Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 7

7
Kuyafukuza mataifa
(Kutoka 34:11-16)
1Mwenyezi Mungu, Mungu wako, akuletapo katika nchi unayoingia kuimiliki, na awafukuzapo mbele yako mataifa mengi, yaani Wahiti, Wagirgashi, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, mataifa saba makubwa tena yenye nguvu kuliko wewe, 2pia Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakapowatia mkononi mwako na ukawashinda, basi ni lazima uwaangamize wote kabisa. Usifanye agano nao, wala usiwahurumie. 3Usioane nao. Usimtoe binti yako kuolewa na mwanawe, au kumchukua binti yake aolewe na mwanao. 4Kwa maana watamgeuza mwanao aache kunifuata, ili aitumikia miungu mingine, nayo hasira ya Mwenyezi Mungu itawaka dhidi yako, naye atakuangamiza ghafula. 5Hili ndilo utakalowafanyia: Vunja madhabahu yao, vunja mawe yao ya kuabudia, katakata nguzo zao za Ashera, na kuchoma sanamu zao kwa moto; 6kwa kuwa wewe ni taifa takatifu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako. Mwenyezi Mungu, Mungu wako, amekuchagua kutoka mataifa yote duniani uwe taifa lake, hazina yake ya pekee.
7Mwenyezi Mungu hakuweka upendo wake juu yenu na kuwachagua kwa sababu mlikuwa wengi mno kuliko watu wengine, kwa maana ninyi ndio mliokuwa wachache sana kuliko mataifa yote. 8Lakini ni kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwapenda ninyi na kutunza kiapo alichowaapia babu zenu kwamba atawatoa ninyi kwa mkono wenye nguvu na kuwakomboa kutoka nchi ya utumwa, kutoka nguvu za Farao mfalme wa Misri. 9Basi ujue kwamba Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ndiye Mungu; ni Mungu mwaminifu, anayetunza agano la upendo kwa maelfu ya vizazi vya wale wanaompenda na kuzishika amri zake. 10Lakini
kwa wale wanaomchukia
atawalipiza kwenye nyuso zao
kwa maangamizi;
hatachelewa kuwalipiza kwenye nyuso zao
wale wamchukiao.
11Kwa hiyo, kuweni waangalifu kufuata maagizo, amri na sheria ninazowapa leo.
Baraka za utiifu
(Kumbukumbu 28:1-14)
12Mkizingatia sheria hizi na kuzifuata kwa uangalifu, basi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atatunza agano lake la upendo nanyi, kama alivyowaapia baba zenu. 13Atawapenda ninyi na kuwabariki na kuongeza idadi yenu. Atabariki uzao wa tumbo lenu, mazao ya nchi yenu, nafaka, divai mpya na mafuta, ndama za ng’ombe wa makundi yenu, na kondoo wa makundi yenu katika nchi ile aliyoapa kuwapa baba zenu. 14Mtabarikiwa kuliko mataifa mengine yote, hakuna wanaume wala wanawake kwenu watakaokosa watoto, wala mifugo yenu haitakuwa tasa. 15Mwenyezi Mungu atawakinga na kila ugonjwa. Mungu hatatia juu yenu ugonjwa wowote mbaya mlioufahamu huko Misri, lakini atatia ugonjwa juu ya wale wote wanaokuchukia. 16Ni lazima mwangamize watu wote ambao Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atawatia mikononi mwenu. Msiwatazame kwa kuwahurumia na msiitumikie miungu yao, kwa kuwa itakuwa mtego kwenu.
17Mnaweza kujiuliza wenyewe: “Mataifa haya ni yenye nguvu kuliko sisi. Tutawezaje kuwafukuza?” 18Lakini msiwaogope. Kumbukeni vyema jinsi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alivyofanya kwa Farao na kwa wote huko Misri. 19Mliona kwa macho yenu wenyewe majaribu makubwa, ishara za miujiza na maajabu, mkono wenye nguvu na ulionyooshwa, ambao kwa huo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliwatoa mtoke Misri. Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atawafanyia hivyo watu wote ambao mnawaogopa sasa. 20Zaidi ya hayo, Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atatuma nyigu miongoni mwao hadi yale mabaki watakaojificha waangamie. 21Msiingiwe na hofu kwa sababu yao, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ambaye yupo miongoni mwenu ni mkuu naye ni Mungu wa kutisha. 22Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atawafukuza mataifa hayo mbele yenu kidogo kidogo. Hamtaruhusiwa kuwaondoa wote kwa mara moja, la sivyo wanyama pori wataongezeka na kuwa karibu nanyi. 23Lakini Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atawatia watu hao mikononi mwenu, akiwatia katika machafuko makubwa hadi waangamizwe. 24Atawatia wafalme wao mikononi mwenu, nanyi mtayafuta majina yao chini ya mbingu. Hakuna hata mmoja atakayeweza kusimama dhidi yenu bali mtawaangamiza. 25Sanamu za miungu yao mtazichoma moto. Msitamani fedha wala dhahabu iliyo juu ya vinyago hivyo, wala msiichukue iwe yenu, la sivyo mtakuwa mmetekwa nayo. Kwa kuwa ni chukizo kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. 26Msilete vitu vya machukizo katika nyumba zenu kwani ninyi, mtatengwa kama vitu hivyo kwa maangamizi. Ukichukie kabisa kitu hicho kwa kuwa kimetengwa kwa maangamizi.

Iliyochaguliwa sasa

Kumbukumbu 7: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia