Kutoka 7:1-13
Kutoka 7:1-13 NEN
Kisha BWANA akamwambia Mose, “Tazama, nimekufanya kuwa kama Mungu kwa Farao, naye Aroni, huyo ndugu yako, atakuwa nabii wako. Utasema kila kitu nitakachokuagiza, naye Aroni ndugu yako atamwambia Farao awaachie Waisraeli watoke katika nchi yake. Lakini nitaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu. Ingawa nitazidisha ishara na maajabu katika Misri, hatawasikiliza. Kisha nitaupeleka mkono wangu juu ya Misri, na kwa matendo makuu ya hukumu nitavitoa vikundi vyangu, watu wangu Waisraeli. Nao Wamisri watajua kuwa Mimi ndimi BWANA nitakapounyoosha mkono wangu dhidi ya Misri na kuwatoa Waisraeli watoke humo.” Mose na Aroni wakafanya sawasawa kama vile BWANA alivyowaagiza. Mose alikuwa na umri wa miaka themanini na Aroni alikuwa na umri wa miaka themanini na mitatu walipozungumza na Farao. BWANA akamwambia Mose na Aroni, “Farao atakapowaambia, ‘Fanyeni muujiza,’ basi mwambie Aroni, ‘Chukua fimbo yako na uitupe chini mbele ya Farao,’ nayo fimbo itakuwa nyoka.” Ndipo Mose na Aroni wakaenda kwa Farao wakafanya sawasawa kama vile BWANA alivyoagiza. Aroni akaitupa ile fimbo yake chini mbele ya Farao na maafisa wake, nayo ikawa nyoka. Farao naye akawaita watu wenye maarifa na wachawi na waganga wa Kimisri, nao wakafanya vivyo hivyo kwa siri ya uganga wao. Kila mmoja alitupa fimbo yake chini, nayo ikawa nyoka. Lakini fimbo ya Aroni ikazimeza zile fimbo zao. Hata hivyo moyo wa Farao ukawa mgumu, naye hakuwasikiliza Mose na Aroni, sawasawa kama vile BWANA alivyokuwa amesema.