Mwanzo 14:17-24
Mwanzo 14:17-24 Biblia Habari Njema (BHN)
Abramu aliporudi baada ya kumshinda mfalme Kedorlaomeri na wenzake, mfalme wa Sodoma alitoka kwenda kumlaki katika bonde la Shawe, (yaani Bonde la Mfalme). Naye Melkisedeki, mfalme wa mji wa Salemu, ambaye alikuwa kuhani wa Mungu Mkuu, akaleta mkate na divai, akambariki Abramu akisema, “Abramu na abarikiwe na Mungu Mkuu, Muumba mbingu na dunia! Na atukuzwe Mungu Mkuu, aliyewatia adui zako mikononi mwako!” Naye Abramu akampa Melkisedeki mchango wake sehemu ya kumi ya vitu vyote alivyokuwa navyo. Mfalme wa Sodoma akamwambia Abramu, “Nipe hao watu, lakini jichukulie mali yote wewe mwenyewe.” Lakini Abramu akamwambia mfalme wa Sodoma, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu Mkuu, aliyeumba mbingu na dunia, kwamba sitachukua uzi au kamba ya kiatu, wala chochote kilicho chako, usije ukajivuna na kusema kwamba umenitajirisha. Basi, sitachukua chochote isipokuwa tu vile vitu vijana wangu walivyokula na sehemu ya wale waliokuwa pamoja nami, Aneri, Eshkoli na Mamre ambao wana haki nayo.”
Mwanzo 14:17-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Abramu aliporudi kutoka kumpiga Kedorlaoma na wale wafalme waliokuwa pamoja naye, mfalme wa Sodoma akatoka amlaki katika bonde la Shawe, nalo ni Bonde la Mfalme. Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye Juu Sana. Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye Juu Sana, Muumba mbingu na nchi. Ahimidiwe Mungu Aliye Juu Sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. Abramu akampa fungu la kumi la vitu vyote. Mfalme wa Sodoma akamwambia Abramu, Nipe mimi hao watu, na hizo mali uchukue wewe. Abramu akamwambia mfalme wa Sodoma, Nimeinua mkono wangu kwa BWANA, Mungu Aliye Juu sana, Muumba mbingu na nchi, ya kuwa sitatwaa uzi wala gidamu ya kiatu wala chochote kilicho chako, usije ukasema, Nimemtajirisha Abramu; isipokuwa hivyo walivyokula vijana, na sehemu za watu waliokwenda nami, yaani, Aneri, na Eshkoli, na Mamre; na watwae wao sehemu zao.
Mwanzo 14:17-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Abramu aliporudi kutoka kumpiga Kedorlaoma na wale wafalme waliokuwa pamoja naye, mfalme wa Sodoma akatoka amlaki katika bonde la Shawe, nalo ni Bonde la Mfalme. Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana. Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi. Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. Abramu akampa fungu la kumi la vitu vyote. Mfalme wa Sodoma akamwambia Abramu, Nipe mimi hao watu, na hizo mali uchukue wewe. Abramu akamwambia mfalme wa Sodoma, Nimeinua mkono wangu kwa BWANA, Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi, ya kuwa sitatwaa uzi wala gidamu ya kiatu wala cho chote kilicho chako, usije ukasema, Nimemtajirisha Abramu; isipokuwa hivyo walivyokula vijana, na sehemu za watu waliokwenda nami, yaani, Aneri, na Eshkoli, na Mamre; na watwae wao sehemu zao.
Mwanzo 14:17-24 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Abramu aliporudi baada ya kumshinda Mfalme Kedorlaoma na wale wafalme waliojiunga naye, mfalme wa Sodoma akatoka kwenda kumlaki katika Bonde la Shawe (yaani Bonde la Mfalme). Ndipo Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai. Alikuwa kuhani wa Mungu Aliye Juu Sana. Naye akambariki Abramu, akisema, “Abarikiwe Abramu na Mungu Aliye Juu Sana, Muumba wa mbingu na nchi. Abarikiwe Mungu Aliye Juu Sana, ambaye amewaweka adui zako mkononi mwako.” Ndipo Abramu akampa Melkizedeki sehemu ya kumi ya kila kitu. Mfalme wa Sodoma akamwambia Abramu, “Nipe hao watu, nawe uchukue hizo mali.” Lakini Abramu akamwambia mfalme wa Sodoma, “Nimeinua mkono wangu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu Aliye Juu Sana, Muumba wa mbingu na dunia, na nimeapa kwamba sitapokea kitu chochote kilicho chako, hata kama ni uzi au gidamu ya kiatu, ili kamwe usije ukasema, ‘Nimemtajirisha Abramu.’ Sitapokea chochote, ila kile tu watu wangu walichokula, na sehemu ambayo ni fungu la watu walioenda pamoja nami, ambao ni Aneri, Eshkoli na Mamre. Wao na wapewe fungu lao.”