Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kut 29:15-39

Kut 29:15-39 SUV

Pia mtwae kondoo mume mmoja; na Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake huyo kondoo mume. Kisha utamchinja huyo kondoo mume, na kuitwaa damu yake, na kuinyunyiza katika madhabahu kuizunguka kando-kando. Kisha utamkata-kata kondoo vipande vyake, na kuyaosha matumbo yake na miguu yake, na kuiweka pamoja na vipande vyake na kichwa chake. Nawe mteketeze kondoo mzima juu ya madhabahu; ni sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya BWANA; ni harufu nzuri, sadaka iliyosongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto. Kisha mtwae huyo kondoo wa pili; na Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake huyo kondoo. Kisha utamchinja kondoo, na kuitwaa damu yake, na kuitia katika ncha ya sikio la Haruni la upande wa kuume, na katika ncha za masikio ya kuume ya wanawe, na katika vyanda vya gumba vya mikono yao ya kuume, na katika vidole vikuu vya miguu yao ya kuume, na kuinyunyiza hiyo damu katika madhabahu kuizunguka kando-kando. Kisha twaa katika hiyo damu iliyo juu ya madhabahu, na katika hayo mafuta ya kutiwa, na kumnyunyizia Haruni, juu ya mavazi yake, na wanawe, na mavazi yao pia, pamoja naye; naye atatakaswa, na mavazi yake, na wanawe, na mavazi ya wanawe, pamoja naye. Tena yatwae mafuta ya huyo kondoo mume, na mkia wake wa mafuta, na mafuta yafunikayo matumbo, na kitambi kilicho katika ini, na figo mbili, na mafuta yaliyo katika hizo figo, na paja la kuume; kwani ni kondoo ambaye ni wa kuwekwa kwa kazi takatifu; utwae na mkate mmoja wa unga, na mkate mmoja ulioandaliwa kwa mafuta, na kaki moja katika kile kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, kilichowekwa mbele ya BWANA; nawe utavitia hivi vyote katika mikono ya Haruni, na katika mikono ya wanawe; nawe utavitikisa-tikisa viwe sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA. Kisha uvitwae vile vitu mikononi mwao, na kuviteketeza juu ya madhabahu, juu ya ile sadaka ya kuteketezwa, viwe harufu nzuri mbele ya BWANA; ni sadaka iliyosongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto. Kisha twaa kidari cha huyo kondoo wa kuwekwa kwake Haruni kwa kazi takatifu, na kukitikisa-tikisa kiwe sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA; nacho kitakuwa ni sehemu yako. Nawe kitakase kile kidari cha ile sadaka ya kutikiswa, na lile paja la sadaka ya kuinuliwa, lililotikiswa, na lililoinuliwa juu, vya yule kondoo wa kuwekwa kwa kazi takatifu, huyo aliyekuwa kwa ajili ya Haruni, na huyo aliyekuwa kwa ajili ya wanawe; navyo vitakuwa vya Haruni na wanawe posho ya lazima sikuzote itokayo kwa hao wana wa Israeli; kwa kuwa ni sadaka ya kuinuliwa; nayo itakuwa ni sadaka ya kuinuliwa itokayo kwa hao wana wa Israeli katika dhabihu zao za sadaka za amani, ni sadaka yao ya kuinuliwa kwa ajili ya BWANA. Na hayo mavazi matakatifu ya Haruni yatakuwa ya wanawe baada yake, wayavae watakapotiwa mafuta, na watakapowekwa kwa kazi takatifu. Huyo mwanawe atakayekuwa kuhani badala yake atayavaa muda wa siku saba, hapo atakapoingia ndani ya hiyo hema ya kukutania, ili atumike ndani ya mahali patakatifu. Nawe twaa huyo kondoo mume aliyekuwa wa kuwekwa kwa kazi takatifu, na kuitokosa nyama yake katika mahali patakatifu. Na Haruni na wanawe wataila ile nyama ya kondoo, na mikate iliyo katika kile kikapu, hapo mbele ya mlango wa hema ya kukutania. Nao watakula vile vitu ambavyo upatanisho ulifanywa kwa hivyo, ili kuwaweka kwa kazi takatifu na kuwatakasa; lakini mgeni asivile, maana, ni vitu vitakatifu. Na kwamba kitu cho chote cha ile nyama, iliyo kwa ajili ya kuweka kwa kazi takatifu, au cho chote cha hiyo mikate, kikisalia hata asubuhi, ndipo utavichoma kwa moto hivyo vilivyosalia; havitaliwa, maana, ni vitu vitakatifu. Ni hivyo utakavyowatendea Haruni na wanawe, sawasawa na hayo yote niliyokuagiza; utawaweka kwa kazi takatifu siku saba. Kila siku utamtoa ng’ombe wa sadaka ya dhambi kwa ajili ya upatanisho; nawe utaisafisha hiyo madhabahu, hapo utakapofanya upatanisho kwa ajili ya hiyo madhabahu; nawe utaitia mafuta, ili kuitakasa. Utafanya upatanisho kwa ajili ya hiyo madhabahu muda wa siku saba, na kuitakasa; ndipo madhabahu itakapokuwa takatifu sana; kila kitu kiigusacho madhabahu kitakuwa kitakatifu. Basi sadaka utakazozitoa juu ya madhabahu ni hizi; wana-kondoo wa mwaka mmoja wawili siku baada ya siku daima. Mwana-kondoo mmoja utamchinja asubuhi; na mwana-kondoo wa pili utamchinja jioni