Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 36:16-38

Ezekieli 36:16-38 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Neno la BWANA likanijia tena, kusema: “Mwanadamu, nyumba ya Israeli walipokuwa wakiishi katika nchi yao wenyewe, waliinajisi kwa mwenendo wao na matendo yao. Mwenendo wao mbele zangu ulikuwa kama mwanamke aliye katika hedhi. Hivyo nilimwaga ghadhabu yangu juu yao kwa sababu walikuwa wamemwaga damu katika nchi na kwa sababu walikuwa wameitia nchi unajisi kwa sanamu zao. Nikawatawanya miongoni mwa mataifa, nao wakaenda huku na huko katika nchi mbalimbali, nikawahukumu sawasawa na mwenendo wao na matendo yao. Tena popote walipokwenda miongoni mwa mataifa walilitia unajisi Jina langu takatifu, kwa kuwa watu walisema kuwahusu, ‘Hawa ndio watu wa BWANA, lakini imewapasa kuondoka katika nchi yake.’ Lakini niliwahurumia kwa ajili ya Jina langu takatifu, ambalo nyumba ya Israeli imelitia unajisi miongoni mwa mataifa huko walikokwenda. “Kwa hiyo iambie nyumba ya Israeli, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Si kwa ajili yako, ee nyumba ya Israeli, kwamba ninafanya mambo haya, bali ni kwa ajili ya Jina langu takatifu, ambalo mmelitia unajisi miongoni mwa mataifa mliyoyaendea. Nitauonyesha utakatifu wa Jina langu kuu, ambalo limetiwa unajisi miongoni mwa mataifa, jina ambalo limetiwa unajisi miongoni mwao. Ndipo mataifa watakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA, asema BWANA Mwenyezi, nitakapojionyesha mwenyewe kuwa mtakatifu kwa kuwapitia ninyi mbele ya macho yao. “ ‘Kwa kuwa nitawaondoa ninyi toka mataifa, nitawakusanya kutoka nchi zote na kuwarudisha kwenye nchi yenu wenyewe. Nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi, nitawatakasa kutoka uchafu wenu wote na kutoka sanamu zenu zote. Nitawapa moyo mpya na kuweka roho mpya ndani yenu, nitaondoa ndani yenu moyo wenu wa jiwe na kuwapa moyo wa nyama. Nami nitaweka Roho yangu ndani yenu na kuwafanya ninyi mfuate amri zangu na kuwafanya kuwa waangalifu kuzishika sheria zangu. Mtaishi katika nchi niliyowapa baba zenu, ninyi mtakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wenu. Nitawaokoa ninyi kutoka unajisi wenu wote. Nitaiita nafaka na kuiongeza iwe nyingi sana nami sitaleta njaa juu yenu. Nitaongeza matunda ya miti na mazao ya mashamba, ili kwamba msipate tena aibu miongoni mwa mataifa kwa ajili ya njaa. Ndipo mtakapozikumbuka njia zenu za uovu na matendo yenu maovu, nanyi mtajichukia wenyewe kwa ajili ya dhambi zote na matendo yenu ya kuchukiza. Ninataka ninyi mjue kwamba sifanyi hili kwa ajili yenu, asema BWANA Mwenyezi. Oneni aibu na mkatahayari kwa ajili ya mwenendo wenu, ee nyumba ya Israeli! “ ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Siku ile nitakapowasafisha kutoka dhambi zenu zote, nitarudisha watu waishi katika miji yenu na magofu yatajengwa upya. Nchi iliyokuwa ukiwa italimwa badala ya kukaa ukiwa machoni mwa wale wote wanaopita ndani yake. Watasema, “Hii nchi iliyokuwa imeachwa ukiwa sasa imekuwa kama bustani ya Edeni, miji ile iliyokuwa magofu, ukiwa na kuangamizwa, sasa imejengewa ngome na kukaliwa na watu.” Ndipo mataifa yanayowazunguka yaliyobakia watakapojua kuwa Mimi BWANA nimejenga tena kile kilichoharibiwa na nimepanda tena kile kilichokuwa ukiwa. Mimi BWANA nimenena, nami nitalifanya.’ “Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Mara nyingine tena nitasikia maombi ya nyumba ya Israeli na kuwatendea jambo hili: Nitawafanya watu wake kuwa wengi kama kondoo, kuwa wengi kama kundi la kondoo kwa ajili ya dhabihu huko Yerusalemu wakati wa sikukuu zao za wakati ulioamriwa. Hivyo ndivyo miji iliyokuwa magofu itajazwa na makundi ya watu. Ndipo watakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA.”

Ezekieli 36:16-38 Biblia Habari Njema (BHN)

Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Waisraeli walipoishi katika nchi yao waliitia unajisi kwa mienendo na matendo yao. Niliyaona matendo yao kuwa sawa na mwanamke aliye najisi wakati wa siku zake. Niliwamwagia ghadhabu yangu kwa sababu ya damu waliyomwaga katika nchi na kwa sababu ya miungu ambayo kwayo nchi ilitiwa unajisi. Niliwatawanya kati ya mataifa, wakasambazwa katika nchi nyingine. Niliwaadhibu kadiri ya tabia yao na matendo yao. Hata walipokuwa miongoni mwa mataifa walilikufuru jina langu takatifu, hata watu wakasema hivi juu yao: ‘Tazama! Hawa ndio wale watu wa Mwenyezi-Mungu, lakini wamelazimika kuondoka katika nchi yake!’ Hiyo ilinifanya kuhangaika juu ya jina langu takatifu ambalo watu wa Israeli walilikufuru miongoni mwa mataifa walikokwenda. Basi, waambie Waisraeli kwamba mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ninachotaka kufanya si kwa faida yenu nyinyi watu wa Israeli, bali ni kwa heshima ya jina langu takatifu mlilolikufuru miongoni mwa mataifa mlikokwenda. Nitalirudishia hadhi yake takatifu jina langu kuu mlilokufuru miongoni mwa mataifa. Hapo ndipo mataifa yatakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Nitawatumia nyinyi kuonesha utakatifu wangu mbele yao. Nitawaondoa nyinyi katika kila taifa na kuwakusanya kutoka nchi zote za kigeni; nitawarudisha katika nchi yenu wenyewe. Nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtatakata uchafu wenu wote na sanamu za miungu yenu yote. Nitawapeni moyo mpya na kuweka roho mpya ndani yenu. Nitauondoa kwenu moyo mgumu kama jiwe na kuwapa moyo wa utii. Nitatia roho yangu ndani yenu; nitawafanya mfuate kanuni zangu na kuzingatia maazimio yangu. Mtakaa katika nchi niliyowapa wazee wenu. Mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu. Nitawaokoa kutoka uchafu wenu wote. Nitaiamuru ngano iongezeke, wala sitawaletea njaa tena. Nitayazidisha matunda ya miti na mazao ya mashamba ili msiaibike tena kwa njaa kati ya mataifa. Kisha mtakapokumbuka mienendo yenu miovu na matendo yenu mabaya, mtajichukia wenyewe kwa sababu ya maovu yenu na machukizo mliyofanya. Lakini jueni kwamba sitafanya hivyo kwa ajili yenu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Oneni aibu na kufadhaika kwa sababu ya matendo yenu, enyi Waisraeli! “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Siku ile nitakapowasafisheni maovu yenu yote, nitaifanya miji yenu ikaliwe, nayo magofu yajengwe upya. Nchi iliyokuwa jangwa italimwa tena, hata atakayepita huko hataiona kuwa jangwa. Nao watu watasema: ‘Nchi hii iliyokuwa jangwa, sasa imekuwa kama bustani ya Edeni, nayo miji iliyokuwa ukiwa, mahame na magofu, sasa inakaliwa na watu, tena ina ngome!’ Hapo mataifa yaliyobaki kandokando yenu, yatatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu niliyejenga upya yaliyoharibiwa na kupanda mbegu katika nchi iliyokuwa jangwa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema, na nitafanya hayo. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Waisraeli wataniomba niwafanye kuwa wengi kama kundi la kondoo, nami nitawafanya hivyo. Wataniomba wawe wengi kama kundi la kondoo wa tambiko, naam, kama kundi la kondoo mjini Yerusalemu wakati wa sikukuu zake. Hivyo ndivyo miji yenu iliyokuwa ukiwa itakavyojaa makundi ya watu. Hapo ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”

Ezekieli 36:16-38 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Tena, neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, nyumba ya Israeli walipokaa katika nchi yao wenyewe, waliitia uchafu kwa njia yao na kwa matendo yao. Njia yao mbele zangu ilikuwa kama uchafu wa mwanamke wakati wa kutengwa kwake. Kwa hiyo nilimwaga hasira yangu juu yao, kwa ajili ya damu waliyoimwaga juu ya nchi, na kwa sababu wameitia uchafu kwa vinyago vyao. Nikawatawanya katika mataifa, wakatapanyika katika nchi nyingi; kwa kadiri ya njia yao, na kwa kadiri ya matendo yao, niliwahukumu. Nao walipoyafikia mataifa yale waliyoyaendea, walilitia unajisi jina langu takatifu; kwa kuwa watu waliwanena, wakisema, Watu hawa ni watu wa BWANA, nao wametoka katika nchi yake. Lakini, niliwahurumia kwa ajili ya jina langu takatifu, ambalo nyumba ya Israeli walikuwa wamelitia unajisi katika mataifa walikoenda. Kwa hiyo; waambieni nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi, sitendi hili kwa ajili yenu, Ee nyumba ya Israeli, bali kwa ajili ya jina langu takatifu, mlilolitia unajisi katika mataifa mlikoenda. Nami nitalitakasa jina langu kuu, lililotiwa unajisi katika mataifa, mlilolitia unajisi kati yao; nao mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, asema Bwana MUNGU, nitakapotakaswa kati yenu mbele ya macho yao. Maana nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote, na kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe. Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni kutoka kwa uchafu wenu wote, na kutoka kwa vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda. Nanyi mtakaa katika nchi ile niliyowapa baba zenu, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu. Nami nitawaokoeni kutoka kwa uchafu wenu wote; nitaiamuru ngano iongezeke, wala sitawaletea njaa tena. Nami nitazidisha matunda ya miti, na mazao ya mashamba, msipate tena kutukanwa na mataifa kwa sababu ya njaa. Ndipo mtazikumbuka njia zenu mbaya, na matendo yenu yasiyokuwa mema, nanyi mtajichukia nafsi zenu kwa macho yenu, kwa sababu ya maovu yenu na machukizo yenu. Ijulikane kwenu ya kuwa silitendi neno hili kwa ajili yenu, asema Bwana MUNGU; tahayarikeni, na kufadhaika, kwa sababu ya njia zenu, Enyi nyumba ya Israeli. Bwana MUNGU asema hivi; Siku ile nitakapowatakaseni kutoka kwa maovu yenu yote, nitaifanya miji ikaliwe na watu, na palipobomolewa pajengwe tena. Nchi iliyokuwa ukiwa italimwa, ijapokuwa ilikuwa ukiwa mbele ya macho ya watu wote waliopita. Nao watasema, Nchi hii, iliyokuwa ukiwa, imekuwa kama bustani ya Adeni; nayo miji iliyokuwa mahame, na ukiwa, na magofu, sasa ina maboma, inakaliwa na watu. Ndipo mataifa, waliobaki karibu yenu pande zote, watajua ya kuwa mimi, BWANA, nimejenga mahali palipoharibika, nami nimepanda mbegu katika nchi iliyokuwa ukiwa; mimi, BWANA, nimesema hayo; tena nitayatenda. Bwana MUNGU asema hivi, Tena kwa ajili ya jambo hili nitaulizwa na nyumba ya Israeli, ili niwatendee; nami nitawaongeza kwa watu kama kundi la kondoo. Kama kundi lililo tayari kutolewa sadaka, kama kundi la Yerusalemu katika sikukuu zake zilizoamriwa; ndivyo itakavyojazwa watu, miji ile iliyokuwa maganjo; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.

Ezekieli 36:16-38 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Tena, neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, nyumba ya Israeli walipokaa katika nchi yao wenyewe, waliitia uchafu kwa njia yao na kwa matendo yao. Njia yao mbele zangu ilikuwa kama uchafu wa mwanamke wakati wa kutengwa kwake. Kwa hiyo nalimwaga hasira yangu juu yao, kwa ajili ya damu waliyoimwaga juu ya nchi, na kwa sababu wameitia uchafu kwa vinyago vyao. Nikawatawanya katika mataifa, wakatapanyika katika nchi nyingi; kwa kadiri ya njia yao, na kwa kadiri ya matendo yao, naliwahukumu. Nao walipoyafikilia mataifa yale waliyoyaendea, walilitia unajisi jina langu takatifu; kwa kuwa watu waliwanena, wakisema, Watu hawa ni watu wa BWANA, nao wametoka katika nchi yake. Lakini, naliwahurumia kwa ajili ya jina langu takatifu, ambalo nyumba ya Israeli walikuwa wamelitia unajisi katika mataifa waliyoyaendea. Kwa hiyo; waambieni nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi Sitendi hili kwa ajili yenu, Ee nyumba ya Israeli, bali kwa ajili ya jina langu takatifu, mlilolitia unajisi katika mataifa mliyoyaendea. Nami nitalitakasa jina langu kuu, lililotiwa unajisi katika mataifa, mlilolitia unajisi kati yao; nao mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, asema Bwana MUNGU, nitakapotakaswa kati yenu mbele ya macho yao. Maana nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote, na kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe. Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda. Nanyi mtakaa katika nchi ile niliyowapa baba zenu, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu. Nami nitawaokoeni na uchafu wenu wote; nitaiita ngano, na kuiongeza, wala sitaweka njaa juu yenu tena. Nami nitazidisha matunda ya miti, na mazao ya mashamba, msipate tena kutukanwa na mataifa kwa sababu ya njaa. Ndipo mtazikumbuka njia zenu mbaya, na matendo yenu yasiyokuwa mema, nanyi mtajichukia nafsi zenu kwa macho yenu, kwa sababu ya maovu yenu na machukizo yenu. Ijulikane kwenu ya kuwa silitendi neno hili kwa ajili yenu, asema Bwana MUNGU; tahayarikeni, na kufadhaika, kwa sababu ya njia zenu, Enyi nyumba ya Israeli. Bwana MUNGU asema hivi; Siku ile nitakapowatakaseni na maovu yenu yote, nitaifanya miji ikaliwe na watu, na palipobomolewa pajengwe tena. Nchi iliyokuwa ukiwa italimwa, ijapokuwa ilikuwa ukiwa mbele ya macho ya watu wote waliopita. Nao watasema, Nchi hii, iliyokuwa ukiwa, imekuwa kama bustani ya Adeni; nayo miji iliyokuwa mahame, na ukiwa, na magofu, sasa ina maboma, inakaliwa na watu. Ndipo mataifa, waliobaki karibu yenu pande zote, watajua ya kuwa mimi, BWANA, nimejenga mahali palipoharibika, nami nimepanda mbegu katika nchi iliyokuwa ukiwa; mimi, BWANA, nimesema hayo; tena nitayatenda. Bwana MUNGU asema hivi, Tena kwa ajili ya jambo hili nitaulizwa na nyumba ya Israeli, ili niwatendee; nami nitawaongeza kwa watu kama kundi la kondoo. Kama kundi lililo tayari kutolewa sadaka, kama kundi la Yerusalemu katika sikukuu zake zilizoamriwa; ndivyo itakavyojazwa watu, miji ile iliyokuwa maganjo; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha