Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Esta 5:1-8

Esta 5:1-8 NENO

Siku ya tatu, Esta alivaa mavazi yake ya kimalkia, naye akasimama katika ua wa ndani wa jumba la mfalme, mbele ya ukumbi wa mfalme. Naye mfalme alikuwa ameketi kwenye kiti chake cha kifalme katika ukumbi, akielekea langoni. Alipomwona Malkia Esta amesimama uani alipendezwa naye, akamnyooshea fimbo ya utawala ya dhahabu iliyokuwa mkononi mwake. Kwa hiyo Esta alikaribia na kuigusa ncha ya fimbo ya mfalme. Kisha mfalme aliuliza, “Malkia Esta, ni nini? Ombi lako ni nini? Hata kama ni nusu ya ufalme, utapewa.” Esta akajibu, “Kama itampendeza mfalme, mfalme pamoja na Hamani waje leo katika karamu niliyomwandalia.” Mfalme akasema, “Mleteni Hamani mara moja, ili tupate kufanya lile Esta analoomba.” Kwa hiyo mfalme na Hamani walihudhuria karamu aliyoiandaa Esta. Walipokuwa wakinywa mvinyo mfalme akamuuliza Esta tena, “Sasa haja yako ni nini? Utapewa. Ombi lako ni nini? Hata nusu ya ufalme, utapewa.” Esta akajibu, “Haja yangu na ombi langu ni hili: Kama mfalme ameona vyema, nami nimepata kibali kwake, na ikimpendeza mfalme kunipa ombi langu na kunitimizia haja yangu, mfalme na Hamani waje kwangu kesho katika karamu nitakayowaandalia. Kisha nitajibu swali la mfalme.”