Kutoka 11
11
Pigo la kumi: Kuuawa wazaliwa wa kwanza
1Basi Mwenyezi Mungu alikuwa amemwambia Musa, “Nitaleta pigo moja zaidi kwa Farao na katika nchi ya Misri. Baada ya hilo, atawaacha mwondoke hapa na atakapofanya hivyo, atawafukuza mtoke kabisa. 2Waambie watu wote kwamba kila mwanaume na kila mwanamke amwombe jirani yake vitu vya fedha na vya dhahabu.” 3(Mwenyezi Mungu akawafanya Wamisri wawe na moyo wa ukarimu kwa Waisraeli, naye Musa mwenyewe akaheshimiwa sana na maafisa wa Farao na watu wote katika nchi ya Misri.)
4Kwa hiyo Musa akasema, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Usiku wa manane, Mimi nitapita katika nchi yote ya Misri. 5Kila mwanaume kifungua mimba katika Misri atakufa, kuanzia mzaliwa wa kwanza wa kiume wa Farao, anayeketi kwenye kiti cha ufalme, hadi mzaliwa wa kwanza wa kiume wa mjakazi, anayesaga nafaka kwa jiwe, pamoja na kila mzaliwa wa kwanza wa mifugo. 6Kutakuwa na kilio kikubwa katika nchi yote ya Misri, kilio ambacho hakijakuwa, wala kamwe hakitakuwa tena. 7Lakini miongoni mwa Waisraeli hakuna hata mbwa atakayembwekea mwanadamu wala mnyama yeyote.’ Ndipo mtajua kuwa Mwenyezi Mungu huweka tofauti kati ya Misri na Israeli. 8Maafisa hawa wako wote watanijia, wakisujudu mbele yangu, wakisema, ‘Ondoka, wewe pamoja na watu wako wote wanaokufuata!’ Baada ya haya nitaondoka.” Kisha Musa, akiwa amewaka hasira, akamwacha Farao.
9Mwenyezi Mungu alikuwa amemwambia Musa, “Farao atakataa kukusikiliza, ili maajabu yangu yapate kuongezeka katika nchi ya Misri.” 10Musa na Haruni wakafanya maajabu haya yote mbele ya Farao, lakini Mwenyezi Mungu akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, wala hakuwaachia Waisraeli waondoke katika nchi yake.
Iliyochaguliwa sasa
Kutoka 11: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.