawe uchukue hizo mali.” Lakini Abramu akamwambia mfalme wa Sodoma, “Nimeinua mkono wangu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu Aliye Juu Sana, Muumba wa mbingu na dunia, na nimeapa kwamba sitapokea kitu chochote kilicho chako, hata kama ni uzi au gidamu ya kiatu, ili kamwe usije ukasema, ‘Nimemtajirisha Abramu.’ Sitapokea chochote, ila kile tu watu wangu walichokula, na sehemu ambayo ni fungu la watu walioenda pamoja nami, ambao ni Aneri, Eshkoli na Mamre. Wao na wapewe fungu lao.”