Kutoka 9
9
Pigo la tano: Vifo vya mifugo
1Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nenda kwa Farao ukamwambie, ‘Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Waebrania, asemalo: “Waachie watu wangu waende ili wapate kuniabudu.” 2Usipowaachia waende, nawe ukiendelea kuwashikilia, 3mkono wa Mwenyezi Mungu utaleta pigo baya kwa mifugo yako, juu ya farasi wako, punda, ngamia, ng’ombe wako, kondoo na mbuzi. 4Lakini Mwenyezi Mungu ataweka tofauti kati ya mifugo ya Israeli na ile ya Misri, kwamba hakuna mnyama wa Mwisraeli atakayekufa.’ ”
5Mwenyezi Mungu akaweka wakati na kusema, “Kesho Mwenyezi Mungu atalitenda hili katika nchi.” 6Siku iliyofuata Mwenyezi Mungu akalitenda: Mifugo yote ya Wamisri ikafa, lakini hakuna hata mnyama mmoja wa Waisraeli aliyekufa. 7Farao akatuma watu kuchunguza, nao wakakuta kuwa hakuna hata mnyama mmoja wa Waisraeli aliyekufa. Lakini moyo wa Farao haukukubali kuwaachia watu waende.
Pigo la sita: Majipu
8Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa na Haruni, “Chukueni majivu ya tanuru, naye Musa ayarushe angani mbele ya Farao. 9Yatakuwa vumbi jepesi juu ya nchi yote ya Misri, pia yatatokea majipu yenye kufura kwenye miili ya watu na ya wanyama katika nchi yote.”
10Basi wakachukua majivu kwenye tanuru na kusimama mbele ya Farao. Musa akayarusha hewani, nayo majipu yenye kufura yakatokea kwenye miili ya watu na ya wanyama. 11Waganga hawakuweza kusimama mbele ya Musa kwa sababu ya majipu yaliyokuwa kwenye miili yao, na kwenye miili ya Wamisri wote. 12Lakini Mwenyezi Mungu akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, naye hakuwasikiliza Musa na Haruni, kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amemwambia Musa.
Pigo la saba: Mvua ya mawe
13Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Amka asubuhi na mapema, usimame mbele ya Farao, umwambie, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Waebrania: Waachie watu wangu waende, ili waweze kuniabudu, 14au wakati huu nitaleta mapigo yangu yenye nguvu dhidi yako, maafisa wako na watu wako, ili upate kujua kuwa hakuna mwingine kama mimi duniani kote. 15Kwa kuwa hadi sasa ningekuwa nimenyoosha mkono wangu na kukupiga wewe na watu wako kwa pigo ambalo lingekufutilia mbali juu ya nchi. 16Lakini nimekuinua wewe kwa kusudi hili hasa, ili nikuoneshe uwezo wangu, na jina langu litangazwe duniani kote. 17Bado unaendelea kujiinua dhidi ya watu wangu, wala hutaki kuwaachia waende. 18Hivyo basi, kesho wakati kama huu nitaleta mvua mbaya sana ya mawe ambayo haijapata kunyesha katika nchi ya Misri, tangu siku ilipoumbwa hadi leo. 19Sasa toa amri mifugo yako na kila kitu ulicho nacho shambani, kipelekwe mahali pa usalama. Kwa sababu mvua ya mawe itamwangukia kila mtu na mnyama ambaye hajaletwa ndani, na ambaye bado yuko nje shambani; nao watakufa.’ ”
20Wale maafisa wa Farao ambao waliliogopa neno la Mwenyezi Mungu wakafanya haraka kuwaleta watumwa wao na mifugo yao ndani. 21Lakini wale waliopuuza neno la Mwenyezi Mungu wakawaacha watumwa wao na mifugo yao shambani.
22Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nyoosha mkono wako kuelekea angani ili mvua ya mawe inyeshe Misri yote: juu ya watu, wanyama, na juu ya kila kitu kinachoota katika mashamba ya Misri.” 23Musa alipoinyoosha fimbo yake kuelekea angani, Mwenyezi Mungu akatuma ngurumo na mvua ya mawe; mwanga wa radi ukamulika hadi nchi. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akanyesha mvua ya mawe juu ya nchi ya Misri; 24mvua ya mawe ikanyesha, na radi ikamulika pote. Ikawa dhoruba ya kutisha zaidi, ambayo haijawahi kutokea katika Misri tangu nchi hiyo iwe taifa. 25Mvua ya mawe ikaharibu kila kitu katika nchi ya Misri kilichokuwa katika mashamba: watu na wanyama; ikaharibu kila kitu kilichoota mashambani na kung’oa kila mti. 26Mahali pekee ambapo mvua ya mawe haikunyesha ni nchi ya Gosheni, ambako Waisraeli waliishi.
27Ndipo Farao akawaita Musa na Haruni akawaambia, “Wakati huu nimetenda dhambi. Mwenyezi Mungu ni mwenye haki, mimi na watu wangu ni wakosaji. 28Mwombeni Mwenyezi Mungu, kwa kuwa tumepata ngurumo na mvua za mawe za kutosha. Nitawaachia mwondoke; hamtahitaji kungoja zaidi.”
29Musa akamjibu, “Nitakapokuwa nimetoka nje ya mji, nitanyoosha mikono yangu juu kumwomba Mwenyezi Mungu. Ngurumo zitakoma na hapatakuwa mvua ya mawe tena, ili upate kujua kuwa nchi ni mali ya Mwenyezi Mungu. 30Lakini ninajua kuwa wewe na maafisa wako bado hammwogopi Bwana Mwenyezi Mungu.”
31(Kitani na shayiri viliharibiwa, kwa kuwa shayiri ilikuwa na masuke, na kitani ilikuwa imechanua maua. 32Hata hivyo, ngano na kusemethi hazikuharibiwa kwa sababu zilikuwa hazijakomaa.)
33Kisha Musa akaondoka kwa Farao, akaenda nje ya mji. Musa akanyoosha mikono yake kuelekea kwa Mwenyezi Mungu, ngurumo na mvua ya mawe vikakoma, mvua haikuendelea tena kunyesha nchini. 34Farao alipoona kwamba mvua ya mawe na ngurumo zimekoma, akafanya dhambi tena. Yeye na maafisa wake wakafanya mioyo yao kuwa migumu. 35Kwa hiyo, moyo wa Farao ukawa mgumu, wala hakuwaachia Waisraeli waende, kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amesema kupitia Musa.
Iliyochaguliwa sasa
Kutoka 9: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.