Ezekieli 28:11-26
Ezekieli 28:11-26 NENO
Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: “Mwanadamu, mfanyie maombolezo mfalme wa Tiro, nawe umwambie: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “ ‘Ulikuwa kipeo cha ukamilifu, ukiwa umejaa hekima na mkamilifu katika uzuri. Ulikuwa ndani ya Edeni, bustani ya Mungu; kila kito cha thamani kilikupamba: akiki nyekundu, yakuti manjano na zumaridi, krisolitho, shohamu na yaspi, yakuti samawi, almasi na zabarajadi. Kuwekwa kwa hayo mapambo na kushikizwa kwake kulifanywa kwa dhahabu; siku ile ulipoumbwa yaliandaliwa tayari. Ulipakwa mafuta kuwa kerubi mlinzi, kwa kuwa hivyo ndivyo nilivyokuweka wakfu. Ulikuwa kwenye mlima mtakatifu wa Mungu; ulitembea katikati ya vito vya moto. Ulikuwa mnyofu katika njia zako tangu siku ile ya kuumbwa kwako, hadi uovu ulipoonekana ndani yako. Kutokana na biashara yako iliyoenea, ulijazwa na dhuluma, nawe ukatenda dhambi. Hivyo nilikuondoa kwa aibu kutoka mlima wa Mungu, nami nikakufukuza, ee kerubi mlinzi, kutoka katikati ya vito vya moto. Moyo wako ukawa na kiburi kwa ajili ya uzuri wako, nawe ukaiharibu hekima yako kwa sababu ya fahari yako. Kwa hiyo nikakutupa chini; nimekufanya kioja mbele ya wafalme. Kwa dhambi zako nyingi na biashara yako ya dhuluma, umenajisi mahali pako patakatifu. Kwa hiyo nilifanya moto utoke ndani yako, nao ukakuteketeza, nami nikakufanya majivu juu ya nchi, machoni pa wote waliokuwa wakitazama. Mataifa yote yaliyokujua yanakustaajabia; umefikia mwisho wa kutisha na hutakuwepo tena milele.’ ” Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: “Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Sidoni, ukatabiri dhidi yake, nawe useme: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “ ‘Mimi ni kinyume chako, ee Sidoni, nami nitapata utukufu ndani yako. Nao watajua kwamba Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nitakapotekeleza hukumu zangu na kuonesha utakatifu wangu ndani yake. Nitapeleka tauni ndani yake na kufanya damu itiririke katika barabara zake. Waliochinjwa wataanguka ndani yake, kwa upanga dhidi yake kila upande. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu. “ ‘Nyumba ya Israeli hawatakuwa tena na majirani wenye nia ya kuwadhuru, wanaoumiza kama michongoma na miiba mikali. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Bwana Mungu Mwenyezi. “ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitakapoikusanya nyumba ya Israeli kutoka mataifa ambako wametawanyika, nitajionesha kuwa mtakatifu miongoni mwao machoni pa mataifa. Ndipo watakapoishi katika nchi yao wenyewe, niliyompa mtumishi wangu Yakobo. Wataishi humo kwa salama na watajenga nyumba na kupanda mashamba ya mizabibu, wataishi kwa salama nitakapowaadhibu majirani zao wote ambao waliwafanyia uovu. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wao.’ ”