Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 36:16-38

Ezekieli 36:16-38 NEN

Neno la BWANA likanijia tena, kusema: “Mwanadamu, nyumba ya Israeli walipokuwa wakiishi katika nchi yao wenyewe, waliinajisi kwa mwenendo wao na matendo yao. Mwenendo wao mbele zangu ulikuwa kama mwanamke aliye katika hedhi. Hivyo nilimwaga ghadhabu yangu juu yao kwa sababu walikuwa wamemwaga damu katika nchi na kwa sababu walikuwa wameitia nchi unajisi kwa sanamu zao. Nikawatawanya miongoni mwa mataifa, nao wakaenda huku na huko katika nchi mbalimbali, nikawahukumu sawasawa na mwenendo wao na matendo yao. Tena popote walipokwenda miongoni mwa mataifa walilitia unajisi Jina langu takatifu, kwa kuwa watu walisema kuwahusu, ‘Hawa ndio watu wa BWANA, lakini imewapasa kuondoka katika nchi yake.’ Lakini niliwahurumia kwa ajili ya Jina langu takatifu, ambalo nyumba ya Israeli imelitia unajisi miongoni mwa mataifa huko walikokwenda. “Kwa hiyo iambie nyumba ya Israeli, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Si kwa ajili yako, ee nyumba ya Israeli, kwamba ninafanya mambo haya, bali ni kwa ajili ya Jina langu takatifu, ambalo mmelitia unajisi miongoni mwa mataifa mliyoyaendea. Nitauonyesha utakatifu wa Jina langu kuu, ambalo limetiwa unajisi miongoni mwa mataifa, jina ambalo limetiwa unajisi miongoni mwao. Ndipo mataifa watakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA, asema BWANA Mwenyezi, nitakapojionyesha mwenyewe kuwa mtakatifu kwa kuwapitia ninyi mbele ya macho yao. “ ‘Kwa kuwa nitawaondoa ninyi toka mataifa, nitawakusanya kutoka nchi zote na kuwarudisha kwenye nchi yenu wenyewe. Nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi, nitawatakasa kutoka uchafu wenu wote na kutoka sanamu zenu zote. Nitawapa moyo mpya na kuweka roho mpya ndani yenu, nitaondoa ndani yenu moyo wenu wa jiwe na kuwapa moyo wa nyama. Nami nitaweka Roho yangu ndani yenu na kuwafanya ninyi mfuate amri zangu na kuwafanya kuwa waangalifu kuzishika sheria zangu. Mtaishi katika nchi niliyowapa baba zenu, ninyi mtakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wenu. Nitawaokoa ninyi kutoka unajisi wenu wote. Nitaiita nafaka na kuiongeza iwe nyingi sana nami sitaleta njaa juu yenu. Nitaongeza matunda ya miti na mazao ya mashamba, ili kwamba msipate tena aibu miongoni mwa mataifa kwa ajili ya njaa. Ndipo mtakapozikumbuka njia zenu za uovu na matendo yenu maovu, nanyi mtajichukia wenyewe kwa ajili ya dhambi zote na matendo yenu ya kuchukiza. Ninataka ninyi mjue kwamba sifanyi hili kwa ajili yenu, asema BWANA Mwenyezi. Oneni aibu na mkatahayari kwa ajili ya mwenendo wenu, ee nyumba ya Israeli! “ ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Siku ile nitakapowasafisha kutoka dhambi zenu zote, nitarudisha watu waishi katika miji yenu na magofu yatajengwa upya. Nchi iliyokuwa ukiwa italimwa badala ya kukaa ukiwa machoni mwa wale wote wanaopita ndani yake. Watasema, “Hii nchi iliyokuwa imeachwa ukiwa sasa imekuwa kama bustani ya Edeni, miji ile iliyokuwa magofu, ukiwa na kuangamizwa, sasa imejengewa ngome na kukaliwa na watu.” Ndipo mataifa yanayowazunguka yaliyobakia watakapojua kuwa Mimi BWANA nimejenga tena kile kilichoharibiwa na nimepanda tena kile kilichokuwa ukiwa. Mimi BWANA nimenena, nami nitalifanya.’ “Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Mara nyingine tena nitasikia maombi ya nyumba ya Israeli na kuwatendea jambo hili: Nitawafanya watu wake kuwa wengi kama kondoo, kuwa wengi kama kundi la kondoo kwa ajili ya dhabihu huko Yerusalemu wakati wa sikukuu zao za wakati ulioamriwa. Hivyo ndivyo miji iliyokuwa magofu itajazwa na makundi ya watu. Ndipo watakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA.”

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Ezekieli 36:16-38

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha