Amosi 6
6
Ole kwa wanaoridhika
1Ole wenu ninyi mnaostarehe na kuridhika katika Sayuni,
na ninyi mnaojisikia salama juu ya Mlima Samaria,
ninyi watu mashuhuri wa taifa lililoendelea kuliko mataifa mengine,
ambao watu wa Israeli wanawategemea!
2Nendeni Kalne mkaone kutoka huko;
mwende hadi Hamathi iliyo kuu,
kisha mshuke hadi Gathi ya Wafilisti.
Je, wao ni bora kuliko falme zenu mbili?
Je, nchi yao ni kubwa kuliko yenu?
3Mnaiweka mbali siku iliyo mbaya
na kuleta karibu utawala wa kuogofya.
4Ninyi mnalala juu ya vitanda vilivyofunikwa kwa pembe za ndovu,
na kujinyoosha juu ya viti vya fahari.
Mnajilisha kwa wana-kondoo wazuri
na ndama walionenepeshwa.
5Ninyi mnapiga vinubi kama Daudi,
huku mkitunga nyimbo za vinanda mbalimbali.
6Mnakunywa mvinyo kwa bakuli zilizojazwa,
na mnajipaka mafuta mazuri,
lakini hamhuzuniki kwa maangamizi ya Yusufu.
7Kwa hiyo mtakuwa miongoni mwa watu wa kwanza kwenda uhamishoni;
karamu zenu na kustarehe kutakoma.
Mwenyezi Mungu anachukia kiburi cha Israeli
8Bwana Mungu Mwenyezi ameapa kwa nafsi yake mwenyewe: Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, asema:
“Nachukia kiburi cha Yakobo,
nachukia ngome zake;
nitautoa mji wao na kila kitu
kilicho ndani yake.”
9Kama watu kumi watabaki katika nyumba moja, wao pia watakufa. 10Kama jamaa ambaye atachoma miili akija ili kuitoa nje ya nyumba, na kumuuliza yeyote ambaye bado anajificha humo, “Je, yuko mtu yeyote pamoja nawe?” Naye akisema, “Hapana,” ndipo atakaposema, “Nyamaza! Haturuhusiwi kutaja jina la Mwenyezi Mungu.”
11Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ameamuru,
naye atabomoa jumba kubwa vipande vipande
na nyumba ndogo vipande vidogo vidogo.
12Je, farasi wanaweza kukimbia
kwenye miamba iliyochongoka?
Je, mtu aweza kulima kwa maksai huko?
Lakini mmegeuza haki kuwa sumu
na matunda ya uadilifu kuwa uchungu:
13ninyi mnaoshangilia kushindwa kwa Lo-Debari
na kusema, “Je, hatukuteka Karnaimu
kwa nguvu zetu wenyewe?”
14Maana Bwana Mwenyezi Mungu,
Mungu wa majeshi ya mbinguni, asema,
“Nitainua taifa dhidi yenu, ee nyumba ya Israeli,
nalo litawatesa kuanzia Lebo-Hamathi
hadi Bonde la Araba.”
Iliyochaguliwa sasa
Amosi 6: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.