Kutoka 28:31-39
Kutoka 28:31-39 Biblia Habari Njema (BHN)
“Utashona kanzu ya kuvalia kizibao kwa sufu ya rangi ya buluu. Itakuwa na nafasi ya kupitishia kichwa katikati, na nafasi hiyo itazungushiwa utepe uliofumwa ili isichanike. Kwenye upindo wake wa chini, kuzunguka pande zote, itapambwa kwa makomamanga ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, kutakuwa pia na njuga za dhahabu kati ya hayo makomamanga: Komamanga, njuga, komamanga, njuga, kuizunguka kanzu yote. Aroni atavaa kanzu hiyo kutekeleza huduma yake ya ukuhani na sauti yake itasikika wakati anapoingia mahali patakatifu mbele yangu na wakati anapotoka, njuga hizo zitasikika, naye hatauawa. “Kisha, utatengeneza kibati cha dhahabu safi na kuchora juu yake kama mtu achoravyo mhuri, ‘Wakfu kwa Mwenyezi-Mungu.’ Kibati hicho utakifunga mbele ya kilemba kwa ukanda wa buluu. Aroni atakivaa kibati hicho kwenye paji la uso wake; kwa hicho kibati atachukua lawama ya makosa ambayo Waisraeli wanaweza kuwa wameyafanya katika kunitolea tambiko takatifu, nami nitazikubali tambiko zao. Utamtengenezea Aroni joho iliyonakshiwa kwa kitani safi na kumfumia kilemba cha kitani safi na ukanda ulionakshiwa vizuri.
Kutoka 28:31-39 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nawe fanya hiyo joho la naivera ya rangi ya buluu yote. Nayo itakuwa na tundu katikati yake kwa kupitisha kichwa; itakuwa na utepe wa kazi ya kusokotwa kuzunguka hilo tundu lake, mfano wa tundu lililo katika kanzu ya chuma, ili lisipasuke. Nawe katika pindo zake utatia makomamanga ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, kuzunguka pindo zake kotekote; na njuga za dhahabu kati ya hayo makomamanga pande zote; njuga ya dhahabu na komamanga, katika pindo za joho kuizunguka pande zote. Nayo itakuwa juu ya Haruni akitumika; na sauti ya hizo njuga itasikika hapo aingiapo ndani ya mahali patakatifu mbele ya BWANA na hapo atokapo nje, ili kwamba asife. Nawe fanya bamba la dhahabu safi na kuchora juu yake, mfano wa michoro ya mihuri, MTAKATIFU KWA BWANA. Nawe ulitie hilo bamba katika ukanda wa rangi ya buluu, nalo litakuwa katika kile kilemba; litakuwa upande wa mbele wa kile kilemba. Nalo litakuwa katika kipaji cha uso cha Haruni, na Haruni atauchukua uovu wa vile vitu vitakatifu, watakavyovitakasa hao wana wa Israeli katika vipawa vyao vyote vitakatifu, nalo litakuwa katika kipaji chake cha uso sikuzote, ili vipate kukubaliwa mbele za BWANA. Na hiyo kanzu utaifuma ya kitani nzuri ya kazi ya urembo, ufanye na kilemba cha nguo ya kitani nzuri, nawe utafanya mshipi wenye kunakishiwa vizuri.
Kutoka 28:31-39 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nawe fanya hiyo joho ya naivera ya rangi ya samawi yote. Nayo itakuwa na tundu katikati yake kwa kupitisha kichwa; itakuwa na utepe wa kazi ya kusokotwa kuzunguka hilo tundu lake, mfano wa tundu lililo katika kanzu ya chuma, ili lisipasuke. Nawe katika pindo zake utatia makomamanga ya rangi ya samawi, na ya rangi ya zambarau, na ya rangi nyekundu, kuzunguka pindo zake kotekote; na njuga za dhahabu kati ya hayo makomamanga pande zote; njuga ya dhahabu na komamanga, njuga ya dhahabu na komamanga, katika pindo za joho kuizunguka pande zote. Nayo itakuwa juu ya Haruni akitumika; na sauti ya hizo njuga itasikilikana hapo aingiapo ndani ya mahali patakatifu mbele ya BWANA na hapo atokapo nje, ili kwamba asife. Nawe fanya bamba la dhahabu safi na kuchora juu yake, mfano wa machoro ya muhuri, MTAKATIFU KWA BWANA. Nawe ulitie hilo bamba katika ukanda wa rangi ya samawi, nalo litakuwa katika kile kilemba; litakuwa upande wa mbele wa kile kilemba. Nalo litakuwa katika kipaji cha uso cha Haruni, na Haruni atauchukua uovu wa vile vitu vitakatifu, watakavyovitakasa hao wana wa Israeli katika vipawa vyao vyote vitakatifu, nalo litakuwa katika kipaji chake cha uso sikuzote, ili kwamba vipate kukubaliwa mbele za BWANA. Na hiyo kanzu utaifuma ya kitani nzuri ya kazi ya urembo, ufanye na kilemba cha nguo ya kitani nzuri, nawe utafanya mshipi wa kazi ya mwenye kutia taraza.
Kutoka 28:31-39 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Shona joho la kisibau lote kwa kitambaa cha rangi ya buluu tupu, na katikati uweke nafasi ya kuingizia kichwa. Kutakuwa na utepe uliofumwa, unaofanana na ukosi kuizunguka nafasi hiyo, ili isichanike. Tengeneza makomamanga ya nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu kuzunguka pindo la hilo joho, na uweke pia vikengele vya dhahabu kati ya hayo makomamanga. Hivyo vikengele vya dhahabu na makomamanga vitapishana kuzunguka upindo wa joho lile. Ni lazima Aroni alivae anapofanya huduma. Sauti ya hivyo vikengele itasikika anapoingia na kutoka Mahali Patakatifu mbele za BWANA, ili asije akafa. “Tengeneza bamba la dhahabu safi na uchore juu yake maneno haya kama vile muhuri huchorwa: MTAKATIFU KWA BWANA. Lifunge hilo bamba kwa kamba ya buluu kwenye kilemba, nalo ni lazima liwe mbele ya kilemba. Aroni alivae bamba hilo kwenye paji la uso wake, naye atachukua hatia kuhusu sadaka takatifu za Waisraeli wanazoweka wakfu, sadaka za aina yoyote. Litakuwa kwenye paji la uso wa Aroni daima ili zikubalike kwa BWANA. “Fuma koti la kitani safi na ufanye kilemba cha kitani safi. Mshipi uwe ni kazi ya mtarizi.