Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 40:17-33

Kutoka 40:17-33 NEN

Kwa hiyo Maskani ya Mungu ilisimikwa katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, katika mwaka wa pili. Mose alipoweka wakfu Maskani ya Mungu, aliweka vitako mahali pake, akasimamisha mihimili, akatia mataruma na kusimamisha nguzo. Kisha akalitandaza hema juu ya Maskani ya Mungu na kuifunika hema, kama BWANA alivyomwagiza. Akachukua ule Ushuhuda na kuuweka ndani ya Sanduku la Agano, akaweka ile mipiko ya kubebea hilo Sanduku na kuweka kiti cha rehema juu yake. Kisha Mose akalileta Sanduku ndani ya Maskani ya Mungu, akatundika pazia ili kulifunika Sanduku la Ushuhuda, kama BWANA alivyomwagiza. Mose akaweka meza ndani ya Hema la Kukutania, upande wa kaskazini ya Maskani ya Mungu nje ya pazia na kupanga mikate juu yake mbele za BWANA, kama BWANA alivyomwagiza. Akaweka kinara cha taa ndani ya Hema la Kukutania mkabala na meza upande wa kusini mwa Maskani ya Mungu na kuziweka taa mbele za BWANA, kama BWANA alivyomwagiza. Mose akaweka madhabahu ya dhahabu ndani ya Hema la Kukutania mbele ya pazia na kufukiza uvumba wenye harufu nzuri, kama BWANA alivyomwagiza. Kisha akaweka pazia kwenye ingilio la Maskani ya Mungu. Mose akaweka madhabahu ya sadaka za kuteketezwa karibu na ingilio la Maskani ya Mungu, yaani Hema la Kukutania, na kutoa juu yake sadaka za kuteketezwa na sadaka za nafaka kama BWANA alivyomwagiza. Akaweka sinia kati ya Hema la Kukutania na madhabahu, akaweka maji ndani yake kwa ajili ya kunawia, Naye Mose, Aroni na wanawe wakayatumia kwa kunawia mikono na miguu yao. Wakanawa kila walipoingia katika Hema la Kukutania au walipoikaribia madhabahu kama BWANA alivyomwagiza Mose. Kisha Mose akafanya ua kuizunguka Maskani ya Mungu na madhabahu, pia akaweka pazia kwenye ingilio la huo ua. Hivyo Mose akaikamilisha kazi.