Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 28:31-39

Kutoka 28:31-39 NEN

“Shona joho la kisibau lote kwa kitambaa cha rangi ya buluu tupu, na katikati uweke nafasi ya kuingizia kichwa. Kutakuwa na utepe uliofumwa, unaofanana na ukosi kuizunguka nafasi hiyo, ili isichanike. Tengeneza makomamanga ya nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu kuzunguka pindo la hilo joho, na uweke pia vikengele vya dhahabu kati ya hayo makomamanga. Hivyo vikengele vya dhahabu na makomamanga vitapishana kuzunguka upindo wa joho lile. Ni lazima Aroni alivae anapofanya huduma. Sauti ya hivyo vikengele itasikika anapoingia na kutoka Mahali Patakatifu mbele za BWANA, ili asije akafa. “Tengeneza bamba la dhahabu safi na uchore juu yake maneno haya kama vile muhuri huchorwa: MTAKATIFU KWA BWANA. Lifunge hilo bamba kwa kamba ya buluu kwenye kilemba, nalo ni lazima liwe mbele ya kilemba. Aroni alivae bamba hilo kwenye paji la uso wake, naye atachukua hatia kuhusu sadaka takatifu za Waisraeli wanazoweka wakfu, sadaka za aina yoyote. Litakuwa kwenye paji la uso wa Aroni daima ili zikubalike kwa BWANA. “Fuma koti la kitani safi na ufanye kilemba cha kitani safi. Mshipi uwe ni kazi ya mtarizi.