Ezra 7
7
Ezra awasili Yerusalemu
1Baada ya mambo haya, wakati wa utawala wa Artashasta mfalme wa Uajemi, Ezra mwana wa Seraya, mwana wa Azaria, mwana wa Hilkia, 2mwana wa Shalumu, mwana wa Sadoki, mwana wa Ahitubu, 3mwana wa Amaria, mwana wa Azaria, mwana wa Merayothi, 4mwana wa Zerahia, mwana wa Uzi, mwana wa Buki, 5mwana wa Abishua, mwana wa Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa kuhani mkuu Haruni. 6Huyu Ezra alipanda kutoka Babeli. Alikuwa mwandishi mwenye ujuzi mwingi katika Torati ya Musa, ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, alikuwa ametoa. Mfalme alikuwa amempa Ezra kila kitu alichoomba, kwa maana Mwenyezi Mungu, Mungu wake, alikuwa pamoja naye. 7Baadhi ya Waisraeli, wakiwemo makuhani, Walawi, waimbaji, mabawabu na watumishi wa Hekalu#7:7 yaani Wanethini (pia 7:24)., nao walikuja Yerusalemu mwaka wa saba wa utawala wa Mfalme Artashasta.
8Ezra aliwasili Yerusalemu mwezi wa tano wa mwaka wa saba wa utawala wa Mfalme Artashasta. 9Ezra alianza safari yake kutoka Babeli siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, naye akawasili Yerusalemu siku ya kwanza ya mwezi wa tano, kwa kuwa mkono wa neema wa Mungu wake ulikuwa juu yake. 10Kwa maana Ezra alikuwa amejitoa kwa moyo wote kujifunza na kushika Torati ya Mwenyezi Mungu na kuwafundisha Waisraeli amri na sheria zake.
Barua ya Ezra kutoka kwa Mfalme Artashasta
11Hii ni nakala ya barua ambayo Mfalme Artashasta alimpa Ezra aliyekuwa kuhani na mwalimu, mtu aliyeelimika katika mambo kuhusu maagizo na amri za Mwenyezi Mungu kwa Israeli.
12Artashasta, mfalme wa wafalme,
Kwa Ezra kuhani, mwalimu wa Torati ya Mungu wa mbinguni:
Salamu.
13Sasa naamuru kwamba mtu yeyote Mwisraeli katika ufalme wangu, pamoja na makuhani na Walawi, ambaye anataka kwenda Yerusalemu pamoja nawe aweza kwenda. 14Unatumwa na mfalme na washauri wake saba kuchunguza habari za Yuda na Yerusalemu kulingana na Torati ya Mungu wako, iliyo mkononi mwako. 15Zaidi ya hayo, uchukue fedha na dhahabu ambazo mfalme na washauri wake wamempa Mungu wa Israeli kwa hiari, Mungu ambaye maskani yake yako Yerusalemu, 16pia fedha na dhahabu zote unazoweza kupata kutoka jimbo la Babeli, pamoja na sadaka za hiari watakazotoa watu na makuhani kwa ajili ya Hekalu la Mungu wao ambalo liko Yerusalemu. 17Hakikisha kwamba fedha hizi zimetumika kununua mafahali, kondoo dume na wana-kondoo pamoja na sadaka za nafaka na sadaka za vinywaji, uvitoe dhabihu juu ya madhabahu ya Hekalu la Mungu wenu katika Yerusalemu.
18Kisha wewe na Wayahudi ndugu zako mnaweza kufanya lolote linaloonekana jema sana kwa fedha na dhahabu zilizosalia, kulingana na mapenzi ya Mungu wenu. 19Uvitoe kwa Mungu wa Yerusalemu vyombo vyote ulivyokabidhiwa kwa ajili ya ibada katika Hekalu la Mungu wako. 20Kitu kingine chochote kinachohitajika kwa ajili ya Hekalu la Mungu wenu ambacho unatakiwa kukitoa, unaweza kukitoa kutoka hazina ya mfalme.
21Mimi, Mfalme Artashasta, sasa naagiza watunza hazina wote wa Ng’ambo ya Mto Frati kutoa kwa bidii chochote kwa Ezra kuhani na mwalimu wa Torati ya Mungu wa mbinguni atakachohitaji kwenu, 22talanta mia moja#7:22 Talanta 100 za fedha ni sawa na kilo 3,400. za fedha, ngano kori mia moja#7:22 Kori 100 za ngano ni sawa na kilo 10,000., divai bathi mia moja#7:22 Bathi 100 za divai ni sawa na lita 2,000., mafuta ya zeituni bathi mia moja, na chumvi kiasi chochote. 23Chochote ambacho Mungu wa mbinguni ameagiza, kifanyike kwa ukamilifu kwa ajili ya Hekalu la Mungu wa mbinguni. Kwa nini pawepo ghadhabu dhidi ya utawala wa mfalme na wanawe? 24Pia ninyi fahamuni kuwa hamna mamlaka ya kuwatoza kodi, ushuru au ada makuhani, Walawi, waimbaji, mabawabu, watumishi wa Hekalu au wafanyakazi wengine kwenye nyumba ya Mungu.
25Nawe Ezra, kufuatana na hekima ya Mungu wenu uliyo nayo, weka mahakimu na waamuzi wote wanaozifahamu sheria za Mungu wenu, ili watoe haki kwa watu wote wa Ng’ambo ya Mto Frati. Nawe inakupasa umfundishe yeyote ambaye hazifahamu. 26Yeyote ambaye hataitii Torati ya Mungu wenu na pia sheria ya mfalme, hakika lazima aadhibiwe kwa kuuawa, kuhamishwa, kunyang’anywa mali au kufungwa gerezani.
27Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zetu, Mungu ambaye kwa njia hii ameweka ndani ya moyo wa mfalme kuipa heshima nyumba ya Mwenyezi Mungu iliyo Yerusalemu, kwa namna hii 28ambaye ameniongezea kibali chake mbele ya mfalme, washauri wake na maafisa wote wa mfalme wenye uwezo. Kwa kuwa mkono wa Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, ulikuwa pamoja nami, nilijipa moyo nikakusanya watu walio viongozi kutoka Israeli wakwee pamoja nami.
Iliyochaguliwa sasa
Ezra 7: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.