Kutoka 27
27
Madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa
(Kutoka 38:1-7)
1“Jenga madhabahu ya mbao za mti wa mshita, kimo chake kiwe dhiraa tatu#27:1 Dhiraa 3 ni sawa na mita 1.35.; itakuwa mraba, urefu wake dhiraa tano#27:1 Dhiraa 5 ni sawa na mita 2.25., na upana wake dhiraa tano. 2Tengeneza upembe kwenye kila pembe ya hizo pembe nne, ili zile pembe na madhabahu ziwe zimeungana, na ufunike madhabahu kwa shaba. 3Tengeneza vyombo vyake vyote kwa shaba: vyungu vyake vya kuondolea majivu, masepetu, mabakuli ya kunyunyizia, uma za nyama, na vyombo vya kuchukulia moto. 4Kisha tengenezea hayo madhabahu wavu wa shaba, na utengeneze pete za shaba kwenye kila moja ya hizo pembe nne za huo wavu. 5Weka wavu huo chini ya ukingo wa madhabahu ili ufikie nusu ya kimo cha madhabahu. 6Tengeneza mipiko ya mti wa mshita kwa ajili ya madhabahu, na uifunike kwa shaba. 7Hiyo mipiko itaingizwa kwenye zile pete ili iwe pande mbili za madhabahu inapobebwa. 8Tengeneza madhabahu yawe na uvungu ndani yake ukitumia mbao. Utaitengeneza sawasawa na vile ulivyooneshwa mlimani.
Ua wa Hema la Kukutania
(Kutoka 38:9-20)
9“Tengeneza ua kwa ajili ya Hema la Kukutania. Upande wa kusini utakuwa na urefu wa dhiraa mia moja#27:9 Dhiraa 100 ni sawa na mita 45., na utakuwa na mapazia ya kitani iliyosokotwa vizuri, 10pamoja na nguzo ishirini na vitako vya shaba ishirini, na kulabu na tepe za fedha juu ya hizo nguzo. 11Upande wa kaskazini utakuwa na urefu wa dhiraa mia moja, nao utakuwa na mapazia, pamoja na nguzo ishirini na vitako vya shaba ishirini, pamoja na kulabu na tepe za fedha juu ya hizo nguzo.
12“Upande wa magharibi wa ua utakuwa na upana wa dhiraa hamsini#27:12 Dhiraa 50 ni sawa na mita 22.5., nao utakuwa na mapazia, na nguzo kumi na vitako vyake kumi. 13Upande wa mwisho wa mashariki jua linakochomoza, ua pia utakuwa na upana wa dhiraa hamsini. 14Mapazia yenye urefu wa dhiraa kumi na tano yatakuwa upande mmoja wa ingilio, pamoja na nguzo tatu na vitako vitatu. 15Kutakuwa na mapazia ya dhiraa kumi na tano#27:15 Dhiraa 15 ni sawa na mita 6.75. kwa upande mwingine wa ingilio, pamoja na nguzo tatu na vitako vitatu.
16“Kuhusu ingilio la ua, weka pazia lenye urefu wa dhiraa ishirini#27:16 Dhiraa 20 ni sawa na mita 9. la nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu pamoja na kitani iliyosokotwa vizuri, kazi ya mtarizi. Pazia hilo litashikiliwa na nguzo nne na vitako vinne. 17Nguzo zote zinazozunguka ua zitakuwa na tepe na kulabu za fedha, na vitako vya shaba. 18Ua utakuwa na urefu wa dhiraa mia moja na upana wa dhiraa hamsini, ukiwa na mapazia ya kitani yaliyosokotwa vizuri yenye urefu wa dhiraa tano kwenda juu na vitako vya shaba. 19Vyombo vingine vyote vinavyotumika katika maskani ya Mungu kwa shughuli yoyote, pamoja na vigingi vyote na hata vile vya ua, vitakuwa vya shaba.
Mafuta ya kinara cha taa
(Walawi 24:1-4)
20“Utawaamuru Waisraeli wakuletee mafuta safi ya zeituni yaliyokamuliwa kwa ajili ya mwanga ili zile taa ziwake mfululizo. 21Katika Hema la Kukutania, nje ya pazia lililo mbele ya Sanduku la Ushuhuda, Haruni na wanawe watahakikisha kuwa taa hizo zinawaka kuanzia jioni hadi asubuhi mbele za Mwenyezi Mungu. Hili litakuwa agizo la milele miongoni mwa Waisraeli kwa vizazi vijavyo.
Iliyochaguliwa sasa
Kutoka 27: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.