Kumbukumbu 27:9-16
Kumbukumbu 27:9-16 NENO
Kisha Musa na makuhani, ambao ni Walawi, wakawaambia Israeli wote, “Nyamaza ee Israeli, sikiliza! Sasa umekuwa taifa la Mwenyezi Mungu, Mungu wako. Mtii Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na kufuata amri zake na maagizo ninayokupa leo.” Siku ile ile Musa akawaagiza watu: Mtakapovuka Mto Yordani, makabila haya yatasimama juu ya Mlima Gerizimu kubariki watu: Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari, Yusufu na Benyamini. Makabila haya yatasimama juu ya Mlima Ebali kwa kutamka laana: Reubeni, Gadi, Asheri, Zabuloni, Dani na Naftali. Nao Walawi watawasomea watu wote wa Israeli kwa sauti kubwa: “Alaaniwe mtu afanyaye sanamu ya kuchonga au mwenye kusubu sanamu, kitu ambacho ni chukizo kwa Mwenyezi Mungu, kazi ya mikono ya fundi stadi, na kuisimamisha kwa siri.” Kisha watu wote watasema, “Amen!” “Alaaniwe mtu amdharauye baba yake na mama yake.” Kisha watu wote watasema, “Amen!”