Ezra 6
6
Amri ya Dario
1Kisha Mfalme Dario alitoa amri, nao wakafanya uchunguzi katika kumbukumbu zilizohifadhiwa katika hazina huko Babeli. 2Kitabu kilipatikana katika ngome la Ekbatana katika jimbo la Umedi; kilikuwa kimeandikwa hivi:
Kumbukumbu:
3Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Mfalme Koreshi, mfalme alitoa amri kuhusu Hekalu la Mungu katika Yerusalemu:
Hekalu na lijengwe upya likiwa mahali pa kutolea dhabihu, na misingi yake ijengwe. Iwe na kimo cha mikono sitini#6:3 Mikono 60 ni sawa na mita 27., upana wa mikono sitini, 4kuta zijengwe kwa safu tatu za mawe makubwa kisha ifuate safu moja ya mbao. Gharama zitalipwa kutoka hazina ya mfalme. 5Pia, vyombo vya dhahabu na vya fedha vya nyumba ya Mungu, ambavyo Nebukadneza alivichukua kutoka Hekalu huko Yerusalemu akavileta Babeli, yapasa virudishwe mahali pake ndani ya Hekalu huko Yerusalemu, yapasa viwekwe ndani ya nyumba ya Mungu.
6Sasa basi, Tatenai, mtawala wa Ng’ambo ya Mto Frati na Shethar-Bozenai pamoja na ninyi, maafisa wenzao wa jimbo hilo kaeni mbali na mahali hapo. 7Msiingilie kazi ya Hekalu hili la Mungu. Mwacheni mtawala wa Wayahudi na viongozi Wayahudi wajenge upya nyumba hii ya Mungu mahali pake.
8Zaidi ya hayo, hapa natoa amri kuhusu mtakalofanya kwa ajili ya wazee wa Wayahudi katika ujenzi wa nyumba hii ya Mungu:
Gharama za watu hawa zitalipwa kikamilifu kutoka hazina ya mfalme, kutoka mapato ya Ng’ambo ya Mto Frati, ili ujenzi usisimame. 9Chochote kinachohitajika kama mafahali wachanga, kondoo dume, wana-kondoo kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa kwa Mungu wa mbinguni, ngano, chumvi, divai na mafuta kama vitakavyohitajika na makuhani huko Yerusalemu, lazima wapewe kila siku pasipo kukosa, 10ili waweze kutoa dhabihu inayompendeza Mungu wa mbinguni na kumwombea mfalme na wanawe hali njema.
11Zaidi ya hayo, ninaamuru kwamba mtu yeyote atakayebadilisha amri hii, boriti itang’olewa kutoka nyumba yake, ichongwe upande mmoja na atumbuliwe nayo. Kwa ajili ya kosa hili nyumba yake ifanywe lundo la taka. 12Naye Mungu, aliyeliweka Jina lake huko, amwangushe mfalme yeyote au watu watakaoinua mikono kubadili amri hii au kuharibu Hekalu hili ambalo liko Yerusalemu.
Mimi Dario nimetoa amri hii. Nayo itekelezwe kwa bidii na kwa makini.
Hekalu linakamilika na kuwekwa wakfu
13Kwa sababu ya amri aliyotoa Mfalme Dario, Tatenai mtawala wa Ng’ambo ya Mto Frati na Shethar-Bozenai na wenzao wakaitekeleza kwa bidii na kwa makini. 14Hivyo wazee wa Wayahudi waliendelea kujenga na kustawi kutokana na mahubiri ya manabii Hagai na Zekaria, wa uzao wa Ido. Wakakamilisha ujenzi wa Hekalu kulingana na agizo la Mungu wa Israeli na amri ya Koreshi, Dario na Artashasta wafalme wa Uajemi. 15Hekalu lilikamilika siku ya kumi na mbili ya mwezi wa Adari, ndio mwezi wa tatu, katika mwaka wa sita wa utawala wa Mfalme Dario.
16Kisha watu wa Israeli: makuhani, Walawi na wengine wote waliohamishwa, wakaadhimisha kule kuwekwa wakfu nyumba ya Mungu kwa shangwe. 17Kwa ajili ya kuwekwa wakfu nyumba hii ya Mungu walitoa mafahali mia moja, kondoo dume mia mbili, wana-kondoo mia nne; sadaka kwa ajili ya dhambi ya Israeli wote walitoa beberu kumi na wawili, mmoja kwa ajili ya kila kabila la Israeli. 18Wakawaweka makuhani katika nafasi zao na Walawi wakawekwa katika makundi yao ya huduma kwa Mungu huko Yerusalemu, kulingana na ilivyoandikwa katika Kitabu cha Musa.
Pasaka
19Katika siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza, waliorudi kutoka uhamishoni wakaadhimisha Pasaka. 20Makuhani na Walawi walikuwa wamekwisha kujitakasa na hivyo wakatakasika. Walawi wakachinja kondoo wa Pasaka kwa ajili ya wana wa waliorudi kutoka utumwani uhamishoni, kwa ajili ya ndugu zao makuhani na wao wenyewe. 21Hivyo Waisraeli waliorudi kutoka uhamishoni wakala Pasaka, pamoja na wale waliokuwa wamejitenga na matendo ya unajisi wa Mataifa jirani ili kumtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli. 22Kwa muda wa siku saba waliiadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu kwa furaha, kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa amewajaza furaha kwa kubadilisha nia ya mfalme wa Ashuru kwamba awasaidie ujenzi wa nyumba ya Mungu, Mungu wa Israeli.
Iliyochaguliwa sasa
Ezra 6: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.