Danieli 11:36-45
Danieli 11:36-45 Biblia Habari Njema (BHN)
“ ‘Mfalme atafanya kama apendavyo. Atajitukuza na kujikweza kwamba yeye ni mkuu kuliko miungu yote, na kumkufuru Mungu wa miungu. Ataendelea kufanikiwa mpaka ghadhabu ifikie kikomo chake, kwani yaliyopangwa lazima yatimie. Mfalme huyo hataijali miungu ya wazee wake wala yule anayependwa na wanawake. Ataidharau miungu mingine yote, kwani atajiweka kuwa mkuu kuliko kila mmoja wao. Badala ya miungu hiyo atamheshimu mungu mlinzi wa ngome, ambaye wazee wake kamwe hawakumwabudu, atamtolea dhahabu, fedha na vito vya thamani, na zawadi za thamana kubwa. Atazishughulikia ngome zake kwa msaada wa mungu wa kigeni. Wale wanaomtambua kuwa mfalme, atawatunukia heshima kubwa, atawapa vyeo vikubwa na kuwagawia ardhi kama zawadi. “ ‘Wakati wa mwisho mfalme wa kusini atamshambulia mfalme huyo wa kaskazini. Lakini mfalme wa kaskazini atajibu mashambulio hayo kwa nguvu kama kimbunga, akitumia magari ya farasi, wapandafarasi na meli nyingi. Atazivamia nchi nyingi na kupita katika nchi hizo kama mafuriko ya maji. Ataivamia hata nchi ile tukufu na kuua maelfu ya watu. Lakini nchi za Edomu, Moabu na sehemu kubwa ya Amoni, zitaokoka kutoka mikononi mwake. Wakati atakapozivamia nchi hizo, hata nchi ya Misri haitanusurika. Atamiliki hazina za dhahabu, fedha na vito vyote vya thamani vya nchi ya Misri. Watu wa Libia na watu wa Kushi watafuata nyayo zake. Lakini habari kutoka mashariki na kaskazini zitamtisha. Naye atatoka kwa hasira kubwa ili kukatilia mbali na kuangamiza wengi. Zaidi ya hayo, atapiga mahema yake makubwa kati ya bahari na mlima mtukufu na mtakatifu. Lakini atakuwa amefikia kikomo chake, na hatakuwapo yeyote wa kumsaidia.
Danieli 11:36-45 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye mfalme atafanya kama apendavyo; naye atajitukuza na kujiadhimisha juu ya kila mungu, naye atanena maneno ya ajabu juu ya Mungu wa miungu, naye atafanikiwa mpaka ghadhabu itakapotimia; maana yaliyokusudiwa yatafanyika. Wala hataijali miungu ya baba zake; wala yeye aliyetamaniwa na wanawake; wala hatamjali mungu awaye yote; maana atajitukuza mwenyewe juu ya wote. Lakini katika mahali pake atamheshimu mungu wa ngome; na mungu ambaye baba zake hawakumjua atamheshimu, kwa dhahabu, na fedha, na vito vya thamani, na vitu vipendezavyo. Naye ataziteka nyara ngome zenye nguvu kwa msaada wa mungu mgeni; na yeye atakayemkubali atamwongeza kwa utukufu; naye atawapa kumiliki wengi; naye ataigawa nchi kwa rushwa. Na wakati wa mwisho mfalme wa kusini atashindana naye; na mfalme wa kaskazini atamshambulia kama upepo wa kisulisuli, pamoja na magari ya vita, na wapanda farasi, na merikebu nyingi; naye ataingia katika nchi hizo, na kufurika na kupita katikati. Tena ataingia katika hiyo nchi ya uzuri, na nchi nyingi zitapinduliwa; lakini nchi hizi zitaokolewa na mkono wake, Edomu, na Moabu, na wakuu wa watu wa Amoni. Naye ataunyosha mkono wake juu ya nchi hizo, hata na nchi ya Misri haitaokoka. Lakini atakuwa na nguvu juu ya hazina za dhahabu na fedha, na juu ya vitu vyote vya Misri vyenye thamani; na Walibya na Wakushi watafuata nyayo zake. Lakini habari zitokazo mashariki na kaskazini zitamfadhaisha; naye atatoka kwa ghadhabu nyingi, ili kuharibu, na kuwaondolea mbali watu wengi. Naye ataweka hema zake za kifalme kati ya bahari na mlima mtakatifu wa uzuri; lakini ataifikia ajali yake, wala hakuna atakayemsaidia.
Danieli 11:36-45 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye mfalme atafanya kama apendavyo; naye atajitukuza na kujiadhimisha juu ya kila mungu, naye atanena maneno ya ajabu juu ya Mungu wa miungu, naye atafanikiwa mpaka ghadhabu itakapotimia; maana yaliyokusudiwa yatafanyika. Wala hataijali miungu ya baba zake; wala yeye aliyetamaniwa na wanawake; wala hatamjali mungu awaye yote; maana atajitukuza mwenyewe juu ya wote. Lakini katika mahali pake atamheshimu mungu wa ngome; na mungu ambaye baba zake hawakumjua atamheshimu, kwa dhahabu, na fedha, na vito vya thamani, na vitu vipendezavyo. Naye ataziteka nyara ngome zenye nguvu kwa msaada wa mungu mgeni; na yeye atakayemkubali atamwongeza kwa utukufu; naye atawapa kumiliki wengi; naye ataigawa nchi kwa rushwa, na wakati wa mwisho mfalme wa kusini atashindana naye; na mfalme wa kaskazini atamshambulia kama upepo wa kisulisuli, pamoja na magari ya vita, na wapanda farasi, na merikebu nyingi; naye ataingia katika nchi hizo, na kufurika na kupita katikati. Tena ataingia katika hiyo nchi ya uzuri, na nchi nyingi zitapinduliwa; lakini nchi hizi zitaokolewa na mkono wake, Edomu, na Moabu, na wakuu wa watu wa Amoni. Naye ataunyosha mkono wake juu ya nchi hizo, hata na nchi ya Misri haitaokoka. Lakini atakuwa na nguvu juu ya hazina za dhahabu na fedha, na juu ya vitu vyote vya Misri vyenye thamani; na Walibia na Wakushi watafuata nyayo zake. Lakini habari zitokazo mashariki na kaskazini zitamfadhaisha; naye atatoka kwa ghadhabu nyingi, ili kuharibu, na kuwaondolea mbali watu wengi. Naye ataweka hema zake za kifalme kati ya bahari na mlima mtakatifu wa uzuri; lakini ataifikilia ajali yake, wala hakuna atakayemsaidia.
Danieli 11:36-45 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
“Mfalme atafanya apendavyo. Atajikweza na kujitukuza juu ya kila mungu, naye atasema mambo ambayo hayajawahi kusikiwa dhidi ya Mungu wa miungu. Atafanikiwa hadi wakati wa ghadhabu utimie, kwa maana kile kilichokusudiwa lazima kitatukia. Hataonesha heshima kwa miungu ya baba zake au kwa yule aliyetamaniwa na wanawake, wala hatajali mungu yeyote, bali atajikweza mwenyewe juu yao wote. Badala ya kuwajali miungu, ataheshimu mungu wa ngome; mungu ambaye hakujulikana na baba zake ndiye atamheshimu kwa dhahabu na fedha, kwa vito vya thamani, na zawadi za thamani kubwa. Atashambulia ngome zenye nguvu mno kwa msaada wa mungu wa kigeni, naye atawaheshimu sana wale watakaomkubali yeye. Atawafanya watawala wa watu wengi, na atagawa nchi kwa gharama. “Wakati wa mwisho, mfalme wa Kusini atapigana naye vita, naye mfalme wa Kaskazini atamshambulia kwa magari ya vita, askari wapanda farasi, na idadi kubwa ya meli. Atavamia nchi nyingi na kuzikumba nchi hizo kama mafuriko. Pia ataivamia Nchi ya Kupendeza. Nchi nyingi zitapinduliwa, bali Edomu, Moabu, na viongozi wa Amoni wataokolewa kutoka mkono wake. Atapanua mamlaka yake juu ya nchi nyingi; hata Misri haitaepuka. Atamiliki hazina za dhahabu na fedha na utajiri wote wa Misri, huku Walibia na Wakushi wakijisalimisha kwake. Lakini taarifa kutoka mashariki na kaskazini zitamshtua, naye ataondoka kwa ghadhabu nyingi ili kuangamiza na kuharibu wengi kabisa. Atasimika mahema yake ya ufalme kati ya bahari na mlima mtakatifu wa kupendeza. Hata hivyo, atafikia mwisho wake, wala hakuna yeyote atakayemsaidia.