Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 8

8
Usimsahau Mwenyezi Mungu
1Uwe mwangalifu kufuata kila agizo ninalokupa wewe leo, ili mweze kuishi, kuongezeka na mweze kuingia mkamiliki nchi ambayo Mwenyezi Mungu aliahidi kwa kiapo kwa baba zenu. 2Kumbuka jinsi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alivyowaongoza katika njia yote katika jangwa kwa miaka hii arobaini, kukunyenyekeza na kukujaribu ili ajue lililoko moyoni mwako, kwamba utayashika maagizo yake au la. 3Alikudhili na kukufanya uone njaa kisha akulishe kwa mana, ambayo wewe wala baba zako hamkuijua, awafundishe kuwa mwanadamu hataishi kwa mkate tu bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mwenyezi Mungu. 4Nguo zenu hazikuchakaa wala miguu yenu haikuvimba kwa miaka hii arobaini. 5Mjue basi ndani ya mioyo yenu kama mtu anavyomwadibisha mwanawe, ndivyo Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atawaadibisha ninyi.
6Shikeni maagizo ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mtembee katika njia zake na kumheshimu. 7Kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawaleta katika nchi nzuri, nchi yenye vijito na mabwawa ya maji, yenye chemchemi zinazotiririka mabondeni na katika vilima; 8nchi yenye ngano na shayiri, mizabibu na mitini, mikomamanga, mafuta ya zeituni na asali; 9nchi ambayo chakula hakitapungua na hamtakosa chochote; nchi ambayo miamba yake ni chuma na mnaweza kuchimba shaba kwenye vilima.
10Mtakapokwisha kula na kushiba, msifuni Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa ajili ya nchi nzuri aliyowapa. 11Jihadharini msimsahau Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mkashindwa kushika maagizo yake, sheria na amri zake ambazo ninawapa leo. 12Angalia wakati mtakapokuwa mmekula na kushiba, mkajenga nyumba nzuri na kukaa humo, 13na wakati makundi yenu ya ng’ombe na mbuzi na kondoo yatakapoongezeka na fedha na dhahabu yenu itakapoongezeka na vyote mlivyo navyo vitakapozidishwa, 14basi mioyo yenu isiwe na kiburi mkamsahau Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliyewatoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa. 15Aliwaongoza kupitia jangwa lile kubwa na la kutisha, nchi ile ya kiu isiyo na maji, yenye nyoka wa sumu na nge. Aliwatolea maji katika mwamba mgumu. 16Aliwapa mana ya kula jangwani, kitu ambacho baba zenu hawakukijua, ili kuwanyenyekeza na kuwajaribu ninyi, na mwishoni apate kuwatendea mema. 17Mnaweza kusema, “Uwezo wangu na nguvu za mikono yangu ndizo zilizonipatia utajiri huu.” 18Lakini kumbukeni Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ndiye ambaye huwapa uwezo wa kupata utajiri, na hivyo kulithibitisha agano lake, ambalo aliwaapia baba zenu, kama ilivyo leo.
19Ikiwa mtamsahau Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mkaifuata miungu mingine, mkaiabudu na kuisujudia, ninashuhudia dhidi yenu leo kwamba hakika mtaangamizwa. 20Kama mataifa Mwenyezi Mungu aliyoyaangamiza mbele yenu, ndivyo ninyi mtakavyoangamizwa kwa kutokumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.

Iliyochaguliwa sasa

Kumbukumbu 8: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia