Ezekieli 22
22
Dhambi za Yerusalemu
1Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
2“Mwanadamu, je, wewe utauhukumu? Je, utauhukumu huu mji unaomwaga damu? Basi uujulishe kuhusu matendo yake yote ya machukizo 3uuambie: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ee mji unaojiletea maangamizi wenyewe kwa kumwaga damu ndani yake na kujinajisi wenyewe kwa kutengeneza sanamu, 4umekuwa na hatia kwa sababu ya damu uliyomwaga, na umetiwa unajisi kwa sanamu ulizotengeneza. Umejiletea mwisho wa siku zako na mwisho wa miaka yako umewadia. Kwa hiyo nitakufanya kitu cha kudharauliwa kwa mataifa na kitu cha mzaha kwa nchi zote. 5Wale walio karibu na wale walio mbali watakudhihaki, ewe mji wenye sifa mbaya, uliyejaa ghasia.
6“ ‘Tazama jinsi kila mkuu wa Israeli aliye ndani yako anavyotumia nguvu zake kumwaga damu. 7Ndani yako wamewadharau baba na mama; ndani yako wamewatendea wageni udhalimu, na kuwadhulumu yatima na wajane. 8Mmedharau vitu vyangu vitakatifu na kuzinajisi Sabato zangu. 9Ndani yako wako watu wasingiziaji, watu walio tayari kumwaga damu, ndani yako wako wale wanaokula vyakula vilivyotolewa mahali pa ibada za sanamu kwenye milima, na kutenda matendo ya uasherati. 10Ndani yako wako wale wanaovunjia heshima vitanda vya baba zao, ndani yako wamo wale wanaowatendea wanawake jeuri wakiwa katika hedhi, wakati wakiwa najisi. 11Ndani yako mtu hufanya mambo ya machukizo na mke wa jirani yake, mwingine kwa aibu kubwa hukutana kimwili na mke wa mwanawe, mwingine humtenda jeuri dada yake, binti ya baba yake hasa. 12Ndani yako watu hupokea rushwa ili kumwaga damu, mnapokea riba na faida ya ziada na kupata faida isiyokuwa halali kutoka kwa majirani ili kupata faida kubwa kupita kiasi. Nawe umenisahau mimi, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
13“ ‘Hakika nitapiga makofi kwa ajili ya faida isiyo halali uliyojipatia na kwa damu uliyoimwaga ndani yako. 14Je, ujasiri wako utadumu au mikono yako itakuwa na nguvu siku hiyo nitakapokuadhibu? Mimi Mwenyezi Mungu nimesema na nitalifanya. 15Nitakutawanya miongoni mwa mataifa na kukutapanya katika nchi mbalimbali nami nitakomesha unajisi wako. 16Baada ya kunajisika mbele ya mataifa, utajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”
17Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 18“Mwanadamu, nyumba ya Israeli imekuwa takataka ya chuma kwangu; wote wamekuwa shaba, bati, chuma na risasi iliyoachwa kalibuni. Wao ni taka ya madini ya fedha tu. 19Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: ‘Kwa kuwa wote mmekuwa takataka ya chuma, nitawakusanya Yerusalemu. 20Kama vile watu wakusanyavyo fedha, shaba, chuma, risasi na bati kalibuni ili kuyeyusha kwa moto mkali, ndivyo nitakavyowakusanya katika hasira yangu na ghadhabu yangu kuwaweka ndani ya mji na kuwayeyusha. 21Nitawakusanya na kupuliza juu yenu moto wa hasira yangu na ghadhabu yangu nanyi mtayeyushwa ndani ya huo mji. 22Kama fedha iyeyukavyo kalibuni, ndivyo mtakavyoyeyuka ndani ya huo mji, nanyi mtajua kuwa Mimi, Mwenyezi Mungu, nimemwaga ghadhabu yangu juu yenu.’ ”
23Neno la Mwenyezi Mungu likanijia tena kusema: 24“Mwanadamu, iambie nchi, ‘Wewe ni nchi ambayo haijatakaswa wala kunyeshewa katika siku ya ghadhabu.’ 25Kuna hila mbaya ya wakuu ndani yake kama simba angurumaye akirarua mawindo yake, wanakula watu, wanachukua hazina na vitu vya thamani na kuongeza idadi ya wajane ndani yake. 26Makuhani wake wameihalifu sheria yangu na kunajisi vitu vyangu vitakatifu, hawatofautishi kati ya vitu vitakatifu na vitu vya kawaida. Wanafundisha kuwa hakuna tofauti kati ya vitu vilivyo najisi na visivyo najisi, nao wanafumba macho yao katika kutunza Sabato zangu, hivyo katikati yao nimetiwa unajisi. 27Maafisa wake walio ndani yake ni kama mbwa-mwitu wararuao mawindo yao, wanamwaga damu na kuua watu ili kupata faida ya udhalimu. 28Manabii wake wanapaka chokaa matendo haya kwa maono ya uongo na utabiri wa udanganyifu. Wanasema, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi,’ wakati Mwenyezi Mungu hajasema. 29Watu wa nchi wanatoza kwa nguvu na kufanya unyang’anyi, wanawadhulumu maskini na wahitaji, na kuwaonea wageni, wakiwanyima haki.
30“Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, ambaye angejenga ukuta na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka kwa ajili ya watu wa nchi ili nisije nikaiangamiza, lakini sikumwona mtu yeyote. 31Hivyo nitaimwaga ghadhabu yangu juu yao na kuwateketeza kwa moto wa hasira yangu, nikiyaleta juu ya vichwa vyao yale yote waliyotenda, asema Bwana Mungu Mwenyezi.”
Iliyochaguliwa sasa
Ezekieli 22: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.