Kumbukumbu la Sheria 4:1-8
Kumbukumbu la Sheria 4:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Mose akaendelea kusema, “Zingatieni basi na kufuata masharti yote na maagizo niliyowafundisha, ili mpate kuishi na kumiliki nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, anawapeni. Msiongeze chochote katika amri ninazowapeni, wala msipunguze kitu; zingatieni amri za Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ambazo ninawapeni. Nyinyi mliona kwa macho yenu mambo ambayo Mwenyezi-Mungu aliyafanya kuhusu Baal-peori. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliwaangamiza watu wote miongoni mwenu waliomwabudu huyo mungu Baal-peori. Lakini nyinyi mliokuwa waaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mko hai hadi leo. “Haya! Nimewafundisheni masharti na maagizo kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, alivyoniamuru nifanye, ili muyazingatie katika nchi mnayokwenda kuimiliki. Shikeni na kuyatekeleza masharti na maagizo hayo maana mkifanya hivyo watu wa mataifa mengine watakapopata kujua masharti hayo, watatambua kuwa nyinyi ni wenye hekima na busara, wakisema: ‘Kweli watu wa taifa hili kuu wana hekima na busara!’ “Hakuna taifa lolote hata liwe kuu namna gani, ambalo mungu wake yuko karibu nalo, kama alivyo karibu nasi Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, tunapomwomba msaada. Wala hakuna taifa lingine lolote hata liwe kuu namna gani, lenye masharti na maagizo ya haki, kama hayo ambayo nimewafundisha siku hii ya leo.
Kumbukumbu la Sheria 4:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na sasa, Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu ninazowafundisha, ili mzitende; mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi anayowapa BWANA, Mungu wa baba zenu. Msiliongeze neno ninalowaamuru wala msilipunguze, mpate kuzishika amri za BWANA, Mungu wenu, ninazowaamuru. Macho yenu yameona aliyoyatenda BWANA kwa sababu ya Baal-peori; maana wote waliomfuata Baal-peori, BWANA, Mungu wako, amewaangamiza kutoka kati yako. Bali ninyi mlioambatana na BWANA, Mungu wenu, mnaishi kila mmoja wenu, hata leo. Angalieni nimewafundisha amri na hukumu, vile vile kama BWANA, Mungu wangu, alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi mwingiayo ili kuimiliki. Zishikeni basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili. Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama BWANA Mungu wetu alivyo kila tumwitapo? Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo?
Kumbukumbu la Sheria 4:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na sasa, Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mzitende; mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo BWANA, Mungu wa baba zenu. Msiliongeze neno niwaamurulo wala msilipunguze, mpate kuzishika amri za BWANA, Mungu wenu, niwaamuruzo. Macho yenu yameona aliyoyatenda BWANA kwa sababu ya Baal-peori; maana wote waliomfuata Baal-peori, BWANA, Mungu wako, amewaangamiza kutoka kati yako. Bali ninyi mlioambatana na BWANA, Mungu wenu, mnaishi kila mmoja wenu, hata leo. Angalieni nimewafundisha amri na hukumu, vile vile kama BWANA, Mungu wangu, alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi mwingiayo ili kuimiliki. Zishikeni basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili. Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama BWANA, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo? Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo.
Kumbukumbu la Sheria 4:1-8 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Sikia sasa, ee Israeli, amri na sheria nitakazokufundisha wewe. Zifuate ili upate kuishi na uingie kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zako, anawapa. Usiongeze wala usipunguze chochote ninachowaamuru ninyi, ila myashike maagizo ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ambayo nawapa. Mliona kwa macho yenu wenyewe kile Mwenyezi Mungu alichokifanya kule Baal-Peori. Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliwaangamiza kutoka miongoni mwenu kila mmoja aliyemfuata Baali wa Peori, lakini ninyi nyote mlioshikamana na Mwenyezi Mungu kwa uthabiti, Mungu wenu, mko hai hadi leo. Tazama, nimewafundisha amri na sheria kama Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, alivyoniamuru mimi, ili mzifuate katika nchi mnayoiingia kuimiliki. Zishikeni kwa uangalifu, kwa kuwa hii itaonesha hekima na ufahamu wenu kwa mataifa, ambayo yatasikia kuhusu amri zote hizi, nao watasema, “Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na ufahamu.” Ni taifa gani jingine lililo kubwa kiasi cha kuwa na miungu yao iliyo karibu nao kama Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, alivyo karibu nasi wakati wowote tunapomwomba? Nalo ni taifa gani jingine lililo kubwa hivi lenye kuwa na amri na sheria za haki kama hizi ninazoweka mbele yenu leo?