Kutoka 8
8
1Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nenda kwa Farao ukamwambie, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu. 2Ukikataa kuwaruhusu kuondoka, basi nitaipiga nchi yako yote kwa kuwaletea vyura. 3Mto Naili utafurika vyura. Watakuja kwenye jumba lako la kifalme na katika chumba chako cha kulala na kitandani mwako, katika nyumba za maafisa wako na kwa watu wako, vyura hao wataingia katika meko yenu na kwenye vyombo vya kukandia unga. 4Vyura watapanda juu yako, juu ya watu wako na maafisa wako wote.’ ”
5Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Mwambie Haruni, ‘Nyoosha mkono wako ukiwa na ile fimbo yako juu ya vijito, mifereji na madimbwi, fanya vyura waje juu ya nchi ya Misri.’ ”
6Ndipo Haruni akaunyoosha mkono wake juu ya maji ya Misri, nao vyura wakatokea na kuifunika nchi. 7Lakini waganga wakafanya vivyo hivyo kwa siri ya uganga wao, nao pia wakafanya vyura kuja juu ya nchi ya Misri.
8Ndipo Farao akamwita Musa na Haruni na kusema, “Mwombeni Mwenyezi Mungu awaondoe vyura kutoka kwangu na kwa watu wangu, nami nitawaachia watu wenu waende kumtolea Mwenyezi Mungu dhabihu.”
9Musa akamwambia Farao, “Ninakupa heshima ya kuamua ni wakati gani wa kukuombea wewe, maafisa wako, na watu wako ili vyura watoke kwenu na kwenye nyumba zenu, isipokuwa wale walio katika Mto Naili.”
10Farao akasema, “Kesho.”
Musa akamjibu, “Itakuwa kama unavyosema, ili upate kujua kwamba hakuna yeyote kama Mwenyezi Mungu, Mungu wetu. 11Vyura wataondoka kwako na katika nyumba zako, kwa maafisa wako na kwa watu wako, ila watabakia katika Mto Naili tu.”
12Baada ya Musa na Haruni kuondoka kwa Farao, Musa akamlilia Mwenyezi Mungu kuhusu vyura aliokuwa amewaleta kwa Farao. 13Naye Mwenyezi Mungu akafanya lile Musa alilomwomba. Vyura wakafia ndani ya nyumba, viwanjani na mashambani. 14Wakayakusanya malundo, nchi nzima ikanuka. 15Lakini Farao alipoona pametokea nafuu, akaushupaza moyo wake na hakuwasikiliza Musa na Haruni, kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amesema.
Pigo la tatu: Viroboto
16Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Mwambie Haruni, ‘Nyoosha fimbo yako uyapige mavumbi ya ardhi,’ nayo nchi yote ya Misri mavumbi yatakuwa viroboto.” 17Wakafanya hivyo, Haruni aliponyoosha mkono wake wenye fimbo na kuyapiga mavumbi ya nchi, viroboto wakawajia watu na wanyama. Mavumbi yote katika nchi ya Misri yakawa viroboto. 18Lakini waganga walipojaribu kutengeneza viroboto kwa siri ya uganga wao, hawakuweza. Nao viroboto walikuwa juu ya watu na wanyama.
19Waganga wale wakamwambia Farao, “Hiki ni kidole cha Mungu.” Lakini moyo wa Farao ukawa mgumu naye hakuwasikiliza, kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amesema.
Pigo la nne: Mainzi
20Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Amka asubuhi na mapema, usimame mbele ya Farao wakati anapoenda mtoni, umwambie, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu. 21Usipowaruhusu watu wangu waondoke, nitatuma makundi ya inzi juu yako na maafisa wako, juu ya watu wako, na ndani ya nyumba zenu. Nyumba za Wamisri zitajaa inzi; hata ardhi itafunikwa na inzi.
22“ ‘Lakini siku ile nitafanya kitu tofauti katika nchi ya Gosheni, ambapo watu wangu wanaishi, hapatakuwa na makundi ya inzi, ili mpate kujua kwamba Mimi, Mwenyezi Mungu, niko katika nchi hii. 23Nitaweka tofauti kati ya watu wangu na watu wenu. Ishara hii ya ajabu itatokea kesho.’ ”
24Naye Mwenyezi Mungu akafanya hivyo. Makundi makubwa ya inzi walimiminika katika jumba la kifalme la Farao na katika nyumba za maafisa wake, pia nchi yote ya Misri ikaharibiwa na inzi.
25Ndipo Farao akamwita Musa na Haruni na kuwaambia, “Nendeni mkamtolee Mungu wenu dhabihu katika nchi hii.”
26Lakini Musa akamwambia, “Hilo halitakuwa sawa. Dhabihu tutakazomtolea Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, zitakuwa chukizo kwa Wamisri. Tukitoa dhabihu ambazo ni chukizo mbele yao, je, hawatatupiga mawe? 27Ni lazima twende mwendo wa siku tatu hadi tufike jangwani ili tumtolee Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, dhabihu, kama alivyotuagiza.”
28Farao akamwambia, “Nitawaruhusu mwende kumtolea Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, dhabihu huko jangwani, lakini hamna ruhusa kwenda mbali sana. Sasa mniombee.”
29Musa akajibu, “Mara tu nitakapoondoka, nitamwomba Mwenyezi Mungu na kesho inzi wataondoka kwa Farao, kwa maafisa wake, na kwa watu wake. Ila hakikisha kwamba Farao hatatenda kwa udanganyifu tena kwa kutokuwaachia watu waende kumtolea Mwenyezi Mungu dhabihu.”
30Ndipo Musa akamwacha Farao na kumwomba Mwenyezi Mungu, 31naye Mwenyezi Mungu akafanya lile Musa alilomwomba. Inzi wakaondoka kwa Farao, kwa maafisa wake na kwa watu wake, wala hakuna hata inzi aliyebakia. 32Lakini wakati huu pia Farao akaufanya moyo wake kuwa mgumu, wala hakuwaruhusu Waisraeli waondoke.
Iliyochaguliwa sasa
Kutoka 8: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.