Ezekieli 47:1-12
Ezekieli 47:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Yule mtu akanirudisha kwenye kiingilio cha hekalu. Huko, maji yalikuwa yakitoka chini ya kizingiti cha hekalu kuelekea upande wa mashariki, (kwa maana hekalu lilielekea mashariki). Maji yalikuwa yakitiririka kutoka chini ya upande wa kusini wa lango la hekalu, kusini mwa madhabahu. Kisha akanipeleka nje kwa njia ya lango la kaskazini. Akanizungusha kwa njia ya nje mpaka lango la nje, upande wa mashariki; na maji yalikuwa yanatoka upande wa kusini. Yule mtu, kwa ufito wake wa kupimia, akapima mita 500 kwenda chini upande wa mashariki, akanipitisha kwenye maji. Maji yalifika kwenye nyayo tu. Kisha akapima tena mita 500, akaniongoza kuvuka maji. Maji yakafika mpaka magoti yangu. Akapima tena mita nyingine 500, naye akaniongoza kuvuka maji. Maji yakafika mpaka kiunoni mwangu. Akapima mita 500 nyingine, na mto ukawa na kilindi kirefu hata sikuweza kuuvuka tena. Haikuwezekana kuuvuka ila kwa kuogelea. Yule mtu akaniambia, “Wewe mtu! Zingatia mambo hayo yote kwa makini.” Kisha, akanirudisha mpaka ukingo wa mto. Nilipofika huko niliona miti mingi sana kwenye kingo za mto. Akaniambia, “Maji haya yanatiririka kupitia nchini hadi Araba; na yakifika huko yatayafanya maji ya Bahari ya Chumvi kuwa maji mazuri. Kila mahali mto huu utakapopita, kutaishi aina zote za wanyama na samaki. Mto huu utayafanya maji ya Bahari ya Chumvi kuwa maji baridi. Kokote utakakopita utaleta uhai. Wavuvi watasimama ufuoni mwa bahari, na eneo kutoka Engedi mpaka En-eglaimu litakuwa la kuanikia nyavu zao. Kutakuwa na aina nyingi za samaki kama zilivyo katika Bahari ya Mediteranea. Lakini sehemu zake zenye majimaji na mabwawa kando ya bahari, hazitakuwa na maji mazuri. Bali hayo yatabaki kuwa maji ya chumvi. Kisha ukingoni mwa mto huo kutaota kila namna ya miti itoayo chakula. Majani yake hayatanyauka wala miti hiyo haitaacha kuzaa matunda. Itazaa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu inapata maji yanayotiririka kutoka maskani ya Mungu. Matunda yake yatakuwa chakula na majani yake yatatumika kuponya magonjwa.”
Ezekieli 47:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Baadaye akanileta tena mpaka lango la nyumba; na tazama, maji yalitoka chini ya kizingiti cha nyumba, kwa njia ya mashariki, maana upande wa mbele wa nyumba ulielekea upande wa mashariki; nayo maji yakashuka toka chini ya upande wa kulia wa nyumba, upande wa kusini wa madhabahu. Ndipo akanileta nje kwa njia ya lango upande wa kaskazini, akanizungusha kwa njia ya nje mpaka lango la nje, kwa njia yake iliyoelekea mashariki; na tazama, maji yalitoka upande wa kulia. Na alipotoka mtu yule, mwenye uzi wa kupimia mkononi mwake, akielekea mashariki, akapima dhiraa elfu moja, akanivusha maji yale; maji yakafika mpaka katika vifundo vya miguu. Kisha akapima dhiraa elfu moja, akanivusha maji yale, maji yakafika mpaka magoti. Kisha akapima dhiraa elfu moja, akanivusha, maji yakafika mpaka viuno. Kisha akapima dhiraa elfu moja, yakawa mto nisioweza kuuvuka; maana maji yamezidi, maji ya kuogelea, mto usiovukika. Akaniambia, Mwanadamu, je! Umeona haya? Kisha akanichukua akanirudisha mpaka ukingo wa mto. Basi nikiisha kurudi, tazama, kando ya ukingo wa mto ilikuwapo miti mingi sana, upande huu na upande huu. Ndipo akaniambia, Maji haya yanatoka kwenda pande za nchi ya mashariki, nayo yanashuka mpaka Araba, na kuingia katika bahari; maji yatokezwayo yataingia baharini, na maji yake yatakuwa safi. Tena itakuwa, kila kiumbe hai kisongamanacho, kila mahali itakapofika mito hiyo, kitaishi; kutakuwapo wingi mkubwa wa samaki, kwa sababu maji haya yamefika huko maana maji yale yatakuwa safi, na kila kitu kitaishi popote utakapofika mto huo. Tena itakuwa, wavuvi watasimama karibu nao; toka Engedi mpaka En-eglaimu, patakuwa ni mahali pa kutandazia nyavu; samaki wao watakuwa namna zao mbalimbali, kama samaki wa bahari kubwa, wengi sana. Bali mahali penye matope, na maziwa yake, hayataponywa; yataachwa yawe ya chumvi. Na karibu na mto, juu ya ukingo wake, upande huu na upande huu, utamea kila mti wa chakula, ambao majani yake hayatanyauka, wala matunda yake hayataisha kamwe; utatoa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu maji yake yanatoka mahali patakatifu; na matunda yake yatakuwa ni chakula; na majani yake yatakuwa ni dawa.
Ezekieli 47:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Baadaye akanileta tena mpaka lango la nyumba; na tazama, maji yalitoka chini ya kizingiti cha nyumba, kwa njia ya mashariki, maana upande wa mbele wa nyumba ulielekea upande wa mashariki; nayo maji yakashuka toka chini ya upande wa kuume wa nyumba, upande wa kusini wa madhabahu. Ndipo akanileta nje kwa njia ya lango upande wa kaskazini, akanizungusha kwa njia ya nje mpaka lango la nje, kwa njia yake iliyoelekea mashariki; na tazama, maji yalitoka upande wa kuume. Na alipotoka mtu yule, mwenye uzi wa kupimia mkononi mwake, kwenda masharikini, akapima dhiraa elfu, akanivusha maji yale; maji yakafika mpaka viweko vya miguu. Kisha akapima dhiraa elfu, akanivusha maji yale, maji yakafika mpaka magoti. Kisha akapima dhiraa elfu, akanivusha, maji yakafika mpaka viuno. Kisha akapima dhiraa elfu, yakawa mto nisioweza kuuvuka; maana maji yamezidi, maji ya kuogelea, mto usiovukika. Akaniambia, Mwanadamu, je! Umeona haya? Kisha akanichukua akanirudisha mpaka ukingo wa mto. Basi nikiisha kurudi, tazama, kando ya ukingo wa mto ilikuwapo miti mingi sana, upande huu na upande huu. Ndipo akaniambia, Maji haya yanatoka kwenda pande za nchi ya mashariki, nayo yanashuka mpaka Araba, na kuingia katika bahari; maji yatokezwayo yataingia baharini, na maji yake yataponyeka. Tena itakuwa, kila kiumbe hai kisongamanacho, kila mahali itakapofika mito hiyo, kitaishi; kutakuwapo wingi mkubwa wa samaki, kwa sababu maji haya yamefika huko maana maji yale yataponyeka, na kila kitu kitaishi po pote utakapofikilia mto huo. Tena itakuwa, wavuvi watasimama karibu nao; toka Engedi mpaka En-eglaimu, patakuwa ni mahali pa kutandazia nyavu; samaki wao watakuwa namna zao mbalimbali, kama samaki wa bahari kubwa, wengi sana. Bali mahali penye matope, na maziwa yake, hayataponywa; yataachwa yawe ya chumvi. Na karibu na mto, juu ya ukingo wake, upande huu na upande huu, utamea kila mti wa chakula, ambao majani yake hayatanyauka, wala matunda yake hayatatindika kamwe; utatoa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu maji yake yanatoka mahali patakatifu; na matunda yake yatakuwa ni chakula; na majani yake yatakuwa ni dawa.
Ezekieli 47:1-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yule mtu akanirudisha mpaka kwenye ingilio la Hekalu, nami nikaona maji yakitoka chini ya kizingiti cha Hekalu yakitiririkia upande wa mashariki (kwa maana upande wa mbele wa Hekalu ulielekea mashariki). Maji yalikuwa yakitoka chini upande wa kusini wa Hekalu, kusini mwa madhabahu. Ndipo akanitoa nje kupitia lango la kaskazini na kunizungusha mpaka kwenye lango la nje linaloelekea mashariki, nayo maji yalikuwa yakitiririka kutoka upande wa kusini. Mtu yule alipokwenda upande wa mashariki akiwa na kamba ya kupimia mkononi mwake, akapima dhiraa 1,000 kisha akanipitisha kwenye hayo maji ambayo yalifika kwenye vifundo vya miguu. Akapima dhiraa 1,000 nyingine na kunipitisha kwenye hayo maji ambayo yalifika magotini. Akapima dhiraa nyingine 1,000 na kunipitisha kwenye hayo maji ambayo yalifika kiunoni. Akapima tena dhiraa 1,000 nyingine, lakini wakati huu yalikuwa mto ambao sikuweza kuvuka, kwa kuwa maji yalikuwa na kina kirefu ambacho ni cha kuogelea, mto ambao hakuna mtu yeyote ambaye angeweza kuvuka. Akaniuliza, “Je, mwanadamu, unaona hili?” Kisha akanirudisha mpaka kwenye ukingo wa huo mto. Nilipofika pale, nikaona idadi kubwa ya miti kila upande wa ule mto. Akaniambia, “Haya maji yanatiririka kuelekea nchi ya mashariki na kushuka mpaka Araba, ambapo huingia Baharini. Yanapomwagikia kwenye hiyo Bahari, maji yaliyoko humo huponywa na kuwa safi. Popote mto huu uendapo kila kiumbe hai kinachoyaparamia hayo maji kitaishi, nako kutakuwa na samaki wengi mno, mara maji haya yafikapo huko. Maji hayo yatakuwa hai na kila kitu kitakachoishi kule mto uendako. Wavuvi watasimama kando ya bahari, kuanzia En-Gedi hadi En-Eglaimu huko patakuwa mahali pa kutandaza nyavu za kuvulia samaki. Samaki watakuwa wa aina nyingi, kama samaki wa Bahari Kuu Lakini madimbwi yake na mabwawa yake hayatakuwa na maji yanayofaa kunywa, bali yatabakia kuwa maji ya chumvi. Miti ya matunda ya kila aina itaota kwenye kingo zote mbili za mto huu. Majani yake hayatanyauka wala haitaacha kuwa na matunda katika matawi yake. Kila mwezi kutakuwa na matunda, kwa sababu maji yatokayo patakatifu yanaitiririkia. Matunda yake yatakuwa chakula na majani yake yatakuwa dawa.”