Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 8:1-15

Kutoka 8:1-15 NENO

Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nenda kwa Farao ukamwambie, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu. Ukikataa kuwaruhusu kuondoka, basi nitaipiga nchi yako yote kwa kuwaletea vyura. Mto Naili utafurika vyura. Watakuja kwenye jumba lako la kifalme na katika chumba chako cha kulala na kitandani mwako, katika nyumba za maafisa wako na kwa watu wako, vyura hao wataingia katika meko yenu na kwenye vyombo vya kukandia unga. Vyura watapanda juu yako, juu ya watu wako na maafisa wako wote.’ ” Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Mwambie Haruni, ‘Nyoosha mkono wako ukiwa na ile fimbo yako juu ya vijito, mifereji na madimbwi, fanya vyura waje juu ya nchi ya Misri.’ ” Ndipo Haruni akaunyoosha mkono wake juu ya maji ya Misri, nao vyura wakatokea na kuifunika nchi. Lakini waganga wakafanya vivyo hivyo kwa siri ya uganga wao, nao pia wakafanya vyura kuja juu ya nchi ya Misri. Ndipo Farao akamwita Musa na Haruni na kusema, “Mwombeni Mwenyezi Mungu awaondoe vyura kutoka kwangu na kwa watu wangu, nami nitawaachia watu wenu waende kumtolea Mwenyezi Mungu dhabihu.” Musa akamwambia Farao, “Ninakupa heshima ya kuamua ni wakati gani wa kukuombea wewe, maafisa wako, na watu wako ili vyura watoke kwenu na kwenye nyumba zenu, isipokuwa wale walio katika Mto Naili.” Farao akasema, “Kesho.” Musa akamjibu, “Itakuwa kama unavyosema, ili upate kujua kwamba hakuna yeyote kama Mwenyezi Mungu, Mungu wetu. Vyura wataondoka kwako na katika nyumba zako, kwa maafisa wako na kwa watu wako, ila watabakia katika Mto Naili tu.” Baada ya Musa na Haruni kuondoka kwa Farao, Musa akamlilia Mwenyezi Mungu kuhusu vyura aliokuwa amewaleta kwa Farao. Naye Mwenyezi Mungu akafanya lile Musa alilomwomba. Vyura wakafia ndani ya nyumba, viwanjani na mashambani. Wakayakusanya malundo, nchi nzima ikanuka. Lakini Farao alipoona pametokea nafuu, akaushupaza moyo wake na hakuwasikiliza Musa na Haruni, kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amesema.

Video ya Kutoka 8:1-15