Ezekieli 47:1-12
Ezekieli 47:1-12 NENO
Yule mtu akanirudisha kwenye ingilio la Hekalu, nami nikaona maji yakitoka chini ya kizingiti cha Hekalu yakitiririkia upande wa mashariki (kwa maana upande wa mbele wa Hekalu ulielekea mashariki). Maji yalikuwa yakitoka chini upande wa kusini wa Hekalu, kusini mwa madhabahu. Ndipo akanitoa nje kupitia lango la kaskazini na kunizungusha mpaka kwenye lango la nje linaloelekea mashariki, nayo maji yalikuwa yakitiririka kutoka upande wa kusini. Mtu yule alipoenda upande wa mashariki akiwa na kamba ya kupimia mkononi mwake, akapima dhiraa elfu moja, kisha akanipitisha kwenye hayo maji ambayo yalifika kwenye vifundo vya miguu. Akapima dhiraa elfu moja nyingine na kunipitisha kwenye hayo maji ambayo yalifika magotini. Akapima dhiraa nyingine elfu moja na kunipitisha kwenye hayo maji ambayo yalifika kiunoni. Akapima tena dhiraa elfu moja nyingine, lakini wakati huu yalikuwa mto ambao sikuweza kuvuka, kwa kuwa maji yalikuwa na kina kirefu ambacho ni cha kuogelea, mto ambao hakuna mtu angeweza kuuvuka. Akaniuliza, “Je, mwanadamu, unaona hili?” Kisha akanirudisha kwenye ukingo wa huo mto. Nilipofika pale, nikaona idadi kubwa ya miti kila upande wa ule mto. Akaniambia, “Haya maji yanatiririka kuelekea nchi ya mashariki na kushuka hadi Araba, ambapo huingia Baharini. Yanapomwagikia kwenye hiyo Bahari, maji hayo huponywa na kuwa safi. Popote mto huu unatakapofika, kila kiumbe hai kinachoingia ndani ya hayo maji kitaishi. Nako kutakuwa na samaki wengi mno, mara maji haya yatakapofika huko. Maji hayo yatakuwa hai, na kila kitu kitaishi popote mto utakapofika. Wavuvi watasimama kando ya bahari; kuanzia En-Gedi hadi En-Eglaimu kutakuwa mahali pa kutandaza nyavu za kuvulia samaki. Samaki watakuwa wa aina nyingi, kama samaki wa Bahari Kuu. Lakini madimbwi yake na mabwawa yake hayatakuwa na maji yanayofaa kunywa, bali yatabakia kuwa maji ya chumvi. Miti ya matunda ya kila aina itaota kwenye kingo zote mbili za mto huu. Majani yake hayatanyauka wala haitaacha kuwa na matunda katika matawi yake. Kila mwezi kutakuwa na matunda, kwa sababu maji yanayotoka patakatifu yataitiririkia. Matunda yake yatakuwa chakula na majani yake yatakuwa dawa.”