Kutoka 29:15-39
Kutoka 29:15-39 NENO
“Chukua mmoja wa wale kondoo dume, naye Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake. Mchinje huyo kondoo dume, chukua damu yake na uinyunyize pande zote za hayo madhabahu. Mkate huyo kondoo dume vipande vipande na usafishe sehemu za ndani pamoja na miguu, ukiviweka pamoja na kichwa na vipande vingine. Kisha mteketeze huyo kondoo dume mzima juu ya madhabahu. Hii ni sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu, harufu ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto. “Mchukue yule kondoo dume mwingine, naye Haruni na wanawe waweke mikono yao juu ya kichwa chake. Mchinje, uchukue sehemu ya damu yake na kuipaka kwenye masikio ya Haruni na wanawe, kwenye vidole gumba vya mikono yao ya kuume, pia kwenye vidole gumba vya miguu yao ya kuume. Kisha nyunyiza hiyo damu pande zote za madhabahu. Pia chukua sehemu ya damu iliyo juu ya madhabahu na sehemu ya mafuta ya upako, umnyunyizie Haruni na mavazi yake, pia wanawe na mavazi yao. Ndipo Haruni na wanawe pamoja na mavazi yao watakuwa wamewekwa wakfu. “Chukua mafuta ya huyu kondoo dume, mafuta ya mkia, mafuta ya sehemu za ndani, kipande kirefu cha ini, figo zote mbili na mafuta yake, pamoja na paja la kulia. (Huyo ndiye kondoo dume kwa ajili ya kuwaweka wakfu.) Kutoka kwa kile kikapu chenye mikate iliyotengenezwa bila chachu, kilichoko mbele za Mwenyezi Mungu, chukua mkate, andazi lililokandwa kwa mafuta, na mkate mwembamba. Viweke vitu hivi vyote mikononi mwa Haruni na wanawe na uviinue mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa. Kisha vichukue vitu hivyo kutoka mikononi mwao, uviteketeze juu ya madhabahu pamoja na sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu nzuri ya kupendeza kwa Mwenyezi Mungu, sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto. Baada ya kuchukua kidari cha huyo kondoo dume wa kuwekwa wakfu kwa Haruni, kiinue mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa, nayo itakuwa fungu lako. “Weka wakfu zile sehemu za kondoo dume aliyetumika kwa kumweka wakfu Haruni na wanawe: kidari kile kilichoinuliwa na lile paja lililotolewa. Siku zote hili litakuwa fungu la milele kutoka kwa Waisraeli kwa ajili ya Haruni na wanawe. Hili ni toleo la Waisraeli watakalotoa kwa Mwenyezi Mungu kutoka sadaka zao za amani. “Mavazi matakatifu ya Haruni yatakuwa ya wazao wake ili waweze kupakwa mafuta na kuwekwa wakfu wakiwa wameyavaa. Mwana atakayeingia mahali pake kuwa kuhani na kuja kwenye Hema la Kukutania kuhudumu katika Mahali Patakatifu atayavaa kwa siku saba. “Chukua nyama ya huyo kondoo dume wa kuwaweka wakfu uipike katika Mahali Patakatifu. Haruni na wanawe wataila ile nyama ya huyo kondoo dume pamoja na ile mikate iliyo kwenye hicho kikapu wakiwa hapo ingilio la Hema la Kukutania. Watakula sadaka hizi ambazo upatanisho ulifanywa kwazo kwa ajili ya kuwaweka wakfu na kuwatakasa. Lakini hakuna mtu mwingine yeyote anayeruhusiwa kuvila, kwa sababu ni vitakatifu. Ikiwa nyama yoyote ya huyo kondoo dume iliyotumika kwa kuwaweka wakfu au mkate wowote umebaki hadi asubuhi, vichomwe. Kamwe visiliwe, kwa sababu ni vitakatifu. “Hivyo utamfanyia Haruni na wanawe kila kitu kama vile nilivyokuamuru: Utachukua muda wa siku saba kuwaweka wakfu. Utatoa dhabihu ya fahali kila siku kuwa sadaka ya dhambi ili kufanya upatanisho. Takasa madhabahu kwa kufanya upatanisho kwa ajili yake, nayo uipake mafuta na kuiweka wakfu. Kwa muda wa siku saba fanya upatanisho kwa ajili ya madhabahu na kuiweka wakfu. Ndipo madhabahu itakuwa takatifu sana na chochote kitakachoigusa kitakuwa kitakatifu. “Kwa kawaida hiki ndicho utakachotoa juu ya madhabahu kila siku: wana-kondoo wawili wenye umri wa mwaka mmoja. Utamtoa mmoja asubuhi na huyo mwingine jioni.