Kutoka 7:1-13
Kutoka 7:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Tazama, mimi nakufanya kuwa kama mungu kwa Farao, naye ndugu yako Aroni atakuwa nabii wako. Utamwambia ndugu yako Aroni mambo yote nitakayokujulisha, naye Aroni nduguyo, atamwambia Farao awaache Waisraeli watoke nchini mwake. Lakini nitaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu. Na hata kama nitazidisha miujiza na maajabu yangu katika nchi ya Misri, Farao hatakusikiliza, na hapo nitaunyosha mkono wangu wenye nguvu na kuiadhibu vikali nchi ya Misri, na kuwatoa watu wangu, makabila ya Israeli, kutoka Misri. Nitafanya hivyo kwa matendo makuu ya hukumu dhidi ya Misri. Wakati nitakapounyosha mkono wangu dhidi ya nchi ya Misri na kuwatoa Waisraeli miongoni mwao. Ndipo Wamisri watakapotambua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.” Basi, Mose na Aroni wakafanya hivyo; naam, walifanya kama Mwenyezi-Mungu alivyowaamuru. Mose alikuwa na umri wa miaka themanini, na Aroni alikuwa na umri wa miaka themanini na mitatu wakati huo walipoongea na Farao. Mwenyezi-Mungu aliwaambia Mose na Aroni, “Farao atakapowaambieni mthibitishe jambo hilo kwa kutenda miujiza, wewe utamwambia Aroni aichukue fimbo yake, aitupe mbele ya Farao, nayo itakuwa nyoka.” Basi, Mose na Aroni wakamwendea Farao na kufanya kama walivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Aroni aliitupa fimbo yake chini mbele ya Farao na maofisa wake, nayo ikawa nyoka. Lakini, Farao akawaita wenye hekima wake na wachawi; hao wachawi wa Misri wakafanya vivyo hivyo kwa uchawi wao. Kila mmoja akaitupa fimbo yake chini, ikawa nyoka. Lakini fimbo ya Aroni ikazimeza fimbo zao. Hata hivyo, moyo wa Farao bado ulibaki kuwa mgumu, wala hakuwasikiliza; ikawa kama alivyosema Mwenyezi-Mungu.
Kutoka 7:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akamwambia Musa, Angalia, nimekufanya wewe kuwa kama Mungu kwa Farao; na huyo ndugu yako Haruni atakuwa nabii wako. Utanena hayo yote nikuagizayo; na ndugu yako Haruni atanena na Farao, ili awape wana wa Israeli ruhusa watoke nchi yake. Nami nitaufanya mgumu moyo wa Farao, nami nitazifanya kuwa nyingi ishara zangu na ajabu zangu katika nchi ya Misri. Lakini Farao hatawasikiza ninyi, nami nitaweka mkono wangu juu ya Misri, na kuyatoa majeshi yangu, watu wangu, hao wana wa Israeli, watoke nchi ya Misri kwa hukumu zilizo kuu. Na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, hapo nitakapounyosha mkono wangu juu ya Misri na kuwatoa wana wa Israeli watoke kati yao. Musa na Haruni wakafanya vivyo hivyo; kama BWANA alivyowaambia, ndivyo walivyofanya. Huyo Musa alikuwa ni mtu wa miaka themanini umri wake, na Haruni alikuwa ni mtu wa miaka themanini na mitatu, hapo waliponena na Farao. BWANA akanena na Musa na Haruni, akawaambia, Farao atakaponena nanyi, na kuwaambia, Jifanyieni miujiza; ndipo utakapomwambia Haruni, Shika fimbo yako, uibwage chini mbele ya Farao, ili iwe nyoka. Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, wakafanya vivyo hivyo kama BWANA alivyowaambia; Haruni akaibwaga fimbo yake chini mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake, ikawa nyoka. Ndipo Farao naye akawaita wajuzi na wachawi; na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo hivyo kwa uganga wao. Wakabwaga chini kila mtu fimbo yake, nazo zikawa nyoka; lakini fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zao. Moyo wa Farao ukawa ni mgumu asiwasikize; kama BWANA alivyonena.
Kutoka 7:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akamwambia Musa, Angalia, nimekufanya wewe kuwa kama Mungu kwa Farao; na huyo ndugu yako Haruni atakuwa nabii wako. Utanena hayo yote nikuagizayo; na ndugu yako Haruni atanena na Farao, ili awape wana wa Israeli ruhusa watoke nchi yake. Nami nitaufanya mgumu moyo wa Farao, nami nitazifanya kuwa nyingi ishara zangu na ajabu zangu katika nchi ya Misri. Lakini Farao hatawasikiza ninyi, nami nitaweka mkono wangu juu ya Misri, na kuyatoa majeshi yangu, watu wangu, hao wana wa Israeli, watoke nchi ya Misri kwa hukumu zilizo kuu. Na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, hapo nitakapounyosha mkono wangu juu ya Misri na kuwatoa wana wa Israeli watoke kati yao. Musa na Haruni wakafanya vivyo; kama BWANA alivyowaambia, ndivyo walivyofanya. Huyo Musa alikuwa ni mtu wa miaka themanini umri wake, na Haruni alikuwa ni mtu wa miaka themanini na mitatu, hapo waliponena na Farao. BWANA akanena na Musa na Haruni, akawaambia, Farao atakaponena nanyi, na kuwaambia, Jifanyieni miujiza; ndipo utakapomwambia Haruni, Shika fimbo yako, uibwage chini mbele ya Farao, ili iwe nyoka. Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, wakafanya vivyo kama BWANA alivyowaambia; Haruni akaibwaga fimbo yake chini mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake, ikawa nyoka. Ndipo Farao naye akawaita wenye akili na wachawi; na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo kwa uganga wao. Wakabwaga chini kila mtu fimbo yake, nazo zikawa nyoka; lakini fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zao. Moyo wa Farao ukawa ni mgumu asiwasikize; kama BWANA alivyonena.
Kutoka 7:1-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha BWANA akamwambia Mose, “Tazama, nimekufanya kuwa kama Mungu kwa Farao, naye Aroni, huyo ndugu yako, atakuwa nabii wako. Utasema kila kitu nitakachokuagiza, naye Aroni ndugu yako atamwambia Farao awaachie Waisraeli watoke katika nchi yake. Lakini nitaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu. Ingawa nitazidisha ishara na maajabu katika Misri, hatawasikiliza. Kisha nitaupeleka mkono wangu juu ya Misri, na kwa matendo makuu ya hukumu nitavitoa vikundi vyangu, watu wangu Waisraeli. Nao Wamisri watajua kuwa Mimi ndimi BWANA nitakapounyoosha mkono wangu dhidi ya Misri na kuwatoa Waisraeli watoke humo.” Mose na Aroni wakafanya sawasawa kama vile BWANA alivyowaagiza. Mose alikuwa na umri wa miaka themanini na Aroni alikuwa na umri wa miaka themanini na mitatu walipozungumza na Farao. BWANA akamwambia Mose na Aroni, “Farao atakapowaambia, ‘Fanyeni muujiza,’ basi mwambie Aroni, ‘Chukua fimbo yako na uitupe chini mbele ya Farao,’ nayo fimbo itakuwa nyoka.” Ndipo Mose na Aroni wakaenda kwa Farao wakafanya sawasawa kama vile BWANA alivyoagiza. Aroni akaitupa ile fimbo yake chini mbele ya Farao na maafisa wake, nayo ikawa nyoka. Farao naye akawaita watu wenye maarifa na wachawi na waganga wa Kimisri, nao wakafanya vivyo hivyo kwa siri ya uganga wao. Kila mmoja alitupa fimbo yake chini, nayo ikawa nyoka. Lakini fimbo ya Aroni ikazimeza zile fimbo zao. Hata hivyo moyo wa Farao ukawa mgumu, naye hakuwasikiliza Mose na Aroni, sawasawa kama vile BWANA alivyokuwa amesema.