Danieli 11:36-45
Danieli 11:36-45 NENO
“Mfalme atafanya apendavyo. Atajikweza na kujitukuza juu ya kila mungu, naye atasema mambo ambayo hayajawahi kusikiwa dhidi ya Mungu wa miungu. Atafanikiwa hadi wakati wa ghadhabu utimie, kwa maana kile kilichokusudiwa lazima kitatukia. Hataonesha heshima kwa miungu ya baba zake au kwa yule aliyetamaniwa na wanawake, wala hatajali mungu yeyote, bali atajikweza mwenyewe juu yao wote. Badala ya kuwajali miungu, ataheshimu mungu wa ngome; mungu ambaye hakujulikana na baba zake ndiye atamheshimu kwa dhahabu na fedha, kwa vito vya thamani, na zawadi za thamani kubwa. Atashambulia ngome zenye nguvu mno kwa msaada wa mungu wa kigeni, naye atawaheshimu sana wale watakaomkubali yeye. Atawafanya watawala wa watu wengi, na atagawa nchi kwa gharama. “Wakati wa mwisho, mfalme wa Kusini atapigana naye vita, naye mfalme wa Kaskazini atamshambulia kwa magari ya vita, askari wapanda farasi, na idadi kubwa ya meli. Atavamia nchi nyingi na kuzikumba nchi hizo kama mafuriko. Pia ataivamia Nchi ya Kupendeza. Nchi nyingi zitapinduliwa, bali Edomu, Moabu, na viongozi wa Amoni wataokolewa kutoka mkono wake. Atapanua mamlaka yake juu ya nchi nyingi; hata Misri haitaepuka. Atamiliki hazina za dhahabu na fedha na utajiri wote wa Misri, huku Walibia na Wakushi wakijisalimisha kwake. Lakini taarifa kutoka mashariki na kaskazini zitamshtua, naye ataondoka kwa ghadhabu nyingi ili kuangamiza na kuharibu wengi kabisa. Atasimika mahema yake ya ufalme kati ya bahari na mlima mtakatifu wa kupendeza. Hata hivyo, atafikia mwisho wake, wala hakuna yeyote atakayemsaidia.