Kumbukumbu 4:1-8
Kumbukumbu 4:1-8 NENO
Sikia sasa, ee Israeli, amri na sheria nitakazokufundisha wewe. Zifuate ili upate kuishi na uingie kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zako, anawapa. Usiongeze wala usipunguze chochote ninachowaamuru ninyi, ila myashike maagizo ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ambayo nawapa. Mliona kwa macho yenu wenyewe kile Mwenyezi Mungu alichokifanya kule Baal-Peori. Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliwaangamiza kutoka miongoni mwenu kila mmoja aliyemfuata Baali wa Peori, lakini ninyi nyote mlioshikamana na Mwenyezi Mungu kwa uthabiti, Mungu wenu, mko hai hadi leo. Tazama, nimewafundisha amri na sheria kama Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, alivyoniamuru mimi, ili mzifuate katika nchi mnayoiingia kuimiliki. Zishikeni kwa uangalifu, kwa kuwa hii itaonesha hekima na ufahamu wenu kwa mataifa, ambayo yatasikia kuhusu amri zote hizi, nao watasema, “Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na ufahamu.” Ni taifa gani jingine lililo kubwa kiasi cha kuwa na miungu yao iliyo karibu nao kama Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, alivyo karibu nasi wakati wowote tunapomwomba? Nalo ni taifa gani jingine lililo kubwa hivi lenye kuwa na amri na sheria za haki kama hizi ninazoweka mbele yenu leo?