Esta 5:1-8
Esta 5:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku ya tatu ya mfungo wake, Esta alivalia mavazi yake ya kimalkia, akaenda akasimama katika ua wa ndani wa nyumba ya mfalme, kuelekea ukumbi wa mfalme. Mfalme alikuwamo ndani, amekaa katika kiti chake cha enzi, kuelekea mlango wa nyumba ya mfalme. Mfalme alipomwona malkia Esta amesimama uani, alipendezwa naye, akamnyoshea fimbo ya dhahabu aliyokuwa ameshika mkononi mwake. Esta akakaribia, akagusa ncha ya fimbo. Hapo mfalme akauliza, “Unataka nini Esta? Niambie unachotaka, nawe utapata – hata kama ni nusu ya ufalme wangu.” Esta akamjibu, “Ukipenda, ewe mfalme, uje leo pamoja na Hamani, kwenye karamu ninayoandaa kwa ajili yako, mfalme.” Mfalme akatoa amri Hamani aje upesi, kama Esta alivyoomba. Basi, mfalme na Hamani wakaenda kwenye karamu aliyoandaa Esta. Walipokuwa wanakunywa divai, mfalme akamwuliza tena Esta: “Unataka nini? Niambie, nawe utapata. Ombi lako ni nini? Hata kama ni nusu ya ufalme wangu, utapewa.” Esta akamjibu, “Ombi langu ni hili: Kama u radhi, ewe mfalme, kukubali ombi langu, basi, naomba wewe na Hamani mje kesho kwenye karamu nyingine nitakayowaandalieni. Wakati huo nitakujulisha ombi langu.”
Esta 5:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa siku ya tatu Esta alijivika mavazi yake ya kifalme, akasimama katika ua wa ndani wa nyumba ya mfalme, kuielekea nyumba ya mfalme; naye mfalme akaketi juu ya kiti chake cha enzi katika nyumba ya mfalme, kuuelekea mlango wa kasri. Ikawa, mfalme alipomwona malkia Esta amesimama uani, yeye akapata kibali machoni pake; naye mfalme akamnyoshea Esta fimbo ya dhahabu aliyokuwa nayo mkononi. Basi Esta akakaribia, akaigusa ncha ya fimbo. Mfalme akamwambia, malkia Esta, unataka nini? Nayo ni haja gani uliyo nayo? Utapewa hata nusu ya ufalme. Esta akasema, Mfalme akiona vema, na aje leo, mfalme na Hamani, kwenye karamu niliyomwandalia. Basi mfalme akasema, Mhimize Hamani, ili ifanyike kama Esta alivyoomba. Hivyo mfalme na Hamani wakafika katika karamu ile aliyoiandaa Esta. Basi mfalme akamwambia Esta pale penye karamu ya divai, Dua yako ni nini? Nawe utapewa; na haja yako ni nini? Hata nusu ya ufalme utatimiziwa. Esta akajibu, na kusema, Dua yangu ni hii, na haja yangu ni hii, Ikiwa nimepata kibali machoni pa mfalme, na mfalme akiona vema kunipa niombalo, na kunitimizia haja yangu, na aje tena mfalme na Hamani kwenye karamu nitakayowaandalia, nami kesho nitafanya kama vile mfalme alivyosema.
Esta 5:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa siku ya tatu Esta alijivika mavazi yake ya kifalme, akasimama katika ua wa ndani wa nyumba ya mfalme, kuielekea nyumba ya mfalme; naye mfalme akaketi juu ya kiti chake cha enzi katika nyumba ya mfalme, kuuelekea mlango wa nyumba. Ikawa, mfalme alipomwona malkia Esta amesimama uani, yeye akapata kibali machoni pake; naye mfalme akamnyoshea Esta fimbo ya dhahabu aliyokuwa nayo mkononi. Basi Esta akakaribia, akaigusa ncha ya fimbo. Mfalme akamwambia, Malkia Esta, wataka nini? Nayo ni haja gani uliyo nayo? Utapewa hata nusu ya ufalme. Esta akasema, Mfalme akiona vema, na aje leo, mfalme na Hamani, kwenye karamu niliyomwandalia. Basi mfalme akasema, Mhimize Hamani, ili ifanyike kama Esta alivyosema. Hivyo mfalme na Hamani wakafika katika karamu ile aliyoiandaa Esta. Basi mfalme akamwambia Esta pale penye karamu ya divai, Dua yako ni nini? Nawe utapewa; na haja yako ni nini? Hata nusu ya ufalme utafanyiziwa. Esta akajibu, na kusema, Dua yangu ni hii, na haja yangu ni hii, Ikiwa nimepata kibali machoni pa mfalme, na mfalme akiona vema kunipa niombalo, na kunifanyizia haja yangu, na aje tena mfalme na Hamani kwenye karamu nitakayowaandalia, nami kesho nitafanya kama vile mfalme alivyosema.
Esta 5:1-8 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Siku ya tatu, Esta alivaa mavazi yake ya kimalkia, naye akasimama katika ua wa ndani wa jumba la mfalme, mbele ya ukumbi wa mfalme. Naye mfalme alikuwa ameketi kwenye kiti chake cha kifalme katika ukumbi, akielekea langoni. Alipomwona Malkia Esta amesimama uani alipendezwa naye, akamnyooshea fimbo ya utawala ya dhahabu iliyokuwa mkononi mwake. Kwa hiyo Esta alikaribia na kuigusa ncha ya fimbo ya mfalme. Kisha mfalme aliuliza, “Malkia Esta, ni nini? Ombi lako ni nini? Hata kama ni nusu ya ufalme, utapewa.” Esta akajibu, “Kama itampendeza mfalme, mfalme pamoja na Hamani waje leo katika karamu niliyomwandalia.” Mfalme akasema, “Mleteni Hamani mara moja, ili tupate kufanya lile Esta analoomba.” Kwa hiyo mfalme na Hamani walihudhuria karamu aliyoiandaa Esta. Walipokuwa wakinywa mvinyo mfalme akamuuliza Esta tena, “Sasa haja yako ni nini? Utapewa. Ombi lako ni nini? Hata nusu ya ufalme, utapewa.” Esta akajibu, “Haja yangu na ombi langu ni hili: Kama mfalme ameona vyema, nami nimepata kibali kwake, na ikimpendeza mfalme kunipa ombi langu na kunitimizia haja yangu, mfalme na Hamani waje kwangu kesho katika karamu nitakayowaandalia. Kisha nitajibu swali la mfalme.”