Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Esta 2:12-19

Esta 2:12-19 NEN

Kabla zamu ya msichana haijafika ya kwenda kwa Mfalme Ahasuero, ilimbidi atimize miezi kumi na miwili ya matunzo ya urembo kama ilivyokuwa imepangwa. Kwa miezi sita walikuwa wajipake mafuta ya manemane, na miezi sita kujipaka manukato na vipodozi. Basi hivi ndivyo ambavyo msichana angeingia kwa mfalme: Kila kitu alichohitaji aliruhusiwa kuchukua kutoka nyumba ya wanawake na kwenda navyo katika jumba la mfalme. Jioni angekwenda pale na asubuhi kurudi sehemu nyingine ya nyumba ya wanawake katika utunzaji wa Shaashgazi, towashi wa mfalme ambaye alikuwa mkuu wa masuria. Hangeweza kurudi kwa mfalme mpaka apendezwe naye na kuagiza aitwe kwa jina lake. Zamu ya Esta ilipofika kwenda kwa mfalme (msichana ambaye Mordekai alikuwa amemlea, binti wa Abihaili mjomba wake), Esta hakutaka vitu zaidi ya vile ambavyo Hegai, towashi wa mfalme aliyekuwa mkuu wa nyumba ya wanawake alivyokuwa amemshauri. Naye Esta alipata kibali kwa kila mtu aliyemwona. Esta alipelekwa kwa Mfalme Ahasuero katika makao ya mfalme mwezi wa kumi, yaani mwezi wa Tebethi, katika mwaka wake wa saba wa kutawala. Basi ikawa mfalme alivutiwa na Esta kuliko wanawake wengine wote, naye akapata upendeleo na kibali kuliko mabikira wengine. Kisha akamvika taji la kifalme kichwani mwake na kumfanya malkia badala ya Vashti. Mfalme akafanya karamu kubwa, karamu ya Esta, kwa wakuu wake wote na maafisa. Mfalme alitangaza mapumziko katika majimbo yake yote na kugawa zawadi kwa ukarimu wa kifalme. Wakati mabikira walikusanyika mara ya pili, Mordekai alikuwa ameketi katika lango la mfalme.